30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

Maimam watumika kusaidia kukabili vifo vya uzazi Zanzibar

VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM

SEPTEMBA mwaka jana, akiwasilisha taarifa ya Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo, katika kipindi cha 2017/2018 mbele ya Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Asha Ali Abdulla, alinukuliwa akisema:

“Elimu zaidi inahitajika kwenye kitengo cha huduma ya mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua na watoto wachanga.”

Anasema takwimu zinaonesha vifo 1,091 vya watoto wachanga na 49 vya uzazi vilitokea katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018.

Anataja sababu kuu ya vifo vya uzazi kuwa ni uelewa mdogo wa wajawazito kuhusu umuhimu wa kujifungulia hospitali na kuchelewa kufanya uamuzi.

Ukweli ni kwamba vifo vitokanavyo na uzazi nchini bado ni changamoto inayokabili jamii, zipo sababu mbalimbali zinazotajwa kuchangia vifo kikiwamo kifafa cha mimba ambacho husababishwa na shinikizo la damu.

Sababu nyingine ni kupasuka kwa fuko la uzazi kunakosababisha kupoteza damu nyingi na maambukizi kabla na baada ya kujifungua.

“Wizara ya Afya  inaendelea kusimamia  na kuratibu shughuli za huduma za wajawazito na watoto ili  kuhakikisha wanapata huduma bora, ambapo katika kipindi cha mwaka 2017/2018 jumla ya wajawazito 94.181 waliohudhuria kliniki angalau mara moja kabla ya kujifungua.

“Katika juhudi za wizara hiyo, kuimarisha huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga, vifo vyote vinavyotokea hufanyiwa uhakiki ili kujua sababu yake na kutafuta mbinu za kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika,” anasema.

Hali halisi

Ripoti ya Jamii na Afya (DHS) ya mwaka 2015 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu inasema asilimia 34 ya wajawazito Visiwani Zanzibar hujifungulia nyumbani, hali ambayo huwaweka katika hatari ya kifo hasa ikiwa mjamzito anakumbana na uzazi pingamizi.

“Ndiyo maana kupitia taasisi yetu isiyo ya kiserikali ya D-Tree International tuliona vema kushirikiana na Serikali, kupitia Wizara ya Afya Zanzibar kuelimisha jamii kuelewa umuhimu uliopo kwa mjamzito kuhudhuria kliniki na kujifungua hospitalini,” anasema Salum Mbarouk ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Uzazi Salama.

Anasema walikusudia kuhamasisha wakina mama hasa wajawazito kuhudhuria kliniki na kwenda kujifungua katika vituo vya afya na hospitalini ili kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Simu za kisasa

Mbarouk anasema ili kuwafikia kwa haraka waliamua kushirikiana na Serikali ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya, kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya 401 ambapo waliwapatia simu za kisasa za mkononi ili kuwaongoza katika kazi zao.

“Simu hizi janja (smartphones) zimewekwa ‘application’ maalumu ambayo inamwezesha mhudumu  kumsajili mjamzito kwenye mradi huu,” anasema.

Anaongeza: “Kupitia simu, muhudumu anawasiliana na mjamzito kwa ukaribu na kumfuatilia hali yake kujua iwapo ana dalili za hatari ama la! akampatia ushauri nasaha kuhusu malaria, Ukimwi, chakula bora na mambo mengine.

“Kupitia njia hiyo, anamhamasisha pia kwenda kituo cha afya na hasa ikiwa atagundua ana dalili zozote za hatari, pia humuunganisha mama na usafiri ili wakati wa kujifungua unapofika asihangaike kupata usafiri.

“Baada ya kujifungua, mhudumu huendelea kumtembelea mama kwa awamu tatu kuangalia maendeleo yake na mtoto kwa ujumla,” anasema.

Umbali wa vituo

Anasema ni muhimu kujua mapema umbali uliopo kutoka eneo anakoishi mjamzito hadi katika kituo cha huduma za afya ama hospitali.

“Kuna vituo vya afya aina tatu, kuna kituo kidogo cha afya ambako mjamzito anaweza kupata huduma hadi ya kliniki lakini hawezi kujifungua katika kituo hicho.

“Kuna kituo cha afya cha kati ambacho kimepewa ruhusa na kimewezeshwa kuwasaidia wajawazito kujifungua, lakini hakiwezi kuzalisha kila mimba.

“Yaani kwa mfano kama mimba ni ya kwanza kwa mujibu wa Wizara ya Afya Zanzibar, mjamzito hawezi kuzalishwa hapo kwa kuwa si rahisi kujua atapata shida gani zinazoweza kuhatarisha uhai wake na wa mtoto.

“Lakini pia mtu mwenye historia ya kusumbuliwa na mimba, hawezi kujifungua kwenye kituo cha kati.

“Kuna zile hospitali za rufaa ambazo mjamzito huhamishiwa kujifungua huko, sasa unaweza kukuta umbali ni mrefu hivyo, muhudumu wa afya hutumia mfumo wake wa simu (mobile application) kumsaidia kujua alipo hadi kituoni ni umbali kiasi gani,” anasema.

