JUSTIN DAMIAN -DAR
ES SALAAM
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imechukua uamuzi wa kuhamishia mali za Benki M kwa Benki ya Azania, baada ya benki hiyo kushindwa kuwa na ukwasi wa kutosha kujiendesha.
Uamuzi wa BoT ni muendelezo wa hatua zinazochukuliwa dhidi ya benki zinazoyumba mtaji.
Mei mwaka jana, BoT iliridhia muunganiko kati ya Benki ya Twiga Bancorp na TPB Benki baada ya Twiga Bancorp kushindwa kujiesha kwa kutokuwa na ukwasi wa kutosha .
Agosti 2018, BoT iliridhia muunganiko kati ya Benki ya Wanawake Tanzania na TPB Benki.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Naibu Gavana wa Benki Kuu, Dk. Bernard Kibese alisema Benki M ilipewa leseni na kuanza kufanya shughuli za benki nchini mwaka 2008, na kuwa miongoni mwa benki zilizokua kwa haraka na kuwa na mali zenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni moja.
Alisema kuhamishia mali za Benki M kwa Benki ya Azania kunatokana na hatua iliyochukuliwa na BoT Agosti mwaka 2018 ambako BoT iliamua kuiweka chini ya usimamizi wake Benki M baada ya kubainika kuwa na upungufu mkubwa wa ukwasi na hivyo kushindwa kulipa madeni yake, zikiwamo amana za wateja.
Alisema kabla ya kuiweka Benki M chini ya usimamizi wake, BoT ilifanya jitihada mbalimbali zikiwamo kufanya mikutano na wamiliki, bodi ya wakurugenzi na menejimenti ya benki.
“Jitihada hizo zilikuwa na lengo la kurekebisha mwenendo wa benki hiyo iweze kufanya shughuli zake za benki kwa mujibu wa taratibu za sheria.
“Hata hivyo, pamoja na benki kupewa muda wa kutosha, jitihada hizo hazikufanikiwa,” alisema Dk. Kibese
Naibu Gavana alisema baada ya kuiweka chini ya usimamizi wake, BoT ilisitisha shughuli za utoaji wa huduma za benki za Benki M kwa siku 90 kuipa nafasi BoT kutathmini hatua za kuchukua kupata ufumbuzi wa tatizo hilo.
“Mnamo tarehe 2 Novemba 2018, Benki Kuu iliongeza muda wa usimamizi kwa siku 60 kupata muda wa kutosha wa kutathimini hali ya fedha ya Benki M, ambayo ilikuwa ni hatua muhimu katika utatuzi wa matatizo ya benki hiyo.
“Benki Kuu ya Tanzania inapenda kuuarifu umma kwamba kwa mamlaka iliyopewa chini ya kifungu cha 59 (4) cha Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006, mchakato wa kupata ufumbuzi wa matatizo ya Bank M umekamilika.
“Baada ya kutathimini njia mbalimbali za kutatua matatizo ya Benki M, mnamo tarehe 2 Januari 2019, Benki Kuu iliamua mali na madeni ya Bank M kuchukuliwa na benki nyingine kama njia ya ufumbuzi wa matatizo ya Benki M,” alisema
Dk. Kibese alisema kwa sasa, BoT, Azania Bank Limited na wadau wengine wanaendelea kuandaa taratibu za sheria za kukamilisha mchakato wa kuhamisha mali na madeni ya Benki M kwenda Benki ya Azania na wateja wenye amana na wadai wengine wataarifiwa tarehe ya kuanza kupata huduma za benki kupitia Azania.