THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, ametaja kilichosababisha timu yake ishindwe kuvuna pointi tatu katika michezo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Zahera, alisema amebaini baadhi ya wachezaji wake wamekuwa wakishindwa kucheza dakika tisini kwa kiwango cha juu kutokana na kuchoka.
Alitolea mfano wa mchezo wao wa juzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Singida United uliomalizika kwa suluhu kwa kusema wachezaji wake walionekana kukata pumzi hivyo kushindwa kufanya kile ambacho walikikusudia.
“Katika mechi tulizocheza za hivi karibuni, wachezaji wangu wameshindwa kufanya kile ambacho nimekuwa nikiwaelekeza, ukimwangalia Matheo Antony na Haritier Makambo, wameonekana kukosa umakini kabisa wanapoingia eneo la hatari la mpinzani.
“Hata katika michezo ya nyuma hali hiyo ilionekana na iliendelea tena katika mchezo dhidi ya Singida United,” alisema Zahera.
Akimwelezea Makambo, alisema mshambuliaji huyo
ameonekana kushuka kiwango
tangu aliporejea nchini kutoka nchini kwake Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
“Kwenye mchezo wetu na Coastal Union nilimtoa
Ibrahim Ajib baada ya kugundua ametoka mchezoni.
“Juzi pia sikuweza kumtumia Haruna Moshi ‘Boban’, kwani nilikuwa nataka kumpumzisha, ukiangalia bado tuna mechi ya ugenini dhidi ya JKT Tanzania kule Tanga,” alisema.
Yanga imeshindwa kuibuka na ushindi katika michezo yake miwili mfululizo ya hivi karibuni ya Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo ni dhidi ya Coastal Union ilipolazimisha sare ya bao 1-1 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na suluhu ya juzi dhidi ya Singida United, Uwanja wa Namfua.
Katika hatua nyingine, kikosi cha Yanga kiliondoka mkoani Singida jana kwenda Tanga ambako itashuka dimbani Jumapili kuumana na JKT Tanzania, Uwanja wa Mkwakwani.
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 55, baada ya kushuka dimbani mara 22, ikishinda 17, sare nne na kupoteza mmoja.