Anaongeza: “Muhudumu huwasiliana  na madereva kabla ya kuongea na mama ili kujua bei  na kumpatia taarifa za umbali wa kituo na gharama za usafiri, namba za simu za madereva ili siku inapowadia apate msaada wa usafiri haraka.

Ushiriki wa wanaume

Anasema ni muhimu wanaume kuwa bega kwa began a wenzi wao katika kufanikisha safari ya uzazi.

Anasema wakati mradi huo ulipoanzishwa visiwani humo, walibaini kuna ushiriki mdogo wa wanaume kwenye masuala ya afya ya mama na mtoto hasa uzazi.

“Baada ya kuona hali hiyo, tukafikiria jinsi gani tutaweza kulifikia kundi hili kuwaelimisha ili nao washiriki moja kwa moja,” anasema.

Anasema waliwapa kazi hiyo ya ufuatiliaji wahudumu wa afya lakini wanapofika majumbani huwakuta wanawake pekee, wanaume huwa tayari wapo kwenye majukumu ya kikazi, juhudi nyingi za kuwashirikisha wanaume zilifanyika kila wilaya na zilianza kuzaa matunda.

“Kwa kuzingatia mila, tamaduni na desturi za Kizanzibar, wanawake wengi hawawezi kufanya uamuzi wowote bila ridhaa ya waume zao, chochote anachofanya na popote anapokwenda lazima aombe ruhusa kwa mumewe.

“Tukaona bila kumpata mwanamume kumwelimisha na kumhamasisha, itakuwa jambo gumu mjamzito kupata msaada wa mume au kusindikizwa kwenda hospitalini kujifungua au kliniki,” anasema na kuongeza:

“Tukasema ni lazima tuwapate wanaume, tukatafakari sehemu ya kwanza kuwapata ni kwenye mikusanyiko yao ya kawaida na sehemu za ibada.

“Kwa sababu pia tuligundua kulingana na ripoti mbalimbali zilizofanywa visiwani hapa, asilimia 99 ya Wazanzibar ni Waislamu.

“Maana yake ni kwamba tukitumia sehemu hiyo tutakuwa tumepata kundi kubwa la wanaume kwa kipindi kifupi, tukaamua kuwatafuta viongozi wa dini ya Kiislamu ambao kimsingi ndiyo ambao muda mwingi huwakusanya wanaume na kuzungumza nao.”

Anaendelea kusema: “Kimsingi kwenye kanuni za Kiislamu, kuna sheria kwamba Imamu yeyote hawezi kuongoza ibada ikiwa idadi ya waumini haijafika 40.

“Pemba ina wilaya nne, tukafikiria kufanya majaribio huko, tukachagua Maimamu 10 katika kila wilaya, tukapata jumla ya 40 ambao tulizidisha na waumini 40 maana yake katika kipindi kifupi tulitarajia kupata wanaume 1,600 na kuendelea.

“Tuliwaita na kuzungumza nao, tukawapa elimu na kuwaeleza kwa kina umuhimu wa ushiriki wa wanaume katika kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa salama.

“Kwa kushirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar na Taasisi ya Kiislamu (UKUEM) tuliandaa hotuba maalumu ambayo walikwenda kuwasilisha katika misikiti yao.”

Ujumbe ulifika?

Anasema walifuatilia kwa karibu iwapo ujumbe huo ulifika ama la, kwa kuhudhuria katika misikiti, kuwasiliana mara kwa mara na Maimamu hao na kuhojiana na wanaume wenyewe.

“Kila ijumaa tulikwenda, ujumbe ulifika na tulipohoji wanaume walitueleza ni ujumbe muhimu ambao walichelewa kuupata na kwamba wanatamani iwe elimu endelevu,” anasema.

Mtazamo hasi

“Wanaume tuliowahoji walitueleza sababu mbalimbali zilizowafanya wawazuie wake zao kwenda kujifungulia vituo vya afya, wapo ambao walidai wanadhalilishwa na watoa huduma.

“Wengine kutokana na imani yao, waliamini kwamba kumpeleka huko mke ikiwa mtoa huduma ni mwanamume inakuwa ni aibu na kashfa kwao, huku wengine wakidai ni kutokana na umbali uliopo kutoka nyumbani hadi katika vituo vya afya,” anabainisha.

Maandalizi

Mbarouk anasema tangu mradi huo ulipoanza ingawa mjamzito huunganishwa na usafiri, hulazimika kuilipia mwenyewe ili kufika kituoni kujifungua.

“Tulifanya hivyo kwa sababu tulitaka wanajamii watambue kwamba hili ni jukumu lao, hata mradi huu utakapofikia tamati, watu waendelee kuhudhuria kliniki na kwenda kujifungua vituoni,” anasema.

Anaongeza: “Tunatamani watu wanavyochangishana michango ya harusi ifike mahala waone jukumu la mjamzito kujifungua salama ni la kwao, wajiandae mapema kumpokea mtoto mtarajiwa.”

Anasema kutokana na mrejesho huo, wanaona mradi huo umekuwa msaada kwa jamii na unaweza pia kufundishwa katika maeneo mengine ikiwamo kanisani ambako wanaume hushiriki ibada.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles