Na MWANDISHI WETU-MBEYA
NAIBU Waziri wa Kilimo, Dk. Mary Mwanjelwa, amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, kumsimamisha kazi Ofisa Kilimo wa wilaya hiyo, anayesimamia zao la pareto, Emmanuel Halinga ili kupisha uchunguzi.
Agizo hilo alilitoa juzi wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Jojo, Kata ya Santilya akiwa kwenye ziara ya kikazi katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini baada ya Mbunge wa Mbeya Vijijini, Oran Njeza (CCM) na wananchi wote waliokuwapo kwenye mkutano huo wa hadhara kumrushia shutuma nzito na kumkataa mtaalamu huyo.
Dk. Mwanjelwa, alisema kuwa pamoja na zao hilo la pareto kuwa la kwanza kwa uzalishaji katika nchi za Afrika, huku likiwa la pili kwa uzalishaji duniani, lakini bado halijamkomboa mkulima nchini jambo ambalo linaonyesha namna ambavyo baadhi ya wataalamu wa kilimo wameshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Alisema kuwa wataalamu wa kilimo walipaswa kusimamia kwa kiasi kikubwa zao hilo kwani pato lake ni wastani wa tani 2,000 kwa mwaka sawa na Sh bilioni 12 hadi 14 na katika kipindi hiki bei ya kuanzia mkulima analipwa Sh 2,300 kwa kilo hadi 3,300 kulingana na ubora wa zao hilo.
Dk. Mwanjelwa, alitoa siku saba kwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Pareto nchini, Lucas Ayo, kutoa sababu za kwanini mnunuzi ni mmoja wa zao hilo jambo ambalo linaonyesha kuwa na harufu ya rushwa au kusababisha kudumaza soko la zao hilo kwa kuwa na mnunuzi mmoja asiyekuwa na ushindani.
“Mkishaanzisha tu vikundi vya vyama vya ushirika, mtoe taarifa mapema iwezekanavyo na Serikali kupitia mrajisi itatoa elimu ya ushirika,” alisema Dk. Mwanjelwa.
Ameagiza zao la pareto kuwa huru ili mkulima awe huru kuuza kwa mnunuzi anayemtaka kwani kwa sasa kuna mnunuzi mmoja tu ambaye anajipangia mwenyewe namna ya kununua zao hilo kwa gharama atakazo.