Edward Kondela-BARIADI
SERIKALI imewataka wafugaji nchini kubadili fikra zao na kutambua umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi kujiepusha na mkono wa sheria i wanapoingiza mifugo yao katika hifadhi na mapori ya akiba.
Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Profesa Elisante ole Gabriel alikuwa akizungumza na baadhi ya wafugaji katika Wilaya ya Meatu, mkoani Simiyu juzi.
Alisema baadhi ya wafugaji wamekuwa wakiingiza mifugo yao katika hifadhi na mapori ya akiba.
Alisema hali imekuwa ikisababisha kutokuwapo uhusiano mzuri kati yao na wahifadhi kwa madai ya kuonewa ilhali wahifadhi hao wanatakeleza sheria za nchi.
“Tunatamani fikra za wafugaji wote nchini zibadilike na zianze kutambua umuhimu wa kufuata sheria, taratibu na kanuni, ndiyo msingi wa mafaniko.
“Niwaombe wafugaji wote nchini watambue kwamba Wizara ya Mifugo na Uvuvi itapenda wafugaji wafuate sheria, taratibu na kanuni, tukifanya hivyo tutakuwa marafiki wa wizara unapokuwa mhalifu unakuwa tena siyo mfugaji bali unakuwa mhalifu,” alisema Profesa Gabriel.
Katibu Mkuu huyo alilazimika kukutana na wafugaji hao kutokana na hivi karibuni ng’ombe kukamatwa katika Pori la Akiba la Maswa.
Wamiliki wa ng’ombe hao walikiri kufanya kosa na kulipa faini waliyotozwa na mahakama baada ya kutiwa hatiani.
“Hivi karibuni ng’ombe walikamatwa katika Pori la Akiba la Maswa, ndipo busara ikatumika kuona jambo hilo linafikia tamati ambako wahusika wamekabidhiwa ng’ombe zao kwa kuwa busara imetumika na siyo kwamba wao wameshinda.
“Kwa mujibu wa sheria wenzetu wa hifadhi wanachofanya ni kusimamia Sheria Namba Tano ya Mwaka 2009 ya Hifadhi ya Wanyamapori kwamba mifugo ikikamatwa inaweza kutaifishwa,” alisema Prof. Gabriel.
Awali akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu kabla ya kuzungumza na wafugaji hao, Prof. Gabriel aliwashukuru madiwani wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Juma Mpina, kwa uelewa wa hali ya juu baada ya Meneja wa Pori la Akiba la Maswa, Lusato Masinde kutoa elimu na sheria iliyotumika na uamuzi uliotolewa na mahakama kwa wafugaji waliyoingiza mifugo katika Pori la Akiba la Maswa.
Alisema kunapaswa kuwapo mawasiliano mazuri kati ya viongozi na jamii ya wafugaji katika maeneo yote nchini kujenga uhusiano mzuri na kuelewa majukumu ya wasimamizi wa hifadhi na mapori ya akiba ambao wamekuwa wakisimamia sheria na hawapo kwa ajili ya kumuonea mtu yeyote.
Katika kikao na wafugaji, Prof. Gabriel, aliwataka wasijichukulie sheria mkononi hata wanapokuwa wamepishana kauli na wasimamizi wa sheria kama ambavyo imekuwa ikijitokeza katika maeneo mbalimbali nchini ambako amebainisha kuwa kwa kufanya hivyo ni kosa kubwa katika sheria.
Awapongeza wafugaji wa Wilaya ya Meatu kwa kuwa watulivu na kuonyesha ushirikiano kwa maofisa wa Pori la Akiba la Maswa baada ya kuingiza mifugo yao katika pori hilo kinyume na sheria na kutii hatua za sheria zilizochukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na wafugaji katika kuhakikisha sekta ya ufugaji inaboreka katika maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Wilaya ya Meatu, Prof. Gabriel, alisema wizara inahakikisha kwa juhudi zote inaboresha sekta ya ufugaji nchini yakiwamo malisho bora kwa kuwapo shamba darasa katika wilaya hiyo na maeneo mengine.