JOHANNESBURG, A.Kusini
CHAMA tawala nchini hapa, African National Congress (ANC), kimefanikiwa kurejea madarakani, lakini safari hii kikiwa kimepata asilimia ndogo ya kura ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa mjini hapa ANC, imepata asilimia 58 ya kura zote kikifuatiwa na Chama cha Democratic Alliance (DA) kilichopata asilimia 21 na chama cha tatu kikiwa ni cha l Economic Freedom Fighters (EFF), ambacho kimepata asilimia 11.
Kwa mujibu wa Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC tatizo la mdororo wa kiuchumi na rushwa ndivyo vilivyoshusha umaarufu wa chama hicho kikongwe cha ANC.
Akizungumza mara baada ya kutangazwa matokeo hayo kiongozi wa ANC, Cyril Ramaphosa,aliwataka wananchi kuungana na kujenga Afrika Kusini yenye umoja.
Mbali na kujenga nchi yenye umoja, kiongozi huyo alisema kuwa ushindi huo umeonesha kuwa wananchi wa taifa hilo bado wanaimani na ANC tangu ilipoingia madarakani mwaka 1994.
“Na sasa tufanye kazi kwa pamoja, watu weusi, wazungu wanaume kwa wanawake, vijana na wazee kujenga Afrika Kusini yenye umoja ni jukumu letu sote, ” Rais Ramaphosa aliwaambia wafuasi wake mjini Pretoria.
Alisema kwamba anaitaka Afrika Kusini ambayo sio ya kiubaguzi wa rangi, kijinsia,kidemokrasia na kimafanikio.
Mwandishi wa BBC, Will Ross anasema kwamba hata hivyo ilikuwa ikifahamika ANC haiwezi kupata idadi kubwa ya kura.
Alisema ingawa idadi ya wafuasi wake wamepungua lakini jambo hilo halikutokana na utendaji wake mbaya pengine walitaka kuwapa nafasi wengi wajaribu kutafuta ufanisi katika kukabiliana na kashfa za rushwa zinazoikabili ANC na kutafuta maendeleo ya kukabiliana na umasikini.
Mwandishi huyo alisema kuwa chama hicho kimepata asilimia 65 katika mabunge yote mawili idadi ambayo imeporomoka ikilinganishwa na asilimia 73 kilichopata miaka mitano iliyopita.