29.9 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

ISMAIL JUMA MWANARIADHA ALIYEZIMIKA GHAFLA

Na ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM

NI simanzi katika tasnia ya michezo kutokana na kifo cha mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania, Ismail Juma.

Huzuni imekuwa kubwa kwa sababu kifo hicho ni cha ghafla huku tasnia ya riadha ikiwa bado inahitaji mchango wake kwenye harakati za kuiletea heshima Tanzania kupitia tasnia hiyo ya riadha.

Taarifa zilizotolewa na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) kupitia kwa Katibu wake, Wilhelm Gidabuday, zinasema kuwa mwanariadha huyo amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari akiwa kwenye pikipiki wakati akirejea nyumbani kwao Babati, Manyara.

Hakika mchezo wa riadha umepata pigo kubwa, Ismail atabaki kukumbukwa kwa yale aliyoyafanya hasa katika kupigania wanariadha wenzake chipukizi kufikia mafanikio.

Inakumbukwa kabla ya kukutwa na umauti, Ismail alitajwa kuwa miongoni mwa wanariadha wanaosaka nafasi ya kufuzu kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola yatakayofanyika Aprili mwakani huko Australia akiungana na wale 10 waliokwisha tajwa.

Ismail alikuwa katika orodha ya wale watakaotafuta viwango kwa mbio za mita 100, 200, 400 na 10,000 akiwa sambamba na Ally Hamis, Joseph Panga, Benjamin Michael, Adinan Chongole na Keneth Joram.

Kwa upande wa wanariadha wa miruko ni Anthon Miranga, Michael Gwandu na Michael Daniford, lengo likiwa kufikisha wanariadha 15 watakaokwenda Madola.

Mwanariadha huyo ameondoka, ila ataendelea kukumbukwa na wadau wa mchezo huo hasa wanariadha wenzake kwa mchango mkubwa aliokuwa akiutoa kipindi cha uhai wake licha ya umri mdogo alionao.

Kifo chake kinaacha kilio na simanzi kubwa ambapo mwanariadha huyo aliwahi kushiriki mashindano mengi ya kimataifa na kurejea na medali Tanzania na hivyo kuwa miongoni mwa wale wanaoitangaza vema nchi kimataifa.

Kabla ya kifo

Marehemu Ismail Juma, Jumapili iliyopita aliibuka mshindi wa mbio za nusu marathon za Istanbul zilizoandaliwa na Dar Rotary zilizofanyika Manyara, lakini pia ameshiriki katika mashindano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi akivunja rekodi ya mbio za Ngorongoro Marathon baada ya kumaliza wa kwanza kwa kutumia saa 1:02.48.

Septemba 16 mwaka huu, Ismail alivunja rekodi ya mwanariadha, Dickson Marwa wa Kenya aliyoiweka Februari 2008 mjini Abu Dhabi, katika Falme za Kiarabu alipotumia dakika 59:52 katika mbio za nusu marathon.

Katika rekodi aliyovunja Ismail, alitumia  dakika 59”30  mashindano yaliyofanyika jijini Mattoni Jamhuri ya Czech akimaliza wa tatu.

Simbu, Sarah Ramadhan wamlilia

Wanariadha wa kimataifa, Alphonce Simbu na Sarah Ramadhan, wanasema kuwa familia ya riadha imepata pigo ambalo haliwezi kuzibwa kwa haraka.

“Ismail alikuwa zaidi ya mdogo wangu kwani mara kwa mara tulikuwa tukiwasiliana na kuzungumza mambo mbalimbali kuhusu riadha.

Alikuwa akinieleza siku moja aje kuvunja rekodi nilizoziweka mimi. Nilimpa moyo wa kumwambia afanye juhudi mazoezini atafanikiwa, alikuwa kijana mwenye uchu wa mafanikio kweli, Mungu ampumzishe ndugu yetu kwa amani,” alisema Simbu.

Sarah alisema: “Nimeshtuka baada ya kupata taarifa za kifo chake, hivi karibuni nilikuwa nazungumza naye juu ya maandalizi yangu kuelekea michuano ya Madola, kwa kweli Taifa limepoteza nguvu kazi ambayo sidhani kama itakuja kutokea siku zijazo, kikubwa tumwombee apumzike kwa amani.”

Kauli ya Gidabuday

Katibu Mkuu wa RT anasema: “Ni majonzi kwangu binafsi, ni majonzi kwa familia ya riadha, alikuwa aingie kambini mwezi huu kujiandaa na mashindano ya Madola-2018.

“Nina hakika pengo lake haliwezi kuzibwa kirahisi na moja kati ya medali tulizozitegemea kwenye madola ilikuwa itoke kwake, jinsi nilivyokuwa nazungumza naye na alivyojipanga kuelekea madola hakika ni ngumu kumsahau, Mungu anayo mipango yake,” anaeleza kwa masikitiko.

Suleiman Nyambui

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa RT ambaye kwa sasa ni mwalimu wa mchezo huo nchini Brunei anasema: “Tunashukuru  Rais wa RT, Antony Mtaka, kwa kazi kubwa liyoifanya kuibua vijana wachanga kama Ismail, lakini Mungu ana mipango yake.

“Ni majonzi kwa familia yake, wanariadha, wanamichezo na Watanzania wote, kwa kile ulichokuwa umewekeza muda, akili na mali, mmojawapo ni huyo, ambaye alikuwa ni tegemeo ya kuleta medali katika mashindano ya Olimpiki 2020 Tokyo katika mbio za marathoni.”

Ishara ya matarajio ya marehemu kuleta marathoni, ni baada ya kuonyesha mwaka huu alipovunja rekodi ya Taifa ya mbio za nusu marathon 21.1 kwa muda wa chini ya dakika moja uliokuwa umewekwa na Dickson Marwa.

WASIFU WAKE

Ismail Juma alizaliwa Agosti 3, 1991, ni mwanariadha wa mbio ndefu ambaye alikuwa akishindana kwenye mbio za mita 10,000.

Mwaka 2015 katika michuano ya riadha ya dunia iliyofanyika China alishiriki mbio hizo lakini alishindwa kumaliza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles