29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 6, 2023

Contact us: [email protected]

Maalim Seif atua Dar kimyakimya

Maalim Seif Sharif Hamad
Maalim Seif Sharif Hamad

NA EVANS MAGEGE,

KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, ametua jijini Dar es Salaam kimyakimya ingawa hakutokea kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho zilizopo Buguruni kama ilivyokuwa imetangazwa.

Kufika kwa Maalim Seif katika ofisi za makao makuu Buguruni kulitangazwa juzi na Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Uhusiano wa Umma, Mbarara Maharagande, alipohojiwa na gazeti la Mtanzania na kueleza kuwa atasindikizwa na wabunge wanane wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, mameya na madiwani.

Maharagande alisema Maalim Seif angeripoti Buguruni jana saa 2:00 asubuhi na kupokewa na wanachama wa CUF wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao pia wangewakaribisha wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa waliotarajiwa kuambatana na Seif kutoka Zanzibar walikoketi kutengeneza kile alichokiita mustakabali muhimu wa chama.

Hata hivyo, taarifa kuwa Maalim hatatokea Buguruni zilianza kusambaa juzi jioni kwenye mitandao ya kijamii kwa madai ya sababu za kiusalama.

Taarifa ya maandishi iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikiwa na jina la Mbunge wa chama hicho, Riziki Shaibu, ilieleza kuwa mapokezi ya Maalim Seif, wajumbe wa Baraza Kuu na Kamati ya Uongozi yameahirishwa baada ya kupatikana taarifa za kuwepo kikundi hatari cha watu wanaoishi ndani ya ofisi ya CUF Buguruni kwa sasa.

“Tunazo taarifa kuwa yapo makundi hatari ya watu yanayoishi ndani ya ofisi huku yakilindwa na vyombo vya dola tangu ofisi hiyo iporwe na aliyewahi kuwa mwanachama na kiongozi wa juu wa CUF, Prof. Lipumba (Ibrahim) akishirikiana na watu wanaomuunga mkono.

“Wakati tunaahirisha mapokezi ya kesho tunajipa muda wa kushauriana na viongozi wa juu wa chama chetu huku tukiwaomba wanachama wote walioko Dar, mikoani na Zanzibar kwani chama na viongozi makini hawawezi kuwa tayari kuona maisha na usalama wa wanachama na viongozi vinahatarishwa kwa kugeuza ofisi kuu kuwa uwanja wa mapambano,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Mbali na taarifa hiyo, akizungumza na gazeti hili mmoja wa watu wa karibu na Maalim Seif alisema kiongozi huyo alikuwa tayari ametua Jijini Dar es Salaam jana.

“Aliyetangaza kwamba atakwenda ofisi za CUF, Buguruni si Maalim Seif mwenyewe, ni kiongozi wa wabunge na madiwani, na wao wamekwishatoa tamko lao” alisema mtu huyo.

Maalim Seif ametua Dar es Salaam siku moja baada ya viongozi wakuu wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kutangaza kukutana.

Jana katika ofisi hizo Buguruni, Prof. Lipumba alitumia muda wake mwingi kumsubiri Maalim Seif na ujumbe wake lakini hakutokea na baadaye alifanya mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa mkutano.

Akizungumza katika mkutano huo, Prof. Lipumba alisema alifika ofisini hapo saa 1.45 asubuhi kumsubiri katibu mkuu wake ili ampangie miongozo ya utendaji kazi wa chama.

Alisema taarifa kuwa Maalim Seif angeripoti ofisini Buguruni alizipata kupitia kwenye vyombo vya habari na kuamua kuwahi ofisini ili akifika ampangie kazi za kukijenga na kukiimarisha chama.

“Sina taarifa rasmi ya ugeni wake lakini nimesikia kwenye vyombo vya habari jana (juzi) kwamba Katibu Mkuu atakuja akifuatana na wabunge na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi, sasa kuweka sawa hili naomba ifahamike Maalim Seif ndiye Katibu Mkuu wa chama chetu na ana ofisi hapa.

“Kwa hiyo yeye wakati wowote kuja ni jambo la kawaida, lakini tangu nimeanza kufanya shughuli za kichama sijamuona. Hata hivyo, wakati wowote anaweza kuja wala hana haja ya kutangaza kwa sababu hapa ni ofisini kwake, aje anione Mwenyekiti nimpe miongozo ya kiutendaji.

