25.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

JPM afichua akaunti 3,000 feki za korosho

AZIZA MASOUD-DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, amesema kuna wafanyabiashara 3,000 walifungua akaunti feki ili walipwe fedha za korosho.

Pia amesema wanaolalamikia fedha za ununuzi wa korosho ni wafanyabiashara wasiokuwa na mashamba na amesisitiza Serikali haitawalipa watu hao kwa kuwa hawana uhalali wa kupata malipo hayo.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana aposhuhudia utiaji saini wa mkataba wa kuuziana tani 36,000 za mahindi zenye thamani ya Sh bilioni 21 kati ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) na Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP).

“Ununuzi wa korosho unaenda vizuri, wanaopiga kelele ni wale makambonga kwa sababu walinunua korosho walifikiri watalipwa fedha, wanapoulizwa mashamba yako wapi hawayaonyeshi kwa hiyo hawalipwi, wale ndio wanapiga kelele na tumeshajua kuna akaunti karibu 3,000 feki watu walizifungua nazo hazilipwi,” alisema.  

Magufuli alisema Serikali haina shida na wafanyabiashara isipokuwa inahitaji watu wanaofanya biashara kwa halali.

Alisema Serikali inawaunga mkono wafanyabiashara waaminifu na si vinginevyo.

“Wafanyabiashara wamekuwa walalamishi mno, mnataka kila siku mbebwe, yapo mambo yakushughulikiwa na Serikali na mengine mshughulikie wenyewe, mpange mkakati wa kufanya biashara ambazo zina manufaa pia kwa wakulima wetu,” alisema.

Kuhusu ununuzi wa chakula na usimamizi wa mazao, aliupongeza uongozi wa NFRA kwa kuiendesha vizuri taasisi hiyo aliyosema awali ililegalega kiutendaji.

“Wizara ya Kilimo mmeanza vizuri lakini NFRA palikuwa na matatizo makubwa, ninamshukuru huyu mama (mkurugenzi) kwa sasa anafanya kazi vizuri, ilikuwa kila mwaka Serikali inatenga fedha kwa ajili ya kununulia tani 250 za chakula.

“Zinakaa pale stoo lakini hizi tani zinapokuwepo wala hatupatagi njaa na tuna muda mwingi hatujapata njaa lakini hatujui hizo tani zinapotelea wapi kila mwaka, kwamba zikishaingia katika stoo zinapotelea huko lakini kiukweli walikuwa wanakula, zilikuwa zinauzwa kwa bei ya kutupwa,” alisema.

Pia alisema kutokana na utendaji wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa NFRA, Vumilia Zikankuba, kuna haja ya kumrasimisha ili afanye kazi vizuri kwa kuwa anakaimu nafasi hiyo.

“Naomba Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa) na mawaziri kama mmemwona anafanya vizuri, msijali miaka, muidhinisheni aendelee maana saa nyingine anashindwa kufanya majukumu yake vizuri, sasa nyingine watu wanaona kuwa mkurugenzi hadi uwe mzee mpeni akishindwa basi shauri yake,” alisema Magufuli.

Pia aliitaka NFRA ibadilike na kuanza kubana matumizi kwa kupunguza wafanyakazi wasio na tija kwa kuwa kwa sasa Serikali haitakuwa inatoa fedha kama ilivyokuwa awali.

“NFRA mbadilike, msitegemee kila mwaka nitakuwa natoa fedha kwa ajili yenu hilo halipo, hakuna uhakika kwamba mwaka huu natoa fedha wakati hakuna hata upungufu wa chakula na fedha zinazotolewa zinakuwa hazina mrejesho wowote,” alisema.

Magufuli alisema taasisi hiyo imekuwa ikitengewa fedha na Serikali kila mwaka lakini kwa sasa hali itakuwa tofauti na mkakati huo umeanza mwaka huu wa fedha.

“Kila mwaka huwa zinatengwa fedha kwa ajili ya NFRA, kwa mwaka huu ilikuwa shilingi bilioni 90, nikakataa nikatoa bilioni 15 nijaribu) kama na zenyewe zitapotea.

“NFRA mpunguze gharama za uendeshaji kwa sababu gharama za operesheni zikiwa juu kila siku mtakuwa mnapata hasara, mjitahidi mtoe mchwa, msijali umri wao wala kukaa kwao muda mrefu NFRA, muwatoe wale ambao hamna uwezo wa kuwatoa mwambieni waziri awatoe na yeye kama hawezi niambie mimi nitawatoa,” alisema.

Pia aliitaka ijipange vizuri kuhakikisha inafanya biashara ya mazao yatakayowakomboa wakulima wanaolia na masoko nchini.

“NFRA mjipange vizuri hizi tani zinazohitajiwa na WFP, wapeni hata wakitaka tani mia muwape kwa sababu wanalipa fedha.

“WFP wameomba tani elfu arobaini na tano, kwanini mmewapa elfu thelathini na sita wapeni hizo walizotaka, Tanzania hatutapata njaa,” alisema.

Magufuli alisema kufanya hivyo kutasaidia kuwa na mzunguko mzuri wa biashara na kuwapa hamasa wakulima kulima mazao mengi.

“Wenzetu wanaopelekewa haya mazao wana migogoro, tuitumie hii kujinufaisha hatusemi kuwa tunaifurahia migogoro iendelee hapana, lakini tuitumie kuuza mazao kwa sababu hata tusipolima tukawauzia wao bado watapigana tu,” alisema.

Alisema NFRA wanapaswa kuwasaidia wakulima ambao ni asilimia 65 ya Watanzania wanaofanya shughuli za kilimo.

Pia aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha inasimamia miundombinu ili kuwasaidia wakulima kufikisha mazao kwa wakati.

“Tunataka kuwa na miundombinu mizuri, reli tumewapa fedha karibu shilingi bilioni tano kwa ajili ya kufufua mabehewa mengine karibu 400 miezi miwili iliyopita, sasa mkayafufue ili msafirishe mizigo hii bahati nzuri mnapopeleka mahindi mnakuwa tayari mmeshatengeneza biashara kwa sababu WFP watawalipa tena hamtalipwa kwa shilingi bali kwa dola sasa mchangamke,” alisema.

Awali Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa, alisema kwa sasa wizara hiyo inafanya kazi ya kuwashauri wakulima wafanye kilimo cha tija na kuhakikisha wanapata masoko ndani na nje ya nchi.

Alisema makubaliano ya ununuzi wa mahindi baina yao na WFP ni sehemu ya utekelezaji wa mpango huo.

“Tunapanga kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya WFP ili tuhakikishe wanachukua mzigo mkubwa kwa sababu miaka ya nyuma walikuwa wanashindwa kuhudumia nchi jirani kutokana na changamoto ya uratibu. Kwa sasa tunataka kuhakikisha mzigo mkubwa unaotoka hapa unanunuliwa WFP,” alisema.

Kwa upande wake, Mwakilishi na Mkurugenzi Mkazi wa WFP hapa nchini, Michael Dunford, alisema mahindi hayo ni sehemu ya tani 160,000 za chakula zenye thamani ya Sh bilioni 132.2 zilizonunuliwa nchini kwa mwaka 2018.

Alisema kutokana na uhusiano mzuri uliopo baina ya WFP na Tanzania, wataendelea kufanya kazi kwa ukaribu na NFRA na taasisi nyingine zinazohusika na ununuzi wa chakula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles