28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

Tuendelee kupiga vita ajira za watoto

Na SAMWEL MWANGA-SIMIYU
PAMOJA na wanaharakati wa haki za binadamu nchini kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu, bado kuna ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto.

Kwa miaka mingi nchini haki za watoto zimekuwa zikikiukwa hasa katika suala la kuwatumikisha katika ajira mbalimbali ambazo haziendani na umri wao kisheria.

Watoto wengi wamekuwa wakitumikishwa katika ajira mbalimbali ambazo zinawaathiri kisaikolojia na hata makuzi ya watoto hao.

Ibara ya 1 ya Mkataba wa Umoja wa Kimataifa wa haki za mtoto 1989 (CRC), imetoa tafsiri ya mtoto ikiwa na maana kuwa ni binadamu yeyote aliye na umri chini ya miaka 18, isipokuwa kama sheria inayotumika inatambua umri wa utu uzima kabla ya hapo.

Hakuna maana ya moja kwa moja ya maana ya mtoto isipokuwa maana hiyo hutegemea mazingira itakayotumika.

Ajira za watoto ni kuwatumikisha watoto walio chini ya miaka 18, kufanya kazi ambazo hawastahili kuzifanya kutokana na umri wao kwani zinawadhoofisha na zinahatarisha maisha yao.

Mkataba wa 182 wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) 1999, unatanabaisha kuhusu mifumo mibaya zaidi ya ajira ya watoto katika ibara ya 3, umetoa tafsiri ya ajira za watoto ni kazi zozote zinazoweza kudhuru afya, usalama na maadili ya watoto.
Ajira za watoto ni jambo linalopigwa vita dunia nzima kutokana na ukweli kwamba ni kazi zinazohatarisha makuzi ya mtoto na kumuweka
katika hatari au hali tete na kumsababishia maisha mabovu mbeleni.

Watoto wana haki kama watu wazima na wanahitaji taratibu za kipekee ili haki hizo ziheshimiwe. Ibara ya 32 ya mkataba wa Umoja wa Mataifa wa haki za mtoto CRC 1989 ambao Tanzania imeuridhia mkataba huo Desemba 2,1990, inasema na kusisitiza “kila  mtoto ana haki ya kulindwa dhidi ya unyonyaji wa kiuchumi na kufanya kazi yoyote ambayo inaweza kutatiza elimu, ama kuwa na madhara kwa afya au maendeleo ya kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii’.

Pamoja na kuwepo kwa mikataba mbalimbali ya kuwalinda watoto dhidi ya utumikishwaji na udhalilishwaji, tatizo hili linaongezeka kwa kasi na
watoto kujikuta wakikosa haki zao za msingi kama kucheza, kupata elimu, kutunzwa na kulindwa.

Kutokana na kushamiri kwa ajira za watoto hapa nchini ambapo baadhi ya wananchi katika jamii zetu wanatumia nafasi hiyo kuwapa ajira ngumu
watoto walio chini ya umri wa miaka 18, sheria inawatambua kuwa bado ni watoto.

Mfano wa ajira hizo ni kufanya biashara, kuponda kokoto, kufanya kazi za nyumbani, kusukuma matoroli na mikokoteni ya mizigo, kuchunga mifugo, kuchota maji, kushusha mizigo kwenye magari yanayoleta bidhaa kwa wafanyabiashara nakadhalika.

Kimsingi haimaanishi kwamba mtoto asifanye kazi yoyote kabisa, hivyo shughuli za nyumbani ni muhimu mtoto kushiriki kwa vile kazi ni sehemu
ya makuzi ya binadamu.

Ajira kwa watoto inayokatazwa ni ile yenye uwezekano wa kumnyima mtoto haki yake ya elimu, kimakuzi katika maeneo ya saikolojia, kimwili, kihisia, kiakili na kimaendeleo.

Kwa vile watoto bado wana akili changa, hufanya maamuzi ambayo huhatarisha maisha yao wakiwa katika ajira, hupenda kujaribu mambo mbalimbali na hata yale ya hatari na hivyo hujikuta wakiumia pale pale au baada ya kipindi kirefu madhara ya kiafya hujitokeza.

Kuna watoto ama kwa kulazimishwa na wazazi/walezi wao au kwa kujishauri wenyewe, hufanya biashara mbalimbali ili wajipatie fedha
kwa matumizi yao.

Watoto wa kike nao wamekuwa wakibeba majukumu makubwa ya kifamilia kuliko uwezo wao, ukilinganisha na wenzao wavulana, wasichana ndio wahudumu wakuu katika majumba ya watu tofauti, licha ya kulipwa ujira
mdogo wamekuwa wakikabiliana na vitendo vingi viovu ikiwemo kunyanyaswa kijinsia.

Ajira hizi za watoto zimekuwa zikihusisha kuwapatia shughuli ambazo ni
nzito sana kwa umri wao. Kama hii haitoshi bado shughuli hizi zinakuwa katika mazingira magumu na yasiyofaa kwa afya ya mwanadamu yeyote. Na
bila kusahau kuna mamilioni ya watoto wanaofanyishwa kazi ambazo hazifai kwa hadhi ya utu.

Ajira za watoto zinastahili kupigwa vita kila kona duniani kutokana na ukweli kwamba kwa kutumia umri wao mdogo, waajiri wa watoto hawa huwadanganya na kuwalipa kiasi kidogo sana cha ujira na mara nyingine kutowalipa kabisa.

Ajira za watoto huwa kikwazo kikubwa katika ukuaji wa kimwili, kimaono na kijamii. Ni kutokana na ukweli huu kwamba, athari za ajira za
watoto ni kubwa mno, watoto wanaathirika kimwili, kisaikolojia, wanakosa haki zao za msingi na mambo mengine mengi, miongoni mwa hayo ni kukosa elimu.

Watoto wengi wanaojiingiza katika ajira za utotoni wanakosa haki yao ya msingi ya kielimu kutokana na ukweli kwamba muda wa kuwepo katika
masomo wao wapo katika ajira.

Watoto wanaathirika sana kisaikolojia pamoja na kiafya. Huko kwenye ajira hujifunza na kuiga mambo mengi kama uvutaji bangi, utumiaji wa
dawa za kulevya na tabia mbalimbali zisizoendana na utamaduni wetu.

Kutokana na watoto kujifunza mambo tofauti wakiwemo kwenye ajira kama vile utumiaji wa dawa za kulevya, hali hii inapelekea ongezeko la watumiaji wa dawa hizo.

Kuongezeka kwa mimba za utotoni. Kuna baadhi ya watoto wa kike ambao huajiriwa kwenye klabu za usiku, ajira ambayo inahatarisha usalama wa
watoto na kupelekea kudhalilishwa kijinsia.

Kuongezeka kwa vifo vya watoto. Kuna watoto ambao huajiriwa katika migodi, ajira ambayo ni hatari kwa watoto, kuna baadhi ya watoto hupoteza maisha yao kwa kuangukiwa na mwamba wa mawe.

Hivyo ni vizuri wazazi/walezi na Serikali kwa pamoja wafuatilie kwa kina ustawi wa watoto na vile vile kuweza kuwadhibiti wale wote wanaowatumikisha watoto kwa masilahi yao binafsi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles