26.8 C
Dar es Salaam
Saturday, September 7, 2024

Contact us: [email protected]

Njombe watekeleza agizo la Rais Magufuli

Elizabeth Kilindi,Njombe

KUTOKANA na agizo la Rais Dk. John Magufuli la kutaka stendi kuu mpya  ya Njombe  kuanza kutumika ifakapo Mei 10,2019 hatimaye stendi hiyo imeanza kazi rasmi.

Akizingumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki, Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri, aliwapongeza wananchi kwa kuitikia wito wa kuhamia katika stendi mpya licha ya kuwepo na shughuli za ujenzi wa stendi hiyo zikiendelea.

“Nawapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi.Wengi mmekuja kushuhudia kama kweli stendi imeanza lakini pia kwa wasafiri, wadau wa vyombo vya usafirishaji mwitikio umekuwa mkubwa na hii inaonesha wazi jinsi mlivyokuwa na kiu ya siku nyingi kuitumia stendi hii” alisema Ruth na kuongeza.

“Tunamshukuru Rais Magufuli kwani kupitia maelekezo yake  kumefanya stendi hii ianze kufanya kazi, ametusaidia sana katika kutusukuma katika siku hizi za mwishoni  na leo tumetekelza agizo lake stendi imeanza kufanya kazi na wananchi wanafuraha iliyopitiliza”alisema.

John Msemwa ni miongoni mwa abiria waliofika kwenye stendi mpya ili kujionea huduma alisema changamoto nyingi kwa sasa zimepungua ukilinganisha na stendi ya awali.

“Kwanza stendi ya zamani ilikuwa ndogo sana hii stendi ni kubwa, miundombinu ni mizuri vyoo maji yapo vyoo vizuri, visafi hata ukiangalia huku hakuna matope kama kule kwenye stendi ya mwanzo. Stendi ya awali matope mengi hasa wakati wa mvua hakuna hata sehemu ya kukaa.huku kuna maeneo mengi ya kukaa ikikamilika itakuwa kivutio” alisema Msemwa.

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda, alisema mpaka sasa ujenzi wa stendi hiyo umekamilika kwa asilimia 95 na kuwa shughuli zolizosalia zinatarajia kukamilishwa ndani ya wiki mbili zijazo.

“Tunashukuru kwa pongezi kwani haikuwa kazi rahisi, asilimia tano zilizosalia tutazikamilisha ndani ya wiki mbili licha ya mabasi kuanza. Tulikuwa pia na kikao na wahandisi ili kuona ni namna gani kazi zilizosalia tunazikamilisha ndani ya wiki mbili licha ya kuwepo na changamoto ya mvua za mara kwa mara,”alisema Mwenda.

Mwenda aliongezea kuwa licha ya kutoa huduma kwa wananchi stendi hiyo pia ni chanzo kikuu cha mapato kwa Halmashauri hiyo na wanataraji kukusanya milioni mia tatu kwa mwaka hayo yakiwa ni makisio ya chini.

Mkurugenzi huyo pia aliendelea kuwasisitizia wananchi kuhakikisha kuwa wanafuata utaratibu uliowekwa wa kuchangia gharama ya Sh 200 kwa wale ambao wanaingia stendi pasipokuwa na tiketi ya abiria.

Akizungumzia suala wa wajasiriamali wadogo alisema umeandaliwa utaratibu mzuri na punde wataelekezwa utaratibu kwa wajasiriamali hao na amewasisitiza kuhakikisha kuwa wanakuwa na kitambulisho cha wajasiriamali.

Mwenda aliwapongeza wananchi kwa mwitikio wao na kusema kuwa ataendelea kutoa tarifa ya mabadiliko yoyote yatakayokuwepo katika stendi hiyo kadri muda unavyozidi kwenda na kwa kadri ya matengenezo yanayoendelea katika stendi hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles