Na MAREGESI PAUL DODOMA
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewataka wabunge ambao katika majimbo yao kuna maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru, wabuni miradi mbalimbali ya kuyaendeleza na kuyahifadhi kwa ajili ya kukuza utalii.
Amesema kama wabunge hao watafanikiwa katika hilo, watakuwa wanachangia katika ukuzaji wa utalii wa ukombozi na wa utamaduni.
Dk. Mwakyembe aliyasema hayo bungeni jana alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2019/20 yenye thamani ya Sh bilioni 30.8.
“Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kujitawala nchi za Afrika ziliendelea kutumia vitabu vya historia vilivyoandikwa na wale wale waliotutawala.
“Hali hii imesababisha michango ya baadhi ya mashujaa wetu wa harakati za ukombozi kutoakisiwa na kutothaminiwa ipasavyo.
“Mfano halisi wa hilo ni shujaa Leti Hema wa Wanyaturu, mwanamama aliyewazuia watawala wa Uerumani kwa zaidi ya miaka mitatu kwa kutumia makundi ya nyuki waliouma wazungu tu na kuwazuiwa wajerumani hao wasikaribie kilima cha Ng’ongo Ipembe na maeneo yote yaliyokizunguka.
“Pia, mwanamama huyo alipokutana na Wajerumani hao kwa mazungumzo ambayo hayakufika mwisho, alikaa juu ya ncha kali ya mkuki, badala ya kukaa kwenye kigoda cha kawaida.
“Shujaa huyu pamoja na mashujaa wengine wa harakati za ukombozi akiwamo Mtemi Isike wa Tabora na Nduna wa Mkomanile wa Wangoni, hawajaandikwa na wala mchango wao hauthaminiwi katika historia ya nchi yetu.
“Kwa hiyo, natoa wito kwa waheshimiwa wabunge ambao katika majimbo yao kuna maeneo yaliyotumiwa na wapigania uhuru, waendelee kubuni miradi mbalimbali ya kuyaendeleza maeneo hayo na kuyahifadhi,” alisema Dk. Mwakyembe.
Wakati huo huo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, iliishauri Serikali iliimarishe Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) liweze kurusha matangazo yake kwa ufanisi.
Maoni hayo yalitolewa na Mjumbe wa Kamati hiyo, Deogratius Ngalawa ambaye pia ni Mbunge wa Ludewa (CCM) alipokuwa akiwasilisha maoni ya kamati yake hiyo.
Mwisho
Zitto: Nitawasilisha hoja
kumchunguza DPP
Na Mwandishi Wetu
-DODOMA
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amesema anakusudia kuwasilisha bungeni kusudio la hoja ya kuunda Kamati Teule ya Bunge, kumchunguza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Amesema pamoja na mambo mengine, lengo la kuwasilisha hoja hiyo ni kutaka kumchunguza DPP dhidi ya tuhuma mbalimbali katika kumaliza mashauri ya jinai.
Zitto alieleza msimamo huo bungeni juzi usiku, baada ya Bunge kuhitimisha mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2019/20.
“Mheshimiwa mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii na naomba niseme kwamba natarajia kuwasilisha kusudio la hoja ya kuunda kamati teule ya Bunge kumchunguza DPP.
“Kamati hiyo itakapoundwa, naomba imchunguze Mkurugenzi wa Mashtaka katika kumaliza mashauri ya jinai kwa makubaliano na watuhumiwa bila kuwapo sheria wezeshi.
“Pia, ntaomba kamati hiyo ichunguze malalamiko ya rushwa katika mchakato wa kumaliza mashauri hayo ya jinai kwa makubaliano na watuhumiwa katika kumaliza mashauri yao.
“Pamoja na hayo, kamati hiyo itakapoundwa, nitaomba ipendekeze njia bora ya sheria kwa ajili ya kuanzisha njia sahihi inayozingatia haki bila kumuonea mtu yeyote,” alisema Zitto.
Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge, alikubaliana na hoja hiyo ya Zitto kwa kile alichosema kuwa mbunge huyo aliiwasilisha kwa kufuta kanuni hasa kanuni ya 120.
Pamoja na Zitto kuwasilisha hoja hiyo kwa mdomo, Chenge alisema kitakachofuata sasa ni kuiwasilisha kwa maandishi kwenda kwa Katibu wa Bunge.
“Waheshimiwa wabunge, mheshimiwa Zitto amewasilisha vizuri kwa mdomo kusudio lake hilo.
“Kinachofuata sasa ni yeye kuliweka katika maandishi, kisha litapelekwa kwa Katibu wa Bunge ili kama litakubaliwa, liwekwe kwenye shughuli za Bunge na kupangiwa siku. “Kwa hiyo, mimi namtakia kila la kheri katika kusudio hilo,” alisema Chenge kisha akaahirisha Bung