Na AZIZA MASOUD- DAR ES SALAAM
RAIS John Magufuli ameweka rekodi mpya ya kulipa deni la taifa ambayo haikuwahi kufikiwa katika kipindi cha miaka 12 iliyopita.
Katika rekodi yake hiyo mpya, Rais Magufuli amefanikiwa kulipa deni la taifa la ndani na nje ya nchi katika kipindi kifupi cha miezi mitatu kwa kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa na mtangulizi wake, Rais Jakaya Kikwete, katika kipindi chote cha miaka 10 aliyokaa madarakani.
Kwa mujibu wa taarifa ya hali ya uchumi wa taifa iliyotolewa jana mbele ya waandishi wa habari na Gavana wa Benki Kuu (BoT), Profesa Benno Ndulu ofisini kwake Dar es Salaam, Rais Magufuli amelipa shilingi bilioni 99 za deni la ndani na amelipa pia Dola za Marekani milioni 90 za deni la nje kwa muda wa siku 90.
Taarifa hiyo ya Gavana Ndulu inaonyesha kuwa kasi hiyo ya ulipaji deni la taifa kwa fedha za ndani ambalo hivi sasa limefikia shilingi trilioni 51 haijawahi kufikiwa kipindi chote cha Serikali ya awamu ya nne.
“Serikali imelipa Dola za Marekani milioni 90 kwa deni la nje ambazo ni sehemu ya Dola za Marekani bilioni 600 zilizokopwa Benki ya Stanbic na imelipa pia shilingi bilioni 99 za deni la ndani.
“Ninaposema limelipwa si kwamba Serikali haikopi kabisa, hapana, kinachofanyika kwa sasa fedha zinazokopwa ni ndogo kuliko zile zinazolipwa tofauti na ilivyokuwa kipindi cha nyuma.
“Utaratibu huo wa ulipaji uliwahi kutokea kati ya mwaka 2003 na 2004 na unaweza kupunguza kasi ya kuongezeka deni la taifa,” alisema Gavana Ndulu.
Katika mkutano huo, Gavana Ndulu alizungumzia pia mwenendo wa ukuaji uchumi kwa nusu mwaka unaoanzia Januari mpaka Juni 2016 kwa kueleza kuwa ukuaji wa pato la taifa umeongezeka hadi kufikia asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.
Alizitaja sekta zilizochangia kuongezeka kwa ukuaji wa uchumi wa taifa kuwa ni uchukuzi na uhifadhi wa mizigo ambayo ni asilimia 17.4, uchimbaji madini na gesi asilimia 13.7, mawasiliano asilimia 13.0 na sekta ya fedha na bima asilimia 13.0.
“Hizo ni sekta zinazosaidia kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, kuna vipimo vinavyokwenda kwa sekta pia vipo vya uchangiaji kwenye ukuaji. Hivi sasa kilimo katika kota ya pili ukuaji wake umeongezeka kwa asilimia 3.4 kwa sababu ya kasi ya uuzaji wa mazao ya nje.
“Katika kipindi hiki cha nusu ya kwanza ya mwaka, sekta ya kilimo katika uchumi na uzito wake ni mkubwa kuliko sekta nyingine yoyote,” alisema Gavana Ndulu.
Alitaja pia sekta ya utalii kuwa ndiyo inayoongoza kwa kuingiza fedha za kigeni kutokana na ongezeko la idadi ya watalii nchini mwaka hadi mwaka.
“Idadi ya watalii kwa mwaka huu mpaka Juni ni 1,137,142 wakati kwa mwaka jana walikuwa 1,075, 541. Hili ni ongezeko la asilimia 5.8,” alisema Gavana Ndulu.
Sekta nyingine aliyoitaja kuingiza fedha nyingi za kigeni ni usafirishaji wa mizigo katika nchi jirani zikiwamo Zambia na Burundi.
“Mpaka Juni, mizigo inayopitia hapa nchini kwenda Zambia iliongezeka kwa asilimia 3.7, Burundi usafirishaji wa mizigo yao uliongezeka kwa asilimia 5.8, Rwanda asilimia 17.5, Malawi asilimia 14 na Uganda asilimia 22.5.
“Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo (DRC) mizigo imepungua hadi kufikia asilimia 12.7 na hii imechangiwa na kuporomoka kwa Randi ya Afrika Kusini ambayo inasababisha gharama ya kusafirishia mizigo nchini humo kupungua.
Aidha, Gavana Ndulu alisema mauzo ya bidhaa nje yameongezeka hadi kufikia asilimia 12.7 kwa sekta ya viwanda na mauzo ya dhahabu yameingiza Sh bilioni 1.3 kutoka Sh bilioni 1.2 kwa mwaka jana.
Alisema BoT imeangalia utekelezaji wa bajeti iliyopangwa na Serikali kwa mwaka 2016/2017 na kugundua kuwa kiwango kikubwa cha fedha zinazotekeleza miradi ya maendeleo zinatokana na makusanyo ya ndani.
“Hii si ripoti ya Wizara ya Fedha bali sisi kama banker (watu wa sekta ya benki) wa Serikali tunaona kinachoingia na kutoka, utendaji wa Serikali kwa upande wa mapato kila mwezi hasa Julai na Agosti, Serikali imezidi malengo kwa makusanyo ya ndani.
“Hakuna fedha nyingi za nje zilizopatikana na matumizi karibu yote yamelipiwa na fedha za ndani kuanzia matumizi ya shilingi mpaka fedha za kigeni yamefanyika kwa kutumia fedha zetu wenyewe,” alisema Prof. Ndulu.
Alifafanua kuwa licha ya matumizi kufanyika kwa fedha za ndani na nje, akiba ya fedha za kigeni iliyopo ni zaidi ya Dola za Marekani bilioni nne.
Alisema kwa mwenendo wa sasa lengo la ukuaji wa pato la taifa kwa asilimia 7.2 kwa mwaka 2016 litafikiwa.
Akizungumzia ukuaji wa pato la taifa kwa robo ya pili ya mwaka, alisema umefikia asilimia 7.9 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 5.8 kwa mwaka jana katika kipindi kama hicho.
Alivitaja vichocheo vilivyosababisha ukuaji huo kuwa ni pamoja na usafirishaji, madini na gesi.
“Shughuli za uchumi zilizochangia kukuza pato la taifa ni pamoja na usafirishaji na uhifadhi wa mizigo kwa asilimia 30.6. Katika usafirishaji kuna vichocheo viwili ambavyo ni usafirishaji wa abiria kwa njia ya barabara na gesi asilia ulioongezeka kwa asilimia 44.
“Usafirishaji wa reli pia umekuwa baada ya kuongezeka kwa mabehewa. Mwaka huu abiria wameongezeka kwa asilimia 77. Sekta nyingine ni uchimbaji wa madini na gesi ambao umesaidia kwa asilimia 20.5 ambayo kwa mwaka jana ilikuwa asilimia 11.2,” alisema Gavana Ndulu.