30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Kesi ya kumhonga Lukuvi yazidi kuunguruma

 KULWAMZEE -DAR ESSALAAM 

SHAHIDI wanne wa Jamhuri, Kamishna Msaidizi wa Ardhi, Mathew Nhonge amedai Mkurugenzi wa Kampuni ya Kiluwa Steal Group Co.ltd na Kiluwa Free Processing Zone, Mohamed Kiluwa (50) anayedaiwa kutoa rushwa ya Sh milioni  90 kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, alipata hati za viwanja 70 kwa halali. 

Anadai baada ya tuhuma hizo  alifutiwa usajiliwa hati zote 70 lakini mahakama ikiamua vinginevyo hakuna atakayebisha. 

Hayo yalidaiwa jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala mbele ya Hakimu Mkazi, Samweli Obas wakati shahidi huyo akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili waSerikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), MaghelaNdimbo.

Akitoa ushahidi, Mathew alidai Kampuni ya Kilua iliomba kumiliki ardhi maeneo ya Kikongo Kibaha,  hati za kumiliki viwanja 73 zilimfikia kwa ajili ya kuzisaini. 

Alidai kati ya hati hizo zilisainiwa 70 kisha kupelekwa kwa msajili wa hati na hati tatu hazikusainiwa kwa sababu kulikuwa na upungufu.

Baada ya hati hizo kusainiwa shahidi anadai alipigiwa simu na Waziri Lukuvi Julai 13 mwaka huu akimuelekeza amfahamishe Kilua aende ofisini kwake akiwa na hati zake. 

Anadai ujumbe huo alimfikishia Shabani na Kilua aliupata,  Julai 16 mwaka huu alienda ofisini kwa waziri ambaye alitaka hati hizo ziongezewe masharti hasa katika uwekezaji wa viwanda.

Mathew anadai  Kilua alifika kwa waziri baada ya kukutana naye mapokezi ya kwenda ofisini kwa waziri kati ya saa nne mpaka saa sita. 

“Sikujua kilichondelea mpaka niliposikia kwa watumishi wa wizara kwamba Kilua kakamatwa kwa rushwa.

“Kutokana na suala la rushwa hati zote zilifutwa katika usajili chini ya kifungu namba 178 cha sheria ya ardhi namba nne,”alidai na kuongeza kwamba kifungu hicho hakiwaelekezi kupeleka hoja mahakamani kabla ya kuzifuta. 

Akihojiwa na wakili wa utetezi, Imani Madega, shahidi huyo alidai viwanja vyote vilipimwa na ardhi hiyo aliomba katika halmashauri kwa utaratibu wa kawaida. 

Anadai hati zote zilizosainiwa kila kitu kilikuwa sawa sawa na aliridhika nazo ndiyo sababu alisaini. 

Alipohojiwa kama katika hatua hizo alimuomba fedha mshtakiwa, alikana kupewa wala kuomba fedha kwa Kilua. 

Anadai hakuona wakati rushwa hiyo ikitolewa, hati mshtakiwa alizipata kwa halali na kwamba endapo mahakama itaamua vinginevyo wizara haitabisha.

Mshtakiwa huyo ambaye yupo nje kwa dhamana, anakabiliwa na shtaka moja la kujihusisha na vitendo vya rushwa.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa Julai 16  mwaka huu kati ya saa 6 na saa 8 mchana  akiwa Mkurugenzi wa kampuni hizo mbili alitoa rushwa ya Dola za Marekani 40,000 (Sh milioni 90) kwa Waziri Lukuvi.

Mshtakiwa anadaiwa kutoa  fedha hizo kwa lengo  kwamba asiwasilishe hati ya umiliki wa kiwanja namba 57 Block B Kikongo na D Disunyura kilichopo eneo la viwanda Kibaha mkoani Pwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles