22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Dk. Magufuli Atamba

g3BAKARI KIMWANGA NA PETER FABIAN, MAGU

MGOMBEA Urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amewataka Watanzania wamchague awe rais kwani atateua waziri mkuu mchapakazi atakayesimamia shughuli za Serikali wakati wote.

Amesema kwamba, anahitaji kuwa na baraza dogo la mawaziri litakalokuwa tayari kwenda kwa wananchi kutatua kero zao.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya kampeni za lala salama zilizofanyika katika Majimbo ya Magu, Sumve, Kwimba na Misungwi mkoani Mwanza.

“Nazijua changamoto zinazowakabili Watanzania hasa wa Mkoa wa Mwanza ikiwamo kukosekana kwa soko la uhakika la pamba.

“Pamoja na wakulima wa pamba kujitahidi kulima na kulizalisha kwa wingi zao la pamba, bado wamekuwa wakikumbana na wanunuzi wajanja wanaowalangua kwa bei ya chini na kuwaacha wakilalamika.

“Kwa hiyo, nawakumbusha, zimebaki siku chache ili kura zipigwe na Magufuli ndiye rais ajaye wa awamu ya tano kwa sababu nimepita kila mkoa Watanzania wanasema hakuna zaidi ya Magufuli.

“Nipeni urais nami sitawaangusha kwa sababu kwangu mimi ni kazi tu!. Ninasema hapa, kwamba nitateua waziri mkuu mchapakazi atakayesimamia mawaziri wengine.

“Pia, nikiwa rais sitaweza kuteua mawaziri wasioweza kufanya kazi ya kutatua kero za Watanzania kwa wakati,” alisema Dk. Magufuli.

Akizungumzia mkakati wa kuondoa mdororo wa zao la pamba kwa wakulima nchini, Dk. Magufuli alisema amejipanga kuhakikisha anajenga uchumi imara wa viwanda.

“Nitasimamia zao la pamba kwa kuliinua ili wananchi wapate bei nzuri na hii itakuwa kazi ya kwanza kwa waziri wangu wa kilimo kuhakikisha anafufua zao hilo pamoja na kufufua viwanda vya kuchambulia pamba vikiwamo vya Nyambiti na Magu.

“Ninataka kujenga uchumi wa viwanda na tutaujenga ili tuweze kuzalisha nyuzi na nguo badala ya kusafirisha marobota nje ya nchi ambako wanatengeneza nguo na kuanza kuzivaa kisha wanatuletea kama mitumba.

“Tutazalisha nguo hapa hapa kwetu na wakulima mtauza pamba yenu na tutatengeneza nguo zetu na kuzisafirisha nje tena kwa kutumia pamba yetu” alisema Dk. Magufuli

Alisema pia kwamba, anajua mikoa ya kanda ya ziwa kuna wafugaji wengi wa ng’ombe, lakini ukosekanaji wa kiwanda cha nyama na ngozi, umesababisha kukosekana kwa bei ya uhakika wa mifugo yao.

 

“Ninataka kuwaambia kwamba, kama tutajenga kiwanda cha kuchakata na kusindika nyama, mazao haya ya ngozi yatakuwa na thamani kubwa.

“Na Serikali ya Magufuli itakuwa ya viwanda ndio maana nasema tukijenga uchumi imara wa viwanda, tutaweza kutoa ajira kwa vijana wetu na tutapandisha pia thamani ya ng’ombe na ngozi.

“Haiwezekani nchi kama Ethiopia leo inazalisha viatu na mikanda, lakini ngozi inatoka hapa kwetu Tanzania, Serikali ya Magufuli inakuja kuijenga Tanzania mpya,” alisema.

Akizungumzia kero ya maji katika mji wa Magu, Dk. Magufuli alisema anaijua changamoto hiyo huku akiutaka uongozi wa halmashauri hiyo kuanza kuitatua ili wananchi waweze kupata maji.

Aliwataka Watanzania kutofanya makosa kwa kuhakikisha wanamchagua yeye ifikapo Oktoba 25 mwaka huu ili aweze kuwatumikia na kuleta mabadiliko ya kweli yenye uchumi imara.

“Nimekwenda, Arusha, Monduli, Kilimanjaro, Shinyanga, Simiyu, Geita, Kagera, Tanga, Morogoro na maeneo mengi, kote huko wanasema Rais ni Magufuli, je wewe unangoja nini?

“Usipoteze kura yako kwa watu ambao hawawezi kushinda, nipigieni kura zote mimi,” alisema Dk. Magufuli

Msafara wazuiwa

Akiwa njiani kuelekea wilayani Magu, msafara wa mgombea huyo ulijikuta ukizuiwa zaidi ya mara nane na kulazimia kusimama na kuomba kura.

Alipokuwa akitoka jijini Mwanza, alizuiwa na wananchi katika baadhi ya maeneo ya Mabatini, Buzuluga, Nyakato na Igoma.

Akiwa katika Kijiji cha Hungumalwa wilayani Misungwi, alisema Serikali yake itahakikisha inawawezesha wachimbaji wadogo kwa kuwapa maeneo ya kuchimba madini pamoja na vifaa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles