22.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Mabilioni ya wanachama NSSF hatarini kuyeyuka

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

SHILINGI bilioni 27.1za wanachama wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), ziko hatarini kupotea baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kubaini dosari katika uwekezaji uliofanywa na shirika hilo katika manunuzi ya ardhi na ujenzi kwenye miradi saba.

Akiwasilisha taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2018, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema taarifa ya ukaguzi maalumu uliolenga zaidi miradi inayohusu ununuzi wa ardhi katika maeneo mbalimbali nchini imebaini udhaifu mkubwa uliofanywa na shirika hilo. 

Alisema uchambuzi wa kamati kwa miradi hiyo saba unaonyesha kuwa jumla ya Sh bilioni 27.1 ambazo ni mali ya wanachama wa NSSF zipo hatarini kupotea kwa sababu ya maamuzi ya uwekezaji usiokuwa na tija.

Aliitaja miradi hiyo ni ujenzi wa Hospitali ya Apollo Dar es Salam, ujenzi wa jengo la ubalozi na biashara Nairobi-Kenya, uzalishaji wa umeme Mkuranga, ujenzi wa nyumba katika eneo la Kiseke na Bugarika mkoani Mwanza na mradi wa ujenzi wa nyumba katika kitalu namba 249 kilichopo eneo la Njiro mkoani Arusha.

Kaboyoka aliitaja mingine ni ule wa Mwandiga Transport Terminal, uliopo mkoani Kigoma na manunuzi ya ardhi katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam.

Kaboyoka ambaye pia ni Mbunge wa Same Mashariki (Chadema), alisema kamati yake imefanya uchambuzi wa kina wa miradi hiyo kama ilivyowasilishwa katika taarifa ya ukaguzi maalumu wa NSSF kwa mwaka 2016/2017 na kubaini dosari ambazo zinaweza kuisababishia Serikali hasara.

HOSPITALI YA APOLLO

Akifafanua jinsi mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Apollo ya Dar es Salaam unavyoweka hatarini fedha za mfuko huo kupotea, alisema licha ya kutumia Sh bilioni 4.19, lakini sasa umetelekezwa.

Mkataba wa mradi huo ulisainiwa Septemba 23 mwaka 2014, kati ya NSSF na Apollo Hospital Enterprises Limited, Singapore.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo wa PAC, makubaliano ya mradi huo yalikuwa Apollo watoe vifaa na kuendesha hospitali hiyo kwa miaka 15 kwa gharama ambayo ingekubaliwa na kugawanywa asilimia 50 kwa 50 kwa wabia wa mradi huo.

Alisema Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alipotembelea mradi huo mapema mwezi Februari 2018, alikuta mradi umetelekezwa na mkandarasi kutokana na eneo hilo kutofikika kwa urahisi kwa sababu ya ujenzi wa mradi wa mabasi yaendayo haraka (Dart).

Zaidi alisema hakuna shughuli inayoendelea, hivyo kuthibitisha uwekezaji usio na tija na matumizi yasiyofaa ya fedha za umma.

JENGO LA UBALOZI NA BIASHARA KENYA

Kuhusu mradi wa ujenzi wa jengo la ubalozi na biashara Nairobi, Kenya, Kaboyoka, ameeleza kwamba hadi sasa jumla ya Sh milioni 854.2 zimekwishatolewa na NSSF katika utekelezaji wa mradi huo na kwamba hadi kamati inakamilisha taarifa hiyo hakuna shughuli zozote zinazoendelea.

Katika mradi huo, Wizara ya Mambo ya Nje inamiliki sehemu ya ardhi jijini Nairobi ambapo waliingia makubaliano na NSSF kujenga jengo la ubalozi na biashara.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, alisema NSSF walitakiwa kutoa fedha kiasi cha Sh bilioni 77.4 na wizara ingechangia ardhi kama sehemu ya mtaji wake (Land for Equity).

MRADI WA UMEME MKURANGA

Mradi wa kuzalisha umeme wa Mkuranga (Mkuranga Power Generation), Kamati hiyo ya PAC imesema hadi sasa NSSF wametumia Sh bilioni tatu na ukaguzi umebaini ardhi iliyonunuliwa haijawahi kupimwa wala haina mipaka, jambo ambalo litasababisha migogoro kwa siku zijazo.

Kaboyoka alisisitiza: “Pamoja na dosari hiyo, hapakuwepo na upembuzi yakinifu wowote kuonyesha economic viability (faida za kiuchumi) za mradi huo na namna fedha za uwekezaji zitakavyorejeshwa.”

Inaelezwa kuwa kabla ya kuanza kwa mradi huo, NSSF, Tanesco (Shirika la Umeme nchini) na TPDC (Shirika la Maendeleo la Petroli), waliingia makubaliano ya kuanzisha mradi wa kuzalisha umeme katika eneo la Mkuranga, Mkoa wa Pwani.

Gharama za mradi huo kwa mujibu wa Kamati ya PAC, zilikadiriwa kuwa Dola za Marekani milioni 490.

NSSF walinunua ardhi yenye ukubwa wa ekari 100 kwa ajili ya mradi na kuchimba visima 11 vya maji katika eneo hilo.

UJENZI WA NYUMBA KISEKE, BUGARIKA MWANZA

Mwenyekiti huyo alisema mradi wa ujenzi wa nyumba katika eneo la Kiseke na Bugarika mkoani Mwanza, kamati hiyo imeeleza hadi kufikia sasa jumla ya Sh bilioni 1.51 ambazo ni sawa na asilimia 80 ya gharama za mradi zimekwishalipwa.

Aidha, Kaboyoka, amelieleza Bunge kwamba, ukaguzi umebaini kuwa NSSF hawajapewa viwanja vyote kwa mujibu wa mkataba, hivyo kuwepo uwezekano wa kupotea kwa fedha za umma.

Pamoja na dosari hiyo, uongozi wa Kata ya Buhongwa, uliwafahamisha wakaguzi kuwa baadhi ya wanavijiji wa eneo hilo hawakulipwa fidia, hivyo wameamua kuvamia eneo hilo na kusababisha hasara kwa NSSF.

Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2008, ambapo NSSF walikubaliana na Halmashauri ya Jiji la Mwanza kununua viwanja 357 katika eneo la Bugarika na viwanja 299 katika eneo la Kiseke kwa gharama ya Sh bilioni 1.89.

UJENZI WA NYUMBA NJIRO

Mradi wa ujenzi wa nyumba katika kitalu namba 249 kilichopo eneo la Njiro Arusha, ripoti imeonyesha licha ya mradi huo kuigharimu NSSF fedha nyingi lakini tayari umevamiwa.

Katika mradi huo ripoti inaonyesha kuwa malipo ya awali yaliyofanyika mwezi Novemba 2010 yalikuwa Sh milioni 132 na malipo ya mwisho yalikuwa Sh milioni 308 yalifanyika Machi 2011.

“Wakaguzi walipotembelea eneo hilo mwezi Januari 2018, walikuta eneo lote limevamiwa na wanakijiji na kujenga majengo kama nyumba za ibada na shughuli nyingine za binadamu. Pamoja na dosari hizo, wakaguzi hawakuweza kupata nyaraka za uhamisho wa ardhi hiyo kutoka kwa muuzaji kwenda NSSF. Hivyo basi hakuna uwezekano wa fedha za umma zilizotumika kununua ardhi hiyo kurejeshwa tena kwa sasa,” alisema Kaboyoka.

 MRADI WA MWANDIGA TRANSPORT

Kuhusu mradi wa Mwandiga Transport Terminal, kamati hiyo ya PAC imeeleza kuwa hakuna shughuli yoyote inayoendelea katika eneo hilo pamoja na kuwa matumizi ya Sh bilioni 1.85 yamekwishafanyika.

Alisema NSSF walipanga kutekeleza mradi wa kituo cha kimataifa cha usafiri katika eneo la Mwandiga, Kigoma lenye ukubwa wa ekari 28 kwa gharama za Sh bilioni 33.3.

Mwenyekiti huyo alisema hadi sasa jumla ya ekari 28 za ardhi zimepatikana kwa gharama ya Sh bilioni 1.85.

Hata hivyo, Kaboyoka, alisema hii ina maana kuwa ekari moja ya ardhi ilinunuliwa kwa wastani wa Sh milioni 66.

UNUNUZI WA ARDHI PWANI, DAR

Kaboyoka alisema kamati ya PAC  imebaini madudu pia katika ununuzi ya ardhi katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kwa gharama ya Sh bilioni 15.8.

“Kamati imebaini kuwa ardhi hiyo ilinunuliwa bila ya kuwepo kwa kamati ya uwekezaji ya Shirika la (Management Investment Committee, MIC) na haikupata idhini ya bodi. Haikuwa hivyo tu, bali imebaini pia ardhi hiyo haikuwa imepimwa na kufanyiwa tathmini ili kujiridhisha na thamani yake halisi ukilinganisha na bei iliyonunuliwa,” alisema Kaboyoka.

MAAZIMIO

Kutokana na hayo yote, Bunge limeazimia Serikali ifanye uchunguzi wa wahusika wote waliohusika katika mchakato wa ununuzi wa ardhi husika kwa malengo ya uwekezaji ambao haukuwa na tija na kisha kuchukua hatua stahiki kwa kuzingatia matokeo ya uchunguzi.

Pia Serikali na bodi za mifuko mipya ya hifadhi za jamii iliyoundwa zihakikishe masuala ya uwekezaji yanafanyika kwa kuzingatia sheria na miongozo ya mamlaka husika kama SSRA (Mamlaka ya usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii) na BoT (Benki Kuu ya Tanzania), ili kuepuka uwekezaji usiokuwa na tija kwa taifa na kwa wanachama wa mifuko husika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles