ROME, ITALIA
SERIKALI ya Italia imekana kupokea ombi lolote la hifadhi kutoka kwa balozi wa Korea Kaskazini, Jo Song Gil mjini Rome ambaye anaripotiwa kuingia mafichoni nchini humo.
Kwa mujibu wa chanzo kimoja cha habari kutoka ndani ya wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa ya Italia, kimeliambia shirika la habari la AFP kuwa hawana taarifa juu ya ombi la aina hiyo na kuongeza kuwa kile ambacho wizara hiyo ilipokea ni ombi la kuijaza nafasi ya balozi huyo, ambaye Korea Kusini imesema anaitwa Jo Song Gil.
Hata hivyo, duru hiyo imesema haijulikani aliko balozi huyo wa Korea Kaskazini na kwamba aliyechukua nafasi yake tayari amewasili Rome.
Shirika la ujasusi la Korea Kusini liliwafahamisha jana wabunge kuhusu hatima ya balozi huyo baada ya gazeti moja kuripoti kuwa Jo Song Gil, mwenye umri wa miaka 47, aliomba hifadhi yeye pamoja na familia yake katika nchi moja ya Magharibi ambayo haikutajwa.