26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mahakama yaipa Serikali siku saba kuwajibu wapinzani

PATRICIA KIMELEMETA- DAR ES SALAAM

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imekataa ombi la Serikali la kujibu hoja ndani ya siku 21 na badala yake imewapa siku saba kuzijibu katika kesi ya kupinga muswada wa vyama vya siasa iliyofunguliwa na viongozi wa vyama vya upinzani.

Kesi hiyo namba 31 ilifunguliwa mahakamani hapo Desemba 20, mwaka jana na viongozi wa vyama vya upinzani ambao ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha  ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, Kaimu Naibu Katibu Mkuu (Bara) wa Chama cha Wananchi (CUF), Joram Bashange na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma wa chama hicho, Salim Bimani.

Kesi hiyo inasimamiwa na jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Barke Sahe, huku upande wa walalamikaji wakiwakilishwa na mawakili; Mpoki Mpare, Daim Halfan, Frederick Kihwelo na Mulwambo.

Walalamikiwa katika kesi hiyo ni Serikali na Mwanasheria Mkuu (AG).

Akisoma uamuzi huo mahakamani hapo jana, Jaji Sale, alisema hakuna sababu ya kuchukua muda mrefu kwa Serikali kujibu hoja za walalamikaji katika kesi ya kupingwa Muswada wa Sheria za Vyama vya Siasa kwa kuwa suala hilo lina masilahi mapana kwa umma.

“Hakuna haja ya kutoa siku nyingi ya kujibu hoja zilizowasilishwa na walalamikaji kwa sababu muswada wenyewe umeandaliwa na Ofisi ya AG na ukizingatia kuwa suala hili lina masilahi mapana kwa umma, natoa siku saba kwa Serikali kujibu hoja,” alisema Jaji Sale.

Katika kesi hiyo, mawakili wa walalamikaji wanapinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi, kinachoeleza kuwa muswada wowote hauwezi kupingwa mahakamani.

Mawakili hao wanadai kuwa muswada huo unakiuka haki za kisiasa za binadamu, kwa kuwa unaharamisha shughuli za kisiasa na kumpa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama vya siasa, yakiwamo ya kiuongozi.

Wanadai kuwa wanahitaji kuwasiliana kwanza na mamlaka na taasisi nyingine za Serikali kwa lengo la kuiwezesha mahakama kutoa uamuzi wa haki.

Pia wanadai kwa kuwa Kamati za Bunge zinatarajiwa kuanza Januari 15, mwaka huu na iwapo mahakama haitapanga muda mfupi kesi yao itakuwa imepitwa na wakati kwa sababu tayari itakuwa imeshashughulikiwa na Bunge.

Pia Wakili Mpoki aliiomba mahakama kutoa zuio la muda kumzuia AG, Bunge na kamati zote zinazohusiana na muswada huo kutoujadili wala kuuwasilisha bungeni hadi shauri lao litakapoamriwa.

Alidai muswada huo unamilikiwa na Serikali na kwamba hakuna mtu mwingine anayeweza kuuzuia isipokuwa mahakama.

Pia Wakili Mpoki alidai kesi hiyo inahusu haki za msingi na kwamba uvunjifu wowote wa masharti ya kikatiba kuhusu haki hizo unaofanywa na Serikali hauwezi kufidiwa.

Jaji Sale aliahirisha kesi hiyo hadi Januari 11, mwaka huu ili upande wa Serikali uweze kuwasilisha majibu ya hoja hizo.

MWISHO

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles