29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Machinjio ya nyama Bariadi ni hatari kwa afya


NA DERCK MILTON

MOJA ya jukumu kubwa la Mamlaka ya Chakula na Dawa nchini (TFDA), ni kulinda afya ya watumiaji wa vyakula, dawa na vipodozi.

Sehemu za machinjio ya nyama zilianzishwa kwa maksudi na serikali ili kuhakikisha kitoweo hicho kinachoandaliwa huko na kupelekwa kwa walaji kinakuwa salama na bora.

Usalama na ubora wa nyama inayotolewa kwenye machinjio ya Halmashauri ya Mji wa Bariadi mkoani Simiyu, unaelezwa na watalaamu wa afya kuwa haupo salama kwani mazingira ya uandaaji wa kitoweo hicho si salama tena.

TFDA kama mamlaka husika hawaHitaji ushahidi mkubwa zaidi ya huu ambao aliutoa Ofisa Afya wa Mkoa wa Simiyu, Reuben Malima kwenye gazeti hili wiki iliyopita ambapo alieleza tishio la magonjwa ya mlipuko yanayoweza kutokea wakati wowote kwa kula nyama inayoandaliwa kwenye machinjio hayo.

Kwenye habari hiyo, Malima anasema kuwa machinjio ya nyama Bariadi, hayastahili kuitwa tena machinjio kutokana na kuwapo ukikwaji mkubwa wa kanuni na taratibu za uchinjaji.

Katika maelezo yake, anasema “Eneo lote la machinjio ni chafu, mifereji ya kutiririsha maji machafu yote imeziba na mimi nimefika kukagua, lakini kuchinjia chini ni kosa kubwa, wanahatarisha afya za watumiaji wa nyama kuna hatari ya kutokea kwa magonjwa hapo,”  

“ Lakini pia hakuna uzio, mbwa, paka na wanyama wengine ambao siyo rafiki kila siku wanazunguka hapo, muda wa kuchinja ukiisha wanakwenda eneo la kuchinjia kutafuta mabaki, hiyo ni hatari sana alafu kesho yake watu wanakuja tena kuchinja,” alieleza Malima. 

Ofisa Afya huyo anasema kuwa uchafu wote unaotokea wakati wa kuchinja umekuwa haupelekwi eneo husika, na badala yake hutupwa kwenye majani yaliyo karibu na machinjio hayo hali ambayo inasababisha wadudu wengi wakiwamo inzi kuzaliana na kuwa tishio kwa afya za watu.

“ Kwa ufupi hali ya machinjio hiyo ni mbaya sana na haifai kuitwa machinjio, lakini hata mazingira hayafanyiwi usafi, eneo limejaa majani, tayari tuliwashauri wahusika na kutoa mapendekezo yetu,”anasisistiza ofisa huyo wa afya.

Licha ya maelezo hayo, MTANZANIA lilichukua jukumu la wiki nzima kila siku asubuhi kwenda kwenye machinjio hayo kwa kujiridhisha na maelezo ya mtaalamu huyo.

Kilichobainika ni ukweli kwa asilimia 100, jambo kubwa ambalo ni hatari sana na linatakiwa kuchukuliwa hatua za haraka ni kitendo cha nyama kuchinjiwa chini kwenye sakafu, eneo ambalo si salama na ni kinyume kabida na utaratibu uchinjaji.

Mbali na hilo, kila baada ya kumaliza shughuli za uchinjaji kila siku kwenye eneo hilo, wanyama kama mbwa na paka ambao si rafiki kwa afya za binadamu, hutembelea maeneo hayo na kuanza kula mabaki.

Kwa ufupi mbwa wamekuwa wakizagaa zagaa aneo la machinjio kama nyumbani kwako au sehemu yao ya kufugiwa, sheria na kanuni zinaeleza machinjio yanatakiwa kuwa na uzio.

Kwa mujibu wa Malima ambaye ni mtaalamu aliyepewa jukumu la kuhakikisha afya za wananchi zinakuwa salama, ametoa taarifa kwenye mamlaka husika juu ya hali ya machinjio hayo lakini hajasikilizwa.

Tunatambua kuwa machinjio ya nyama kwenye halmashauri nchini, yapo chini ya mkurugenzi wa halmashauri husika na ndiye mwenye dhamana ya kuboresha na kuhakikisha vigezo vyote vinavyohusu sekta hiyo vinazingatiwa.

Ushauri wangu hapa ni kwamba, mkurugenzi ameambiwa na mtaalamu mwenye dhamana ya sekta hiyo anahitaji nini zaidi ya kuchukua hatua haraka?

Niseme tu kwa kuwa kinga ni bora kuliko tiba hatupaswi kusubiri yatokee madhara makubwa ndipo tuanze kukimbizana, kulaumiana, kuwajibishana kwa vile inawezekana marekebisho yakafanywa na machinjio zetu zikawa sehemu salama kwa afya.

Nimalizie makala haya kwa kusema kwamba, katika hili TFDA haiwezi kukwepa lawama ikiwa kutatokea madhara makubwa kwa wananchi kwa kuwa hili lipo ndani ya uwezo wenu.

Na ni jambo la kushangaza kwamba mpaka hali inafikia hatua hiyo mamlaka kama hiyo haina taarifa juu ya ubora wa machinjio inayotegemewa na asilimia kubwa ya wananchi wa Bariadi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles