Askari Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro wakitoa vifurushi vya dawa za kulevya aina ya mirungi iliyokutwa imehifadhiwa kwenye mabegi yanayotumiwa na wanafunzi baada ya kukamatwa eneo la Latina wilayani Hai juzi.
MWANDISHI WETU-MOSHI
WAFANYABIASHARA na wasafirishaji wa mirungi wameibuka na mbinu nyingine mpya ya kujigeuza wanafunzi na kuficha mirungi katika mikoba midogo inayotumiwa na wanafunzi kuhifadhi madaftari kwa lengo la kukwepa mkono wa polisi.
Mbinu nyingine ambazo Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro iibaini hivi karibuni ni pamoja na kutumia magari ya fahari yakiwamo Toyota Land Cruser, Toyota Alphasad, Toyota Vanguard na kufanyia mabadiliko gari ya Toyota Noah kurahisisha ubebaji wa mirungi kwa kificho.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Hamis Issah, alisema wasafirishaji wa mirungi wameendelea kubuni mbinu kila kukicha baada ya zile za awali kushtukiwa na polisi.
Alitoa a onyo kwa wamiliki wa magari ya abiria kutojiingiza katika mtego wa kusafirisha dawa hizo.
“Hapa kuna mizigo ambayo imekamatwa na askari wetu wakiwa barabarani, hii ni mbinu mpya ya usafirishaji.
“Hii mikoba unayoiona yote ni inaonyesha mbebaji amebeba madaftari anaenda shuleni.
“Lakini haya siyo madaftari ni mirungi ni mizigo iliyokamatwa kwenye mabasi tofauti tofauti,” alisema Kamanda Issah.
Alisema katika tukio hilo watuhumiwa tisa wakiwamo wanawake wawili wamekamatwa wakiwa na kilogramu 64 baada ya polisi kupekuwa magari matatu ya abiria yaliyokuwa yakitokea yakiendelea na safari kutoka Moshi kwenda Arusha.
“Naona mbinu zinaendelea kubadilika ndani ya wiki mbili, mbinu tatu tofauti, kwanza ya kujaza kwenye magari, pili ya kutoboa magari.
“Tatu kama mwanafunzi nyingine kama mtu anaenda hospitali amejifunga maplasta sasa hizi mbinu zitafika mpaka lini na sisi tunashukuru askari wangu wanafanya kazi vizuri,” alisema.
Kamanda Issah aliwataja wanaoshikiliwa hadi sasa kuwa ni Ibrahim Masuli, Godfrey Richard, Chrispin Baltazar, Fanuel Hamad na Jackline Mushi.
Wengine wakiwa ni Lucy Petro , Nuru Haruna, Silvesta Fabian na Minyari Miandei.
Alisema kwa sasa apolisi wameamua kupekuwa magari yote yakiwamo ya abiria huku akiwataka abiria kutoa ushirikiano kwa polisi wanapoona mizigo yenye shaka ili kuwaondolea adha ya kuchelewa kufika safari zao kutokana na usumbufu watakaopata barabarani.
“Tunawasihi abiria maana kuna abiria wengine wakiona askari wanapekua gari wanakasirika, msikasirike hii ndiyo kazi ya kupekuwa.
“Vinginevyo muwe mnatuambia ndani ya gari amepanda mtu wa ajabu na amebeba madawa ya kulevya ya mirungi hapo ndiyo itakuwa ni na nafuu na tutafanya kazi kwa muda mfupi muendelee na safari,” alisema.
Issah aliwataka wamiliki wa mabasi ya abiria kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi kuhakikisha biashara hiyo inakoma kwa kukataa kubeba abiria wenye mizigo ambayo wanatilia shaka.
Alisema kuendelea kuwabeba kutasababisha kuwaingiza katika matatizo na vyombo vyao.
“Kuna watu wakiona gari inapekuliwa wanatubeza.
“Hivi sasa tukikuona wewe unatubeza askari watakukamata … wanawabeza askari wanaofanya kazi yao halafu tutakuhoji unatubeza kwa sababu gani.
“Kwa hali kama hiyo tunaagiza askari waendelee kukamata mirungi na wasiiache,” alisistiza.
Kukamatwa kwa dawa hizo kunafanya idadi kamili ya mirungi ailiyokamatwa katika wiki mbili kufikia kilogramu 564 pamoja na vyombo vya usafiri yakiwamo magari matatu na pikipiki moja.