“Nimekuja saa mbili kasoro robo hapa ofisini, tangu nimeingia sijawaona wabunge kwa hiyo nilistaajabu kusikia watamsindikiza kwa sababu kwa kawaida inatakiwa Katibu Mkuu wa chama anapokuja kwenye ofisi zake za chama haji kwa kusindikizwa.

“Yeye anakuja kufanya kazi zake za kawaida, anaweza akaja na vijana waliopo hapa ni walinzi wa chama wanafahamu Katibu Mkuu kuwa ni kiongozi wao,” alisema Prof. Lipumba.

Alipoulizwa mtizamo wake kuhusu uamuzi wa wabunge wa chama hicho kumsindikiza Maalim Seif katika ofisi kuu za Buguruni, alisema wakati mwafaka ukifika atafanya nao mazungumzo.

Alisema kinachofanyika sasa ni jitihada za kurejesha umoja ndani ya chama kwa waasisi na wazee na kutafuta nafasi ya kuketi kwenye meza ya mazungumzo na Maalim Seif.

“Hatujawapangia muda wa kukamilisha mazungumzo yao na Seif, lakini nina imani hakutakuwa na tatizo kabisa. Tunatarajia mambo yatakwenda vizuri kisha tutaanza kuzunguka wilayani na mikoani kujenga chama,” alisema Prof. Lipumba.

Aidha, alipoulizwa kuhusu hali ya kifedha ya chama, alisema baada ya kuingia ofisini kwake alitaarifiwa kuwa akaunti zote za chama hazina fedha.

Alisema anakusudia kupangua safu ya wakurugenzi wa idara mbalimbali za chama hicho na kuteua wapya ili kuimarisha utendaji kazi.

“Suala la fedha linasimamiwa na bodi ya wadhamini wa chama na Katibu Mkuu,  Maalim Seif ndiye mhasibu mkuu.

“Kwa taarifa nilizonazo mpaka sasa hakuna senti yoyote iliyopo katika akaunti yetu ya benki na sababu nilizoambiwa ni kwamba fedha nyingi zilitumika katika mkutano mkuu ambao haukuwa na ulazima wa kuwapo kwa hiyo hali yetu si nzuri kifedha na kuna taratibu muhimu tunataka kuzichukua katika hali hii,” alisema Prof. Lipumba.

Akizungumzia taarifa zilizoenea kuwa ofisi hizo zinalindwa na Jeshi la Polisi, alisema hazina ukweli kwa sababu hawajaona polisi tangu alipofika ofisini hapo.

“Tangu nimefika hapa ofisini sijaona polisi wala sijakutana na polisi na hakuna polisi aliyekuja ofisini kwangu au wenzangu mmemuona mnionyeshe?” alihoji Prof. Lipumba

Mwenyekiti huyo wa CUF alieleza pia kuwa hatarajii wanachama wa chama hicho wa upande wa Zanzibar kujiunga na chama kingine cha siasa kwa sababu wanaujua uchungu wa kukijenga chama hicho.

“Ninavyowajua wana – CUF na waasisi wa chama hicho kutoka Zanzibar kuwashawishi wahamie Chadema watakwambia ni heri kufa kuliko kujiunga Chadema, hivi niwaulizeni katika maandamano ya kutetea haki ya demokrasia Zanzibar ni viongozi gani wa Chadema walikuwa mstari wa mbele kuwatetea Wazanzibari? Kwa hiyo siamini wana – CUF Zanzibar watafanya hivyo,” alisema Prof. Lipumba na kuongeza:

“Maalim ana walinzi wa Serikali kwa nafasi yake ya Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Kiongozi mstaafu na ana walinzi wa chama kama Katibu Mkuu.

“Hapa kwenye ofisi yetu kuna walinzi wa chama, Blue Guard, wengi anawafahamu hata kwa sura kwa hiyo hana haja ya kwenda polisi kuomba ulinzi wa kuja kwenye ofisi za chama.

“Wajue kuwa Mwenyekiti wa CUF mpaka uchaguzi ujao ni Profesa Lipumba na Katibu Mkuu ni Maalim Seif, hivyo utaratibu wowote wa mambo ya kichama unafuata matakwa ya katiba na si mitandao ya kijamii,” alisema.

Jitihada za kumpata Maalim Seif na wasaidizi wake wa karibu kuzungumzia kushindwa kwake kufika Buguruni hazikuweza kuzaa matunda mpaka sasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
580,000SubscribersSubscribe

Latest Articles