23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Coulibaly alivyobadilisha mitazamo ya mashabiki Simba

BADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

AKIBA ya maneno ni silaha kubwa sana hasa pale unapokosa uhakika wa jambo. Moja kati ya usajili uliofanywa na klabu ya Simba msimu huu na kuwakosha idadi kubwa ya mashabiki wake, ni ule wa raia wa Zambia, Clatous Chama.

Wengi walitamani kumjua nani alifanikiwa usajili wa Chama, hasa kutokana na kuonyesha kiwango cha juu katika baadhi ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Baada ya beki, Shomari Kapombe kuumia, Simba iliingia mtaani kusaka mbadala wake na ndipo ikainasa saini ya Zana Coulibaly, raia wa nchini Ivory Coast.

Kapombe aliumia huku akiwa kwenye kiwango cha hali ya juu, hivyo mashabiki wa Simba walikuwa na imani kwamba mbadala wa mchezaji huyo lazima afikie uwezo wa Kapombe au zaidi.

Michezo michache ya awali katika michuano ya Ligi Kuu ambayo mchezaji huyo alipewa nafasi ili kuwaonesha mashabiki wake kile alichonacho, wengi wao walimaliza akiba ya maneno, wachache sana ambao walibakiza maneno juu ya mchezaji huyo.

Wapo viongozi wa Simba ambao pia hawakuwa na imani na mchezaji huyo ambaye inadaiwa ana mkataba wa miezi sita ndani ya Wekundu hao wa Msimbazi.

Wapo mashabiki wa Simba ambao walikuwa wanasikika mitaani wakidai kuwa wamehujumiwa katika usajili wa mchezaji huyo.

Nadhani Coulibaly ambaye amekuwa akitumia lugha ya Kifaransa, usajili wake  Simba unahusishwa na beki mwingine wa timu hiyo raia wa Ivory Coast, Pascal Wawa.

Katika michezo hiyo ya awali, Coulibaly, alionekana kutokuwa fiti kwa mchezo, lakini kocha wa timu hiyo, Patrick Aussems, aliendelea kuwa na imani naye kwamba muda mwafaka utakapofika atakuwa na msaada mkubwa kwa kikosi chake.

Mchezo wa kwanza ambao alianza kuwashangaza mashabiki wa timu hiyo ni ule wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, uliochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

Awali, Simba walikubali kichapo cha mabao 5-0 kule nchini Misri, hivyo kuwapa wakati mgumu Simba kwenye uwanja wa nyumbani.

Katika mchezo huo wa marudiano mashabiki walikosa imani baada ya kumwona Coulibaly akiwa kwenye kikosi cha kwanza, hivyo wengi wao waliamini itakuwa njia kwa upande wake wa kulia ambao anacheza mchezaji huyo.

Lakini aliwashangaza mashabiki hao baada ya kuonesha kiwango cha hali ya juu tangu ajiunge na timu hiyo, pia ni yeye aliyepiga krosi iliyozaa bao la ushindi huo wa Simba dhidi ya Al Ahly wa bao 1-0.

Katika mchezo wa mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya Yanga SC, bado mashabiki wa Simba hawakuwa na imani naye tena, huku wakiamini wachezaji wa Yanga wenye kasi kama vile Mrisho Ngassa, wangeweza kupita kwa urahisi, lakini bado alikuwa imara na kuweza kuwadhibiti washambuliaji wa timu hiyo.

Mbali na kuwadhibiti wachezaji wa Yanga, lakini alikuwa na kazi kubwa ya kuongeza mashabulizi hasa kwa kupiga krosi mara kwa mara.

Coulibaly ni yeye ambaye aliwainua mashabiki wa Simba pale alipompiga chenga beki wa kati wa Yanga, Abdallah Shaibu (Ninja) na kumwacha akiwa ameanguka chini kisha kupiga krosi.

Baada ya mchezo huo, Simba sasa wameanza kuwa na imani na mchezaji huyo kutokana na kile alichokionesha kwenye michezo miwili iliyopita.

Coulibaly si mchezaji wa kwanza kutiliwa shaka kipaji chake baada ya kusajiliwa katika Ligi ya Tanzania Bara, Obrey Chirwa naye alikuwa mmoja kati ya wachezaji wa aina hiyo ambaye alitiliwa shaka kiwango chake hasa katika michezo kadhaa ya mwanzo.

Mshindi wa tuzo ya Ballon d’Or mwaka jana, Luka Modric, alikuwa mmoja kati ya wachezaji ambao walikuwa wanazungumzwa vibaya katika Ligi ya Hispania baada ya kujiunga akitokea England katika klabu ya Tottenham.

Lakini kwa sasa mchezaji huyo anatajwa kuwa kiungo bora nchini Hispania hasa kutokana na kuisaidia klabu yake ya Real Madrid kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa mara tatu mfululizo pamoja na kuifikisha Croatia fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana nchini Urusi.

Mchezaji mwingine ambaye alikuwa na wakati mgumu kwa mashabiki baada ya kusajiliwa ni Thierry Henry, alipojiunga na Arsenal akitokea Juventus mwaka 1999, mchezaji huyo alicheza michezo nane bila ya kufunga bao, lakini sasa ni mmoja kati ya wachezaji walioacha historia ya upachikaji mabao ndani ya kikosi hicho.

Bado Coulibaly anahitaji muda zaidi ndani ya klabu ya Simba kwa ajili ya kuonyesha ubora wake, tunatakiwa kuwa na akiba ya maneno ingawa itabidi afanye kazi ya ziada ili kumweka benchi Kapombe ambaye anapokuwa fiti uwezo wake uwanjani huwa si wa kutiliwa shaka.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles