27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 8, 2021

Mkutano wa Trump, Kim watikisa dunia

HANOI, VIETNAM

RAIS wa Marekani, Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un walikutana mjini hapa jana, ikiwa ni mara ya pili baada ya kukutana katika tukio la kihistoria nchini Singapore, Juni mwaka jana.

Wawili hao walikutana mbele ya bendera sita za kila taifa, wakishikana mikono na kubadilishana tabasamu wakati walipoungana kwa chakula cha usiku katika hoteli ya kihistoria ya Hanoi, ambako Trump alitamka kuwa uhusiano wao ni mzuri.

“Uhusiano wetu ni maalumu mno,” alisema Trump katika moja ya kauli alizotoa kuhusu wao.

“Ni heshima kuwa na Mwenyekiti Kim. Ni heshima kuwa pamoja naye,” alisema Trump, ambaye mara kwa mara alimsifu kiongozi mwenzake huyo.

Kwa upande wake, Kim aliusifu uamuzi wa kishupavu wa Trump kufungua milango ya majadiliano, ambayo Trump alionekana kuzungumza zaidi huku akiiahidi Korea Kaskazini mambo mazuri.

Trump, Kim wala chakula pamoja

Trump na Kim walionekana kuchangamka na kuwa na mwonekano wa kirafiki wakati walipoanza kukutana kwa chakula cha usiku.

“Hakuna kitu kama kuwa na chakula kizuri cha faragha cha usiku,” alitania Trump huku akiamuru kupunguzwa kwa idadi ya waandishi waliokuwa wakichukua picha ndani ya chumba.

Wakiwa wamekaa katika meza mviringo na Waziri wa Mambo ya Nje ya Marekani, Mike Pompeo na Kaimu Mnadhimu Mkuu, Mick Mulvaney, Trump aliwataka wapigapicha kuhakikisha yeye na Kim ‘wanatokeleza’ katika picha zao.

“Tunatarajia kuwa na kazi nyingi kesho,” Trump alisema na kuongeza baadaye kuwa uhusiano wao ni maalumu sana.

Ikulu ya Marekani – White House ilisema uamuzi wa kuhusisha waandishi wachache wakati wa chakula cha usiku ulitokana na unyeti wa mikutano hiyo.

Katibu wa Habari wa Ikulu, Sarah Sanders alisema; “Kutokana na unyeti wa mikutano, tuna nafasi chache kwa kundi dogo, lakini tutahakikisha uwakilishi wa wapigapicha, TV, redio na magazeti katika vyumba vyote.

“Tunaendelea na majadiliano, lakini daima tutahakikisha vyombo vya habari vya Marekani vinapata nafasi kadiri iwezekanavyo.”

Mwandishi mmoja, Vivian Salana alikosoa uamuzi wa White House akisema; “Awali Sarah Sanders alitufahamisha hakuna mwandishi wa gazeti atakayeruhusiwa kutokana na unyeti uliopo. Lakini wakati waandishi wenzetu walipoungana nasi kupinga, wakaamua kumruhusu mwandishi mmoja wa gazeti.”

Kim amsifu Trump kwa uamuzi wa kishujaa

Kim alisema mkutano wake wa pili na Trump unatokana na uamuzi wa kishupavu wa kisiasa wa rais huyo wa Marekani.

Akiwaambia waandishi wa habari akiwa kando ya Trump jana, Kim alisema kumekuwa na fikra nyingi, juhudi na uvumilivu baina ya sasa na tangu wakutane Juni mwaka jana nchini Singapore.

Kim alisema ‘dunia ya nje’ imeshindwa kuuelewa vyema uhusiano wa Marekani na Korea Kaskazini katika kipindi cha baada ya mkutano ule wa Singapore.

 Alisema ana matarajio mkutano wa Hanoi utazaa matunda kwa kila mtu.

Kim alisema wawili hao walikuwa na mazungumzo mazuri ya dakika 30 walipokutana kwa chakula cha usiku jana.

Trump aahidi kumsaidia Kim

Akirejea mpango wa Marekani wa kutumia vishawishi vya kiuchumi, ambavyo anaamini vitamshawishi Kim kuachana na silaha za nyuklia, ambazo taifa lake limekuwa likizitengeneza kwa miaka mingi, Trump aliiahidi Korea Kaskaini kuisaidia ifikie katika ustawi mkubwa.

 “Nadhani nchi yako ina uwezekano mkubwa wa kupaa kiuchumi.

“Nadhani una wakati ujao mzuri kwa nchi yako, wewe ni kiongozi mkubwa. Nasi tuko nanyi tutasaidia hilo litokee,” alisema Trump kumwambia Kim.

Kim naye alisema anashukuru kuwa wameweza kuvishinda vikwazo vyote na kukutana tena.

Akijibu hilo, Trump alisema; “Hii ni heshima ya kuwa na Mwenyekiti Kim, ni heshima hakika kuwa pamoja Vietnam.

“Inafurahisha kuwa nawe, hakika tulikuwa na mkutano wenye mafanikio nchini Singapore Juni mwaka jana.

“Baadhi ya watu wanataka kuona unaenda haraka, nimeridhika, nawe umeridhika. Tuna furaha sana namna tunavyofanya.”

Wakati waandishi wa habari walipokuwa wakipaza sauti kuuliza maswali yaliyoelekezwa zaidi kwa Trump, si Kim wala mwenzake waliowajibika kuitikia.

Mwandishi mmoja alikuwa akiuliza kuhusu ufichuzi wa hivi karibuni wa mwanasheria wa zamani wa Rais Trump, Michael Cohen.

Trump alianza kuwasili

Trump alianza kuwasili eneo la mkutano, Hoteli ya Metropole, ambako alikuwa akipungiwa mikono na watu waliojipanga mitaani pamoja na kupiga picha kwa simu zao tangu akitokea hoteli aliyofikia ya J.W Marriott mjini Hanoi.

Njia aliyopitia kuna ubalozi wa Korea Kaskazini.

Msafara wa Kim pia ulikuwa njiani kuelekea hotelini hapo akitokea Melia Hotel.

Walivyowasili Vietnam

Trump aliwasili juzi mjini Hanoi akiwa na ndege ya Air Force One. Na akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter; “Nimewasili Vietnam. Ahsanteni sana watu wote kwa makaribisho mjini Hanoi. Umati wa ajabu na upendo mkubwa.”

Kim aliwasili kwa kutumia treni mapema juzi, baada ya safari ya siku tatu ambayo ilikuwa ya umbali wa kilomita 3,000 kutoka mji mkuu wa Korea Kaskazini – Pyongyang kupitia China. Kwa kufanya hivyo amefuata nyayo za baba na babu yake waliopendelea kutumia usafiri huo.

Hata hivyo Kim anafahamika kupendelea ndege zaidi, uamuzi wa kutumia treni umetokana na sababu za kiusalama zaidi kwa sehemu kubwa ikipitia taifa mshirika la China.

Alitumia sehemu ya mwisho ya safari yake kutoka mpaka wa Vietnam na China hadi Hanoi kwa kutumia gari.

Walinzi wake waliwasili kwa ndege ya mizigo

Walinzi wa kiongozi huyo waliwasili Hanoi mapema Jumapili asubuhi wakiwa wamepanda ndege ya mizigo ya Korea Kaskazini, Air Koryo Ilyushin-76.

Makumi ya wanaume warefu waliovalia suti nyeusi, mashati maupe na tai walionekana wakishuka kutoka katika ndege hiyo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Noi Bai wakishusha pia maboksi makubwa.

Hata hivyo, haikuweza kujulikana mara moja iwapo gari aina ya Limopusine la Kim liliwasili Hanoi pia siku hiyo, baada ya juhudi za wanahabari kulitafuta kushindikana.

Hata hivyo siku moja kabla ya Kim kuwasili, gari hilo lilionekana mitaani likiwa limezungukwa na walinzi.

Ndege hiyo chapa P-914 iliyotengenezwa mwaka 1990 ni ile ambayo ilibeba Limousine la Kim na walinzi nchini Singapore wakati wa mkutano wa kwanza na Trump.

WALINZI