29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

BUNGE LAWAGOMEA WALIOFUKUZWA CUF

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA

BUNGE limeweka wazi kuwa haliwatambui wanachama wanane waliovuliwa uanachama na Chama cha Wananchi (CUF) na baadaye kutangazwa kuvuliwa nafasi zao za ubunge na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Wanachama hao waliokuwa wabunge wa viti maalumu, walivuliwa uanachama wao na Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba kutokana na ukosefu wa nidhamu.

Wanachama hao ni Saumu Sakala, Salma Mwassa, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Khadija Salum Al-Qassmy, Halima Ali Mohamed, Riziki Shahali Ngwali na Severina Mwijage.

Baada ya wabunge hao kufukuzwa, NEC ilifanya uteuzi wa wabunge wapya ambao ni Rukia Ahmed Kassim, Shamsia Mtamba, Kiza Mayeye, Zainab Mndolwa, Hindu Mwenda, Sonia Magogo, Alfredina Kahigi na Nuru Awadh Bafadhili.

Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Katibu wa Bunge, Steven Kigaigai, alisema anapenda umma ufahamu kwamba nafasi za ubunge zilizoachwa wazi baada ya wabunge husika kufukuzwa uanachama, zilijazwa na NEC.

Alisema nafasi hizo zilijazwa kwa mujibu wa sheria na waliopatikana kuzijaza, wanaendelea kutekeleza majukumu yao kibunge ipasavyo.

“Ni vema ifahamike kuwa hakuna sehemu yoyote katika uamuzi huo wa mahakama inapoelezwa kuwa wabunge hao wanatakiwa kurudishiwa ubunge wao,” alisema Kigaigai.

Alisema kilichoamuliwa na Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Novemba 10 mwaka huu, katika shauri namba 479 la mwaka 2017, lililofunguliwa na waliokuwa wabunge wanane wa Bunge la Tanzania wa viti maalumu kupitia CUF, ni uamuzi wa awali uliotolewa kwenye mapingamizi.

“Viongozi ambao waliamuru kuwa walalamikiwa wasitishe utekelezaji wa uamuzi wa kuwafukuza uanachama na vilevile kutojadili suala lolote kuhusu uanachama wa walalamikaji, hadi mahakama itakapokamilisha kusikiliza shauri la msingi, ambalo lilifunguliwa la kupinga uamuzi wa CUF kuwafukuza uanachama, na kwa mujibu wa kumbukumbu za mahakama bado uamuzi wa mwisho kuhusu shauri hilo haujatolewa,” alisema Kigaigai.

Alisema kumekuwa na tafsiri isiyokuwa sahihi ya uamuzi huo wa mahakama inayotolewa na baadhi ya watu na mitandao ya kijamii kusambaa taarifa potofu kuwa wabunge wa CUF wamerejeshwa.

Kigaigai alisema taarifa hizo si za kweli na kwamba Bunge halitambui jambo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles