26.9 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Mwanafunzi aliyepooza akikata fimbo aanza matibabu

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

AMOS Gabriel, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari  Samora Machel  Mbeya, ambaye sasa amekuwa mlemavu kutokana na kuanguka kutoka juu ya mti, amesimulia maumivu na mateso anayopitia kutokana na kuvunjika uti wa mgongo.

Akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalum katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) jana, Amos alisema anatamani kurejea shuleni kuendelea na masomo ingawa kwa sasa ni vigumu.

“Natamani kurudi shuleni lakini shida iliyopo ni kwamba nani atanisaidia kule shuleni, mimi hapa nilipo sasa hivi sina hisia yoyote, siwezi kuzuia haja ndogo wala kubwa.

“Sasa nikienda shuleni na hali hiyo ikanitokea  itakuwaje, nani atanisaidia?

“Watu watanitenga… kwa kweli najisikia vibaya mno ninapotafakari, nipo nyumbani lakini kule shuleni wenzangu wanaendelea na masomo,” alisema.

Akisimulia jinsi mkasa huo ulivyotokea, alisema siku hiyo mwalimu wao aliingia darasani na kuwaeleza walikuwa wameshindwa  mtihani wake hivyo aliagiza yeye na mwenzeke waende kutafuta fimbo za kuwaadhibu.

“Tulitoka nje na mwenzangu kwenda kutafuta fimbo tulizoagizwa, tulitafuta maeneo ya chini, tukakosa, nikamwambia mimi nipande juu ya mti uliokuwapo eneo hilo ili nikate.

“Nilimwambia tukichelewa kurudi mwalimu atatugombeza, atasema tumechelewa makusudi, mti ule ulikuwa ni mrefu mithiri ya mwembe mkubwa… nilipanda nikafanikiwa kuzikata fimbo kadhaa, nikageuka ili nishuke chini.

“Lakini nilipogeuka ghafla niliteleza, nikadondoka, niliangukia kichwa sehemu ya nyuma, nijitahidi kujizuia ili mgongo wangu usiumie, nilijigonga shingo, nikajikuta tayari mgongo wangu nao umegonga chini, nilihisi maumivu makali,” anasimulia.

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa MOI, Dk. Nicephorus Rutabasibwa ambaye ndiye anayemuhudumia mtoto huyo alisema Amos aliumia kwa kiwango kikubwa.

“Kutokana na kuumia uti wa mgongo kwa kiasi kikubwa hivi sasa miguu ya Amos imekosa nguvu kuanzia eneo la kifuani kuelekea chini ya mwili wake, ndiyo maana hawezi kusimama na kutembea,” alisema.

Alisema matatizo ya uti wa mgongo yakitokea mara nyingi kwa bahati mbaya ngozi huwa haihisi kama kuna maumivu.

“Ndiyo maana alipata vidonda vinamsumbua sehemu ya nyonga, tunachofanya sasa ni kumsafisha vidonda vilivyomtoka, tunatarajia baada ya wiki moja hadi mbili atakuwa amepona, tutawasiliana na wataalamu wenzetu (plastic surgeon) wa Muhimbili   wamfanyie upasuaji wa kupandikiza ngozi,” alisema.

Asaidiwa kiti

Mwananchi mmoja, Genister Masawe alisema yeye na familia yake waliguswa na kumsaidia kiti cha kutembelea kijana huyo baada ya kuona picha yake iliyorushwa mtandaoni.

“Binti yangu mmoja aliiona akaiweka katika group la WhatsApp la familia, basi tukaguswa, tukajikusanya na kununua kiti hiki…bahati nzuri nikaambiwa leo anakuja kliniki hapa Muhimbili, hivyo nimemkukabidhi,” alisema.

Mama mzazi wa Amos  ambaye ni mkazi wa Mbagala, Swaumu Sesema,  alishukuru familia hiyo kwa msaada huo waliompatia.

“Tangu Juni  mwaka huu hadi sasa ametumia zaidi ya Sh milioni tisa kumtibu, namshukuru Naibu Spika kwa kunisaidia kumpata Dk. Ruta.

“Alisema atahakikisha anafanya kila awezalo aweze kurejea hali nzuri aweze kwenda shule kuendelea na masomo yake,” alisema.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo ambaye alifika hospitalini hapo kumjulia hali Amos, alikataa kuzungumza na MTANZANIA.

Alisisitiza   amekwenda kufuatilia mchakato wa kumkatia bima ya afya mwanafunzi huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles