27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Sitta asimamisha vigogo watano TRL

samuelNA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Uchukuzi, Samuel Sitta, amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Reli Tanzania (TRL), Kipallo Kisamfu na wengine wanne ili kupisha uchunguzi wa kashfa ya uingizaji wa mabehewa feki ya mizigo yaliyoigharimu Serikali Sh bilioni 230.
Viongozi wengine waliosimamishwa ni Mkuu wa Mitandao, Ngosomwile Ngosomiles, Mhasibu Mkuu, Mbaraka Mchopa, Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Jasper Kisiranga na Meneja Mkuu wa Manunuzi, Ferdinand Soka.
Alitangaza uamuzi huo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ripoti alizopewa za uingizwaji wa mabehewa mabovu 150 na suala la aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Madeni Kipande.
Kutokana na uamuzi huo, Waziri Sitta alimteua Mhandisi Elias Mshana kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa TRL.
Alisema mabehewa mabovu yaliingizwa nchini mwaka jana kupitia kandarasi ya Kampuni ya M/S Hindustan Engineering and Industrial Limited ya India, ambako imebainika pamoja na ubovu huo, yalikuwa yamelipiwa asilimia 100 ya gharama zote ambazo ni Sh bilioni 230.
Alisema sababu zilizomfanya kuwasimamisha kazi viongozi hao ni kuhusika kwao kuingiza mabehewa ambayo yana kasoro, uzembe katika uagizaji na ufuatiliaji kiwandani yalipokuwa yakitengenezwa.
“Huu ni uzembe na hujuma, mimi kama kiongozi sitamstahi yeyote atakayekuwa sehemu ya hujuma hiyo,” alisema Sitta.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini kama kulikuwa na hujuma.
Alisema ameunda kamati itakayoongozwa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru), Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi katika Sekta ya Umma (PPR) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Waziri Sitta ametoa muda wa wiki tatu kuanzia Aprili 20 mwaka huu kwa ajili ya kukamilisha uchunguzi wa sakata hilo.
Kuhusu Kipande aliyesimamishwa kazi, Waziri Sitta alisema timu iliyokuwa inachunguza tuhuma zake imekamilisha kazi na kuikabidhi Machi 24, mwaka huu ili hatua za kisheria zichukuliwe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles