Na CHRISTIAN BWAYA
FIKIRIA unazungumza na mtu makini anayefanya jitihada za kuhakikisha unajiona kweli kuna mtu anafuatilia kile unachokisema. Fikiria unaongea na mtu asiye na haraka ya kukujibu, asiye na papara kwenye mazungumzo, asiyetoa maelezo yasiyo na umuhimu kwa sababu kwake, kile unachokizungumza wewe, ndicho chenye umuhimu kuliko kitu kingine chochote kwa wakati huo.
Watu wenye umakini wa kiwango hiki wanao uwezo mkubwa wa kugusa mioyo yetu na kutufanya tujisikie kuwa watu wa thamani. Unapoongea na mtu mwenye uwezo huu hutatamani kuachana naye. Utatamani kuendelea kuongea na kuongea kwa sababu unajua kabisa kuwa anakusikiliza. Kisaikolojia, uwezo wa kumsikiliza mtu ni tiba ya nafsi yake. Watu wengi wanaumwa nafsi kwa sababu hawajapata mtu wa kuwasikiliza kwa makini na hivyo kuwafanya wajione ni watu wa thamani.
Kama umewahi kukutana na watu wasio makini unaweza kuelewa naongelea nini. Fikiria unaongea na mtu lakini macho yake yanafuatilia wapita njia, vidole vyake vinabonyeza simu, anakula miayo na hata namna alivyokaa tu unaona kabisa hachukulii mazungumzo yenu kwa umakini unaostahili. Wengine hufikia kiwango cha kupokea simu bila hata kukuomba ruhusa. Unaongea ghafla unastuka jamaa kasimama anacheka na simu. Unajisikiaje?
Unapokuwa mtu asiye na umakini kwenye mazungumzo watu hawawezi kukuchukulia kwa umakini. Huwezi kuwa mtu anayekatisha kauli za watu, unamalizia sentensi usizojua zingeishiaje, unataka wewe tu ndio usikilizwe na bado ukategemea utaheshimika. Umakini kwenye mazungumzo ni mtaji muhimu.
Swali, ni kwanini baadhi ya watu wana uwezo mkubwa wa kuwa makini kwenye mazungumzo kuliko wengine? Kwanini wapo watu wanaojua kusikiliza kuliko wengine? Je, tunazaliwa na umakini au tunajifunza?
Hili si swali rahisi. Lakini kwa ujumla tunaweza kusema, umakini ni matokeo ya kujitambua. Mtu yeyote anaweza kujifunza kuwa makini na akajitambua. Mtu anayejitambua kwa kawaida  ni mnyenyekevu kwa sababu anajua kuwa wengine, kama alivyo yeye, nao wanastahili kupewa heshima na kuthaminiwa kama alivyo yeye. Mtu anayejitambua si tu anaelewa upungufu wake lakini pia anafahamu namna gani upungufu huo unaweza kuathiri uhusiano wake na watu. Kwahiyo kujitambua ni pamoja na kuwajibika na kuchukua hatua za kurekebisha upungufu ulionao na kuufanyia kazi ili uwe mtu bora zaidi.
Njia mojawapo ya kujifunza kuwa mtu makini ni kupata muda wa kuwa peke yako. Hapa nina maana ya kupata nafasi ya kujitenga na watu kwa muda na kufunga milango yote inayokuletea taarifa kutoka nje ili uweze kufungua milango ya ndani mwako na kujisikiliza. Watu wengi hatuna tabia hii. Muda wote tunaongea na watu, tunasikiliza wengine wanasemaje, tunafuatilia yanayoendelea duniani na hatuna muda wa kutulia na kujisikiliza. Matokeo yake tunakuwa watu wenye kukata tamaa, tusio na furaha na wakati mwingine tunakosa umakini kwenye maisha.
Kwa muda sasa nimejenga tabia ya kujisikiliza. Kila siku ninatenga muda fulani kulingana na majukumu ya siku hiyo na kupata muda wa kutulia na kurudi ndani yangu. Katika hali hii ya utulivu, ninajitafakari, ninajiwekea kioo kiikague nafsi yangu, kinisaidie kujikosoa na kisha kinisaidia kutafakari namna ninavyoweza kujirekebisha. Nimeona faida yake.
Kwanza, ninapokuwa kwenye utulivu ninakuwa na uwezo mzuri zaidi wa kujielewa kuliko kusubiri watu wengine waniambie mimi ni nani. Utulivu unakuwa sawa na kufunga milango inayoingiza kila kitu kutoka nje na kufungu milango ya ndani yangu. Katika hali hii ya utulivu, ninakuwa na uwezo mzuri zaidi wa kubaini upungufu nilionao na kuufanyia kazi pasipokusubiri watu wengine waniambie. Kuna nyakati ninagundua niliwaudhi watu ambao hata pengine hawakuudhika, lakini nikajirekebisha kwa sababu nilitenda kinyume na kanuni zangu binafsi.
Lakini pia, katika nyakati hizi za utulivu, ninakuwa na muda wa kuweka mawazo yangu pamoja. Kwangu, namna nzuri zaidi ya kuweka mawazo yangu ni kuandika. Ninacho kitabu maalumu ninachokitumia kuandika mambo ninayoyatafakari. Kwa hiyo kwangu, njia nzuri ya kujitafakari ni kuandika.
Pia, katika nyakati hizi za utulivu, ninapokuwa mbali na watu, ninapokuwa nimejifungia mahali nisikoweza kufikiwa na watu, ninapokuwa nimezima simu na mitandao ninakuwa na wakati mzuri wa kujisomea mambo mbalimbali na hata kusikiliza hotuba za watu wenye maarifa mbalimbali. Utulivu huu unanisaidia kumaliza vitabu vinne vyenye ukubwa wa wastani kila mwezi. Bila utulivu, ni vigumu kupata muda wa kusoma kitabu na kukimaliza.
Katika maisha yangu halisi ya kila siku, nimeona kadri ninavyopata muda wa kuwa peke yangu, ninakuwa na unyenyekevu zaidi. Utulivu wa nafsi unanisaidia kutulia hata ninapozungumza na watu. Unaweza kujaribu na utaona matokeo yake.
Christian Bwaya ni mhadhiri wa saikolojia na unasihi, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Â Simu: 0754 870 815