MGOMBEA Urais wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayeungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, amelifunga jiji la Mbeya kwa mapokezi na kuomba kura akisema hana mchezo na kazi.
Pia, ameendelea kuwasisitizia wananchi, umuhimu wa kulinda kura zao baada ya kupiga hadi kitakapoeleweka.
Lowassa aliyasema hayo jana kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Ruanda Nzovwe vilivyopo jijini hapa.
“Wana Mbeya, kuna rafiki yangu aliniambia umeshinda, mwingine akasema huwezi kushinda kwa sababu wataiba kura. Mimi nasema nipeni kura nyingi hata wakiiba zitoshe, kaeni kituoni mpaka kieleweke, huu ni mwaka wa kuitoa CCM madarakani,” alisema Lowassa.
Lowassa aliueleza umma huo, kwamba kuna watu wanapita mitaani kutoa rushwa na kununua shahada za kura, lakini wasiwe na hofu nao.
“Wakikupa hizo hela, kula, akikupa laki tano, mwambie akupe milioni moja, akishakupa na akaendelea kukusumbua, mwambie asikusumbue hizo ni pesa za Lowassa.
“Mimi nataka mnitume nikawafanyie kazi, sina mchezo, nitaunda Serikali itakayofanya kazi kwa spidi ya 120 kwa saa,” alisema Lowassa.
FREEMAN MBOWE
Naye Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema wamegundua njama za kuiba kura zitakazofanywa na CCM usiku wa tarehe 24 kwa kupita mitaani na kugawa fedha za kura feki.
Ili kudhibiti hali hiyo, alisema siku hiyo Ukawa watafanya doria usiku kucha ili kuhakikisha hakuna fedha zinazogawiwa wala kura feki zitakazosambazwa.
“Nia ya Ukawa ya kupigania Katiba ya wananchi iko pale pale kwani Serikali ya awamu ya tano itaipigania kadri itakavyowezekana ili kiu ya wananchi juu ya Katiba hiyo ipatikane,” alisema Mbowe.
Alisema pia kwamba, uchaguzi wa mwaka huu ni wa kihistoria kwa kuwa unahusu maisha ya watu, watoto na utajibu maombi ya Watanzania.
Pamoja na hayo, alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), siyo huru na kwamba wanachama wa Chadema watahakikisha wanalinda kura zao.
“Kwa miaka 25 tumepiga kelele tukidai tume huru ya uchaguzi lakini kilio chetu hakikusikika kwa sababu CCM inajua tukiwa na tume huru, haiwezi kubaki madarakani.
“Kama tume yetu siyo huru, tuna wajibu wa ziada wa kulinda kura zetu. sheria inasema huturuhusiwi kusimama wala kukaa chini ya mita 200 kutoka kituoni. Kwa hiyo, ukihesabu mita 200 kutoka kituoni, una uhuru wa kuwa eneo hilo,
“Jambo hili limezua hofu ndani ya tume, ndani ya Serikali, ndani ya CCM na kwa Rais Jakaya Kikwete kwa sababu anasema tukishapiga kura, tukalale. Sasa namwambia Rais Kikwete ushauri huo akawape CCM, sisi hatuutaki,” alisema Mbowe.
Alisema pia kwamba, wanachama wa Chadema na wapenzi wao, hawatafanya fujo bali watakuwa na ujasiri wa kupiga na kulinda kura zao kwa sababu hakuna anayeweza kuzuia mpango wa Mungu kwa kutumia askari au nguvu.
FREDERICK SUMAYE
Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye, alisema kutokana na CCM kushindwa kuwatumikia wananchi kama ilivyowaahidi, leo hii kuna shule zimefungwa kwa takribani miezi mitatu kwa kukosa vyoo.
Kuhusu fedha za kutoa elimu bure, alisema Lowassa akiingia madarakani hana sababu ya kutegemea gesi asili bali anachotakiwa kufanya ni kuziba mianya ya wizi wa fedha.
Kwa mujibu wa Sumaye, kama wezi hao watadhibitiwa, zitapatikana fedha nyingi zitakazotumiwa kuwasomesha Watanzania pamoja na kuimarisha sekta ya afya.
MBEYA YASIMAMA
Wakati hayo yakiendelea, Lowassa aliyefika Mbeya mjini saa 10 jioni, alitumia takribani dakika 40 kufika kwenye uwanja wa mkutano.
Wakati akitoka kwenye uwanja wa ndege wa zamani wa mbeya kwenda uwanjani, baadhi ya vijana na akina mama waliokuwa wakisindikiza msafara huo, walikuwa wakifagia barabara, kupiga deni na wengine kutandika kanga ili gari la mgombea huyo lipite.
Alipofika jukwaani, zilitumika tena takribani dakika 10 kuwatuliza wananchi waliokuwa wakishangalia muda wote tangu mgombea urais huyo alipoanza kuingia uwanjani.
Msafara huo ulipofika eneo la Kabwe na Soweto, kulikuwa na kundi la wananchi waliozuia msafara wake na kumlazimu Lowassa kufungua sehemu ya juu ya gari lake na kuwapungia mkono wananchi.
Kwenye baadhi ya maeneo, polisi walilazimika kutumia nguvu ili kuwatawanya watu hao ambao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za hamasa na kufuta vumbi magari yaliyokuwa kwenye msafara huo kwa nguo zao.
Kutokana na uwanja wa Ruanda Nzovwe kufurika, barabara ya Mbeya -Tunduma inayopita karibu na uwanja huo, ilipitika kwa tabu kutokana na watu kusimama kwenye barabarani.
JOHN MREMA
Naye Meneja Kampeni wa CCM, John Mrema, alisema Serikali imewaongeza polisi posho kutoka Sh 180,000 hadi Sh 300,000 ambazo alisema zimeongezwa ili kuwashawishi askari polisi waweze kuiunga mkono CCM.
Pamoja na hayo, alisema posho hizo zitafutwa baada ya uchaguzi mkuu kupita kwa kuwa hazikuwa kwenye bajeti ya Serikali iliyopitishwa na Bunge Juni mwaka huu.