22.7 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

Watu 207 walipuliwa kanisani

  • Walikuwa kwenye ibada ya Pasaka nchini Sri Lanka

Colombo, Sri Lanka

WATU 207 wameuawa na wengine 450 kujeruhiwa katika mashambulio ya mabomu dhidi ya makanisa na hoteli nchini Sri Lanka.


Milipuko minane iliripotiwa katika mashambulio dhidi ya makanisa matatu katika miji ya Kochchikade, Negombo na Batticaloa ambayo yalishambuliwa wakati wa ibada ya Pasaka.


Pia hoteli za The Shangri La, Cinnamon Grand na Kingsbury ambazo zipo mjini Colombo zililengwa katika mashambulio hayo.
Jumapili ya Pasaka ni moja ya siku kuu muhimu katika kalenda ya waumini wa dini ya Kikristo. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kujihusisha na mashambulio hayo.


Mashambulio hayo yamesababisha kuibuka kwa hofu na huenda wapiganaji wa kundi la Islamic State waliorejea kutoka Mashariki ya Kati wakawa tishio kwa usalama wa nchi hiyo.
Amri ya kutotoka nje imewekwa kuanzia saa 12.00 jioni hadi saa 12.00 asubuhi kuanzia jana kwa saa za Sri Lanka.


Serikali pia imetangaza kuwa itadhibiti matumizi ya mitandao yote ya jamii kwa muda kama njia ya kukabiliana na watu waliohusika na mashambulio hayo.
Kanisa la St Sebastian mjini Negombo limeharibiwa vibaya na milipuko hiyo.


Pia kumeripotiwa idadi kubwa ya watu waliyojeruhiwa katika Kanisa la St. Anthony mjini Kochchikade, ambao ni moja ya wilaya ya Colombo.
Raia tisa wa mataifa ya kigeni ni miongoni mwa watu waliouawa mjini Colombo, kwa mujibu wa vianzo vya hospitali vilivyozungumza na Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC.


Pamoja na hali hiyo vyanzo hivyo mjini Batticaloa vimesema kuwa karibu watu 27 wamefariki dunia mjini humo.
Ofisa wa Hoteli ya Cinnamon Grand ambayo ipo karibu na makazi rasmi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa, AFP kuwa mtu mmoja alifariki dunia kutokana na mlipuko huo.

KAULI ZA VIONGOZI
Rais Maithripala Sirisena, ametoa tarifa ya kuwaomba wananchi kuwa watulivu na kuwasaidia maofisa wake katika uchunguzi.
Naye Waziri Mkuu Ranil Wickremesinghe ambaye anaongoza mkutano wa dharura alisema, “Nalaani vikali shambulio la watu wetu leo. Natoa wito kwa Wa -Sri Lanka wote kuungana wakati huu mgumu.”


Katika mtandao wake wa Twitter, Waziri wa Fedha, Mangala Samaraweera aliandika kuwa mashambulio haya yamepangwa na kutekelezwa ili, “Kuua watu, kusababisha taharuki na kugonganisha watu na yamesababisha vifo vya watu wengi wasiokua na hatia.”


Waziri mwingine , Harsha de Silva, amesema mashambulio hayo ni ya kuogopesha, “Nimeona hali ya kusikitisha katika Kanisa la St. Anthony Shrine mjini Kochchikade. Nimeona vipande vya miili ya watu iliyotapakaa kila sehemu.”

HISTORIA YA SRI LANKA
Tangu mapigano ya wenyewe kwa wenyewe kukomeshwa mwaka 2009, kumeripotiwa ghasia kwa miaka kadhaa nchini Sri Lanka.
Waumini wa Budha wamekua wakishambulia misikiti na mali inayomilikiwa na waumini wa dini ya Kiislamu, hali ambayo ilisababisha kutangazwa hali ya hatari Machi mwaka 2018.


Mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yalimalizika baada ya wapiganaji wa kundi la Tamil Tigers kushindwa.
Kundi hilo lilipigania uhuru wa jamii ya Tamil walio wachache kwa miaka 26. Mapigano hayo yanakadiriwa kusababisha vifo vya watu kati ya 70,000 na 80,000


Sri Lanka inakadiriwa kuwa na idadi ya wakazi takriban milioni 20.
Walio wengi ambao ni asilimia 74.9 ni Wasinhala ambao kwa kawaida ni wafuasi wa Ubuddha wa madhehebu ya Theravada. Takriban asilimia 11.2 ni Watamili ambao wengi wao ni Wahindu na wanaishi hasa kaskazini mwa kisiwa hicho.


Lugha zao ni Kisnhala na Kitamil ambazo ni lugha rasmi. Pia Kiingereza kinatambulika.
Pia wapo Wamori Waislamu asilimia 10 ambao ni Wasuni, wengi wao wanajiona machotara wa Kiarabu. Pia kuna Wakristo asilimia saba huku Wakatoliki wakiwa 5.6 na waliobaki ni Waanglikana na Waprotestanti.
Karibu wananchi wote wanajali na kuthamini dini katika maisha yao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,580FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles