25.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Dar kinara biashara ya binadamu- Lugola

Felix Mwagara-Zanzibar

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, amesema Dar es Salaam inaongoza kwa biashara ya kusafirisha binadamu huku akitoa onyo kali kwa wanaojihusisha na biashara hiyo.

Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo ya siku tano ya watekelezaji wa sheria ya kuzuia biashara hiyo haramu, katika hoteli ya Ngalawa, mjini Unguja, Zanzibar, Lugola alisema wanaofanya kazi hiyo waiache mara moja maana Serikali itawashughulikia.

“Tatizo hili linaweza onekana likawa dogo, lakini ukweli ni kwamba sote tunafahamu ni kubwa na limeendelea kukua kila mwaka.

“Uzoefu wa utendaji kutoka sekretareti hususan kutokana na wahanga wanaookolewa unaonyesha biashara hii inafanyika sana Mkoa wa Dar es Salaam Tanga, Mwanza, Kigoma, Geita, Dodoma, Singida, Arusha, Manyara, Shinyanga na Tanzania Zanzibar,” alisema Lugola.

Lugola alisema licha ya changamoto hizo,   Serikali katika kipindi cha kuanzia Januari mpaka Desemba 2018 imewaokoa   Watanzania 147 waliokuwa waathirika wa biashara haramu ya usafirishaji binadamu. Kati ya waathirika  141walikuwa wakitumikishwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Pia Lugola alisema waathirika sita walikuwa wakitumikishwa nje ya nchi ambako watano waliokolewa kutoka Thailand na   mmoja kutoka Malaysia, na  mmoja mwingine aliokolewa   nchini alipokuwa akitumikishwa na taratibu za kumrudisha kwao Msumbiji   zinafanyika.

“Napenda kuwahakikishia Watanzania wote kuwa hatutamuacha salama mtu yeyote anayejihusisha na biashara hii, waiache mara moja kabla mkono wa sheria haujawafikia,” alisema Lugola.

Alisema Serikali ya Tanzania haijaikataza Watanzania kufanya kazi nje ya nchi, bali imeweka taratibu zenye lengo za kumlinda Mtanzania na madhara yatokanayo na biashara hiyo haramu.

  Katibu wa Sekretarieti ya Taifa ya Kuzuia na Kupambana na Biashara hiyo Haramu kutoka Wizara hiyo, Separatus Fella, alisema zaidi ya washiriki 80 wamekwisha kufika katika mkutano wa mafunzo hayo  na matarajio yake makubwa washiriki watapata elimu nzuri kwa ajili ya kupambana na biashara hiyo haramu.

“Mafunzo haya yanatolewa kwa wadau wanaotekeleza sheria ya kuzuia na kupambana na biashara hiyo ambao ni  maofisa polisi, uhamiaji, waendesha mashtaka, mahakimu, maofisa ustawi jamii na mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali (NGO’s) yaliyopo Zanzibar,” alisema Lugola.

Fella alisema mafunzo hayo yanafanyika kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Shirika la Marekani linalojihusisha na Masuala ya Utafiti (RTI).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles