29.9 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

Tahadhari ya ebola

Na mwandishi wetu – dar es salaam

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, amesema licha ya kuwa hakuna mgonjwa wa ebola aliyeripotiwa nchini, Serikali imeanza kuchukua tahadhari kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.

Dk. Ndugulile aliyasema hayo Dar es Salaam jana, ikiwa ni wiki moja tangu ugonjwa huo kuripotiwa kuua watu nchini Uganda, huku Kenya nako akiripotiwa kuwapo mgonjwa mmoja.

“Tanzania hatuna mgonjwa wa ebola, lakini kumekuwa na tatizo la ebola Congo (Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo – DRC) na Uganda ambako umeingia wiki iliyopita.

“Sisi kama Tanzania hatujaripoti mgonjwa yeyote ambaye ameugua ugonjwa huu, lakini kama Serikali tumeendelea kujipanga, kuhakikisha kwamba tunachukua tahadhari zote kuhakikisha tunajilinda dhidi ya ugonjwa huu kuingia ndani ya nchi,” alisema Dk. Ndugulile.

Dk. Ndugulile pia alisema wameweka mifumo ya ufuatiliaji watu wanaoingia nchini kupitia mipaka na viwanja vya ndege na kwa madereva wa magari makubwa yanayotoka nje ya nchi na wafanyabiashara.

“Kwa Watanzania wanaokwenda Congo tumeweka utaratibu wa kuwafuatilia wanaporejea nchini kwa kuangalia wapi walikuwa na shughuli walizokuwa wakizifanya na wanapoingia nchini wanakokwenda maeneo gani,” alisema.

Aliongeza kutokana na kufanya ufuatiliaji huo, itakuwa rahisi kujua sehemu alizopita na kuambukiza kwa kuwa jinsi ulivyo ugonjwa huo kila anayekutana naye ana uwezo wa kumwambukiza.

“Hivyo tunalazimika kufuatilia mnyororo mzima kujua idadi ya aliosalimiana nao na alijihusisha na jamii ipi ili kuhakikisha kuwa tuko salama,” alisema Ndugulile.

Alisema pia tayari kuna maeneo yametengwa kuwahifadhi wagonjwa, mifumo ya kimaabara, ufuatiliaji wa wahisiwa na mazoezi kwa wataalamu wa afya kwa ajili ya utayari.

“Tayari vifaa maalumu vimefungwa viwanja vya ndege na mipakani kuangalia kila anayeingia, wanaoenda Congo,” alisema.

Aliwataka wafanyabiashara kuendelea na shughuli zao ila akawataka wachukue tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.

Alitoa rai kwa wananchi kuhakikisha shughuli za uchumi zote zinaendelea bila kufunga mipaka kwa kuwa Tanzania bado iko salama, hatujawahi kupata mgonjwa.

Dk. Ndugulile alisema pamoja na kuwa hakuna mgonjwa aliyeripotiwa, Watanzania waendelee kuchukua tahadhari, hasa wanapomwona mtu ameugua au ana dalili za ugonjwa huo.

“Watanzania wachukue tahadhari wanapomwona mtu ama ameugua ghafla, ana homa kali, anatoka damu sehemu mbalimbali za mwili au kufariki ghafla, akiwa na dalili hizo watoe taarifa kwa mamlaka ili wataalamu wa afya wakafanye uchunguzi,” alisema Dk. Ndugulile.

Aliongeza kuwa kwa mtu aliyefariki akiwa na dalili hizo asizikwe kwanza, hadi wataalamu wafanye uchunguzi na wananchi wasijihusishe na masuala ya mazishi bila kujua kama ni ebola au ugonjwa unafanana.

MGONJWA ACHUNGUZWA KENYA

Katika hatua nyingine, mtu anayehisiwa kuwa na virusi vya ugonjwa wa ebola amewekwa kizuini katika Hospitali ya Kericho, eneo la Bonde la Ufa kusini-magharibi mwa Kenya.

Mgonjwa huyo ambaye ni mwanamke, anaripotiwa kuwa na dalili zinazowapata wagonjwa wa ebola.

Maofisa wa afya katika Kaunti ya Kericho, walisema mwanamke huyo alisafiri kutoka Malaba eneo la mpaka kati ya Kenya na Uganda.

Hakuna ripoti yoyote iliyotolewa ya kuwepo kwa ugonjwa wa ebola karibu na mpaka wa Malaba isipokuwa eneo la Magaharibi mwa Uganda.

Sampuli za damu za mgonjwa huyo zimechukuliwa kwa ajili ya kufanyiwa vipimo na matokeo yake yanatarajiwa kutoka baada ya saa 12-24.

Mamlaka za nchini Kenya zimesema kuwa mgonjwa huyo alikwenda hospitali binafsi siku ya Jumapili, alikuwa na homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya viungo, maumivu ya koo na alikuwa akitapika.

Alitibiwa malaria kwenye hospitali ndogo, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya .

Alifanyiwa tena kipimo cha malaria na majibu yalionesha hana malaria.

Kutokana na hali hiyo, wahudumu wa afya walimpa rufaa kwenda Hospitali ya Kaunti ya Kericho ambayo ina uwezo wa vifaa na kuhudumia wagonjwa wa ebola kwa kuwatenga.

Inaelezwa baada ya kufika katika hospitali hiyo, alianza kuharisha , lakini sasa taarifa zinasema anaendelea vyema.

Idara ya Huduma za Afya ya Kaunti ya Kericho, imesema inafuatilia kwa karibu suala hili na inafanya kazi pamoja na Serikali kuu kuhakikisha kuwa hatua madhubuti zinafuatwa kuhakikisha usalama wa kiafya kwa wengine.

Serikali ya Kaunti Kericho imetoa wito kwa watu kuwa watulivu na wenye subira.

Wiki iliyopita, mtoto wa kiume wa miaka mitano na bibi yake mwenye umri wa miaka 50 walifariki dunia nchini Uganda kwa ugonjwa wa ebola na Shirika la Afya Duniani (WHO) lilithibitisha.

Mtoto huyo, mdogo wake wa miaka mitatu  ambaye naye alitibiwa ugonjwa huo na bibi yake walitokea nchini DRC.

Tayari wahudumu 4, 700 nchini Uganda wamepewa chanjo dhidi ya ugonjwa huo.

Katika kipindi cha miezi 10, zaidi ya watu 2,000 wameripotiwa kuugua ebola, na wengine 1,400 kufariki nchini DRC. 

Mlipuko wa ebola ni wa pili kwa ukubwa nchini DRC, kukiwa na ripoti ya kutokea maambukizi mapya wiki za hivi karibuni.

Kuenea kwa kasi kwa ugonjwa huo kunatokana na wafanyakazi wa afya kutoaminika kutokana na machafuko nchini humo.

Watu hawawaamini watoa huduma za afya, hivyo watu wenye dalili za ugonjwa huo kushindwa kupata matibabu.

TAARIFA MUHIMU

Ebola ni ugonjwa unaosabibishwa na virusi ya homa ya hemoraji (yaani kumwaga damu sana). 

Kati ya watu 10 waliopata virusi vya ebola, wastani kati ya watano hadi tisa hufa. 

Virusi vyake husambaa haraka na kusababisha vifo zaidi ya asilimia 50 ya waathirika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles