Na ANNA RUHASHA
IDADI kubwa ya wanafunzi wa darasa la tano na saba katika Shule ya Msingi Chifungu katika Halmsahuri ya Buchosa wilayani Sengerema , wanajishughulisha na uvuvi hali inayochangia kuwa watoro shuleni, imefahamika.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Novatus Mtabi, akizungumza kwenye mahafali ya darasa la saba, alisema utoro umekuwapo shuleni hapo kwa muda mrefu kwa vile baadhi ya wanafunzi hujishughulisha na uvuvi.
Mtabi alisema wanafunzi wanaoongoza kwa uvuvi ni wa kiume wakati watoto wa kike wao hukimbilia visiwani na mijini ambako hujishughulisha na kazi za ndani hali hiyo imekuwa ikiongeza utoro kwa wanafunzi hao.
Alisema mbali na changomoto hizo shule hiyo pia inakabiliwa na uchakavu wa miundombinu ya kujifunzia husasan madarasa kutokuwa na sakafu na nyumba za walimu na kutokuwapo maji safi na salama.
Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Sengerema, Elizabeth Kirumbu, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo, aliwakumbusha wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wao hatua inayosaidia kujua kama kuna changamoto zinazowakabili .
“Niwaombe wazazi na walezi kufuatilia maendeleo ya masomo ya watoto wenu.
“Hatua hii itasaidia kubaini mtoto wako ana changamoto zipi siyo kulipa ada tu halafu na kukaa, ukifuatilia mienendo ya masomo ya mwanao ni hazina tosha katika kumuandalia maisha bora, ”alisema Kirumbu.
Pia aliwaomba wazazi kuwafungulia akaunti za kuwatunzia fedha kidogo kidogo watoto wao kusaidia kupunguza changamoto kwa wanafunzi kukatisha masomo kutokana na kukosa mahitaji muhimu wakati akipata elimu.
Mmoja ya wanafunzi ambaye amekuwa mtoro kutokana na kuvua samaki ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema chanzo kikubwa cha kukatisha masomo na kukimbilia visiwani ni wazazi wao kutowatimizia mahitaji muhimu kama kuwapatia sare za shule.