28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Samia kumrithi JPM 2025?

JAVIUS KAIJAGE

Ni wazi kwamba kutokana na mchakato wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kumpata mpeperusha bendera kuwa mrefu, wakati mwingine hupelekea kuwa vigumu kumbaini mhusika atakayeibuka kidedea.     

Nasema huwa ni vigumu kumbaini mpeperusha bendera wa chama hicho kikongwe nchini, kwani historia yake katika baadhi ya matukio inaonyesha hivyo.       

Katika uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1995, jina la Benjamin Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu), ambaye kimsingi pamoja na kuwa aliwahi kuwa mwandishi wa habari wa Mwalimu Nyerere huku akishika nyadhifa mbalimbali za uongozi kitaifa na kimataifa, lakini hakupewa kipaumbele jambo la  kushangaza ndiye aliyepitishwa katika mchujo wa mwisho.        

Miaka kumi baadaye wakati CCM ikijiandaa kumpata mpeperusha bendera mpya mara baada ya Mkapa kukamilisha muda wake kikatiba,  Jakaya Kikwete (Rais wa Awamu ya Nne) alipewa nafasi kubwa na akaibuka kidedea japo inasemekana palikuwepo na mizengwe kadhaa kwa baadhi ya wagombea akiwemo Dk. Salim Ahmed Salim.        

Baada ya miaka kumi ya Kikwete, huku CCM ikionekana kuyumba na kuporomoka umaarufu wake kutokana na harufu ya ufisadi na rushwa huku ndani yake pakiibuka makundi, hatimaye wazee akina Mkapa na Ali Hassan Mwinyi (Rais wa Awamu ya Pili )waliamua kumwibua Rais wa sasa, Dk. John Magufuli kama njia mojawapo ya kukinusuru chama kwani ndiye mwanasiasa aliyeonekana angalau ana mikono safi ukilinganisha na wengine.          

Hata hivyo pamoja na ugumu wa kubashiri mpeperusha bendera wa CCM mara baada ya JPM kung’atuka, bado Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kasimu Majaliwa wanaanza kuzungumzwa katika vinywa vya watanzania kwamba wanafaa kuvivaa viatu vya mzee wa ‘‘HAPA KAZI TU’’         

Katika wanasiasa hawa wawili wanaoanza kumezewa mate kuwa wanaweza kulivusha taifa katika bahari ya Sham, kwanini Samia Suluhu Hassan?           

Samia anawekwa katika mizani ya Urais wa 2025  ukizingatia yeye ni mwanamke kwani historia ya nchi yetu inaonyesha kuwa tangu kupata uhuru kwa serikali zote kwa maana ya serikali ya Tanganyika iliyo ndani ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, hakuna mwanamke aliyewahi kuwa Rais na Amiri Jeshi mkuu.          

Ni Samia kwa sababu yeye ni Mzazibari. Ni dhahiri Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hakuna kipengele cha kupokezana madaraka katika pande hizi mbili za Muungano, lakini yafaa ikumbukwe kwamba tangu kuasisiwa kwa Muungano mwaka 1964,  Zanzibar imebahatika kumtoa Rais mmoja wa Muungano na hivyo kuendelea kuibuka manung’uniko kwamba hakuna haki na usawa.         

Ni Samia anayeweza kuirithi mikoba ya JPM kutokana na yeye kuwa mwislam. Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache yasiyoendekeza masuala ya udini na ukabila.

Lakini saikolojia ya mwanadamu katika kuendelea kudai kutimiziwa haki na usawa iko palepale na ndiyo maana ukifuatilia kwa ukaribu hata michakato ya nyuma katika kumpata mgombea wa CCM  imekuwa ikiwa makini.          

Awamu ya kwanza ilikuwa ni ya Mkristo, ya pili Mwislamu, ya tatu Mkristo, ya nne Mwislamu na hatimaye ya tano ambayo iko madarakani ni ya Mkristo.         

Si tu Samia kuwa mwanamke, mzanzibari na mwislamu vinampa nafasi ya kuwa kiongozi mkuu wa nchi, bali pia mwanasiasa huyu mbali na kuwa na uzoefu katika masuala ya uongozi lakini inasemekana ni msikivu na mwenye huruma.        

Hata hivyo Tanzania hahitaji uislamu/ukristo, uzanzibari/uzanzibara katika kumpata Rais, lakini si vibaya ikimpata mwanamke kama ataonekana kuwa na sifa stahiki kwa mujibu wa katiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles