30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

Daktari: Mbasha hakubaka shemeji yake

Emmanuel Mbasha
Emmanuel Mbasha

Na Veronica Romwald, Dar es Salaam
VIPIMO vya kimaabara alivyofanyiwa binti wa miaka 17 ambaye anadaiwa kubakwa na mfanyabiashara na mwimbaji wa muziki wa injili, Emmanuel Mbasha, havijaonyesha kama alifanyiwa kitendo hicho.
Ushahidi huo umetolewa jana na daktari Migole Mtuka wa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
Mbele ya Hakimu Flora Mjaya, Dk. Mtuka alisema Mei 26, mwaka jana, binti huyo – ndugu wa mwimbaji wa nyimbo za injili, Flora Mbasha, mke wa Emmanuel Mbasha – alifikishwa katika hospitali hiyo na kudai amebakwa.
Dk. Mtuka alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo, alimfanyia kipimo cha macho na kisha kutaka kumfanyia kipimo cha kimaabara ambacho hutolewa bure hospitalini hapo.
Alisema hata hivyo binti huyo hakupima kipimo hicho badala yake alirudishwa nyumbani.
“Alirudishwa hospitalini siku nane baadaye, yaani Juni 3, mwaka jana na nilipomfanyia kipimo hicho sikuona chochote, nikawajazia katika PF3 kile nilichokiona,” alisema Dk. Mtuka.
Mara baada ya daktari huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, waliingia mashahidi wengine wawili ndani ya chumba cha mahakama kwa ajili ya kutoa ushahidi wao.
Hata hivyo, mahakama haikuweza kusikiliza ushahidi huo baada ya kupata taarifa za msiba wa mmoja wa mahakimu aliyewahi kufanya kazi katika mahakama hiyo kabla ya kuhamishwa.
Kutokana na hali hiyo, Hakimu Mjaya alihairisha kesi hiyo hadi Aprili 20, mwaka huu ambapo itatajwa tena kwa ajili ya kuwasikiliza mashahidi hao.
Mbasha anadaiwa kumbaka binti huyo mwenye umri wa miaka 17, ambaye ni shemeji yake kati ya Mei 23 na 25 mwaka jana eneo la Tabata jijini Dar es Salaam ambako alikuwa akiishi naye.
Septemba 5 mwaka jana, binti huyo aliieleza mahakama kwamba alibakwa na shemeji yake huyo kwa awamu mbili tofauti kabla ya kufanikiwa kukimbia.
Kesi hiyo inasikilizwa mahakamani kwa siri kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai ya mwaka 2003 sura ya 20 kifungu cha 186, kifungu kidogo cha tatu ili kulinda haki ya binti huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles