PATRICIA KIMELEMETA
BARAZA Kuu la Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi nchini (Tucta) linatarajia kukutana Aprili 2 ambalo pamoja na mambo mengine, litajadili mapendekezo ya kima cha chini cha mishahara.
Akizungumza na gazeti hili Jijini Dar es Salaam jana, Rais wa Shirikisho hilo, Tumaini Nyamhokya alisema kuwa, baraza hilo pia litajadili maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Mbeya ambapo Rais, Dk. John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Alisema kwa sasa Kamati maalumu ya kushughulikia mishahara iliweza kufanya utafiti kuhusiana na hali halisi ya maisha kwa sasa, kima cha chini cha mishahara wanaopata wafanyakazi, gharama za pango na matumizi mengine ili waweze kuleta mapendekezo yao.
“Kuna kamati maalumu ya mishahara ambayo ipo kwa mujibu wa katiba yetu,inafanya kazi ya kuangalia hali halisi ya maisha ya wafanyakazi kwa sasa, kima cha chini cha mshahara wanaopata, gharama za pango na nauli na matumizi mengine wanayokumbana nayo, wanatarajia kuwasilisha mapendekezo yao kwenye kikao cha Baraza Kuu kinachotarajiwa kufanyika Aprili 2 mwaka huu,”alisema Nyamhokya.
Aliongeza mara baada ya kumalizika kwa kikao cha baraza hilo, wataweza kuangalia kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta zote binafsi na serikali ili waweze kuwasilisha mapendekezo yao kwa Rais Magufuli siku ya wafanyakazi.
Alisema mpaka sasa, wafanyakazi wanapata kiasi kidogo cha mishahara ambacho hakiwezi kukidhi mahitaji ya kila siku ukilinganisha na kupanda kwa gharama za maisha.
Alisema licha ya kuwasilisha mapendekezo ya kuiomba serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara ili uweze kufikia 750,000 kwa wafanyakazi wa serikali, lakini mpaka sasa bado wanapokea Sh 375,000.
“Wafanyakazi wa serikali wanapata kima cha chini cha mshahara kuanzia Sh 375,000 na kuendelea, huku sekta binafsi wakipata kuanzia Sh 100,000 kwa mwezi kulingana na ofisi anayofanyia kazi,”alisema.
Aliongeza kiasi hicho ni kidogo na kwamba hakiwezi kukidhi gharama za maisha, jambo ambalo limechangia kujitokeza kwa malalamiko ya kupanda kwa gharama za maisha.
Alisema lakini pia, wameiomba serikali kupunguza gharama za kodi inayokatwa kwenye mishahara yao ambayo imekua kero ya muda mrefu, jambo ambalo litasaidia kumpunguzia mzigo mfanyakazi kutokana na hali ngumu ya maisha.