27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

OPERESHENI LOLIONDO YAPOTOSHWA

Na Masyaga Matinyi

-Arusha

OPERESHENI inayoendelea kuwaondoa wavamizi kwenye mpaka na ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti (Senapa), haina uhusiano na eneo la kilomita za mraba 4,000 lenye mgogoro uliodumu kwa takribani miongo miwili.

Eneo hilo la kilomita za mraba 4,000 ambamo kuna vijiji 8, ni la Pori Tengefu Loliondo (LGCA), ambapo wataalamu wa uhifadhi kwa kipindi kirefu wamependekeza ligawanywe kwa lengo la kutenganisha kilomita za mraba 1,500, kwa ajili ya shughuli za uhifadhi na 2,500 zilizosalia kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Operesheni hiyo iliyoanza Jumapili iliyopita (Agosti 13, 2017), inafanywa kwa pamoja na askari wa Senapa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na askari polisi wilayani Ngorongoro.

Pia inafadhiliwa na Serikali kwa asilimia 100 kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), tofauti na taarifa zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kuna fedha ambazo zimetoka nje ya mfumo wa Serikali.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Mfaume Taka, alisema kuna kundi la wanaharakati ambao kwa makusudi wameamua kupotosha ukweli, kwa masilahi binafsi.

Alisema operesheni hiyo inahusisha eneo la mpaka wa Senapa, NCAA na LGCA, eneo ambalo lina urefu wa kilomita za mraba 90 na upana wa kilomita za mraba tano, hivyo ukubwa wa eneo la operesheni ni kilomita za mraba 450.

Taka alisema taarifa zinazosambaa kuwa ni operesheni ya kuwaondoa wananchi waliomo kwenye kilomita za mraba 1,500 si za kweli, kwani maamuzi ya ugawaji wa eneo hilo yanasubiri maagizo ya Waziri Mkuu.

Miongoni mwa taarifa za upotoshaji (nakala tunayo), ni ile iliyotolewa siku chache zilizopita na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Tanzania Human Rights Defenders Coalition (THRDC), Onesmo Olengurumwa.

Katika taarifa yake, Olengurumwa amedai kuwa hiyo imelenga kuwaondoa wenyeji wa eneo hilo kutoka kilomita za mraba 1,500 na kwamba nyumba za asili (maboma) yamechomwa moto, mifugo imepotea, wananchi wamepigwa na wengine kujeruhiwa kwa risasi.

Pia amedai mbali ya operesheni hiyo kuwahusisha askari wa Senapa, NCAA na polisi, lakini pia inashirikisha kampuni ya uwindaji wa kitalii katika eneo hilo, Ortello Business Cooperation (OBC).

Mkuu wa Wilaya alisema: “Jumapili iliyopita nimesikiliza taarifa za BBC na Reuters nikashangaa sana, eti maboma zaidi ya 50 yamechomwa moto, upotoshaji wa hali ya juu.

“Serikali ambao sisi ni wawakilishi wake, haipo kuonea mtu au watu, kwa hiyo hakuna aliyekurupuka na kuanza operesheni. Tulipita maeneo yote husika na kuyakagua, kazi ambayo ilihusisha madiwani na viongozi wengine.

“Na pia ni vizuri kuweka wazi kuwa yaliyochomwa si maboma, ni malanja (nyumba za muda) na malanja hayo yapo katika eneo la Senapa ambalo ni mpaka kisheria (buffer zone).

“Kazi inayoendelea ni kusafisha mpaka wa Serengeti, lakini kuna ambao tumewakuta ndani kabisa ya hifadhi, huku wakijua kabisa ni kinyume cha sheria kuishi na kuingiza mifugo. Hawa tumewakamata na kuwapeleka Mugumu, Serengeti wakashtakiwe.

“Tuliowakamata ndani ya hifadhi ni Marima Kairung, Otimbau Yiele, Setayi Lemian, Kipoye Taki na Saruni Taki. Hawa wanakwenda mahakamani.”

Pia alizitaka asasi za kiraia katika eneo hilo kuacha kutoa taarifa zenye upotoshaji, kwani taarifa hizo zimekuwa zikichanganya wananchi na kuipaka Serikali matope ndani na nje ya nchi.

“Baada ya ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Loliondo mwishoni mwa mwaka jana na kutoa maagizo kuwa NGOs hapa zihakikiwe, zilitulia nyingine zikahamishia shughuli zao Arusha. Sasa naona zinarejea tena baada ya operesheni kuanza,” alisema.

Tatizo la Loliondo tofauti na maeneo mengine ya hifadhi ni kuwapo migogoro inayochochewa na wanaharakati na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), mengi yakiwa yanatoka nje nchi au kuongozwa na wageni.

NGOs hizo zina ofisi katika vijiji vilivyomo ndani ya Pori Tengefu ambavyo ni Ololosokwan, Soitsambu, Oloipir, Olorian Maiduguri, Losoito Maaloni, Arash na Piyaya.

NGOs hizo ni Tanzania Pastoralists Community Forum, Ujamaa-CRT, PINGO’s Forum, Tanzania Pastoralists Hunter Gatherers  Organization, Pastoral    Women Council, CORDS, PALISEP, NGONET na Maasai Pastoralist Development Organization–Lareto.

Wiki iliyopita Serikali ilizionya NGO’s zilizopo Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha, kwa kuendelea kupokea fedha kutoka Uingereza na nchi jirani ili kuchochea na kuonyesha bado kuna mgogoro mkubwa.

Onyo hilo lilitolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ambaye alikanusha madai ya  askari kuchoma maboma ya wananchi, ambapo uchomaji huo unafanywa na mashirika hayo kwa lengo la kupotosha ukweli ili kuwashawishi wanaowapa fedha.

Profesa Maghembe alisema tayari Serikali ilikwishakuwatangazia wafugaji waliokuwa wakiishi na kufuga ndani na mpakani mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Loliondo kuondoka kwa hiari yao kabla ya kuondolewa kwa nguvu.

Operesheni hiyo iliyoanza Agosti 12, mwaka huu Kata za Piyaya, Arash, Maalon, Oleipiri, Soitsambu, Lorien na Ololosokwan imelenga kuwaondoa kwa nguvu wafugaji wote waliokaidi kuondoka kwa hiari.

Kazi hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli, inatekelezwa na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Ngorongoro, ikishirikiana na Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Serengeti, Kikosi Maalumu kutoka Senepa na NCAA.

Akifafanua kuhusu onyo la Serikali kwa NGO’s, Prof. Maghembe alisema zipo baadhi ya NGO’s ambazo hupokea fedha kwa ajili ya kuendelea kuonyesha eneo la Loliondo halijatulia.

“NGO’s hizi zinapata fedha zake kutoka Uingereza na nchi nyingine kwa kusema kwamba kuna mgogoro. Kwa hiyo ni lazima wachochee kuonyesha mgogoro ili nawao wapate fedha za kujikimu kimaisha yao, kwa hiyo Loliondo tuna shida.”

“NGO’s nyingine zilizoko pale ni za kutoka nchi jirani wala si za Tanzania. Nyote mnajua siku za karibuni rais ametoa onyo watu wenye mifugo ndani ya hifadhi waondoke.

“Na kama imekuwa mingi na hawawezi kuichunga mahali walipo basi wauze, sasa Loliondo kuna mifugo mingi sana kwenye Pori la Akiba la Loliondo,” alisema Prof. Maghembe.

Alisema pori hilo lina jumla ya kilomita za mraba 4,000 na kutokana na kuendelea kupanuka kwa jamii hiyo ya kifugaji, Serikali iliridhia kukata kilomita za mraba 2500 ili zitumiwe na wananchi.

Alisema Serikali katika kuonyesha inawajali wananchi wake, iliwapelekea maji na huduma nyingine za kijamii zinazotakiwa katika eneo hilo. Na eneo lililobakia la kilomita za mraba 1500 zikiendelea kuwa Pori la Akiba.

“Katika eneo hilo la kilomita za mraba 1,500, asilimia 51 ya eneo hilo lina vyanzo vya maji ya mito inayopeleka maji katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

“Kwa hiyo ni lazima eneo hilo libakie kuwa hifadhi. Lakini pia wanyama wanapotawanyika Serengeti kwenda Kaskazini na kutoka Kaskazini kwenda Kusini, hupitia kwenye eneo hilo la kilomita za mraba 1, 500,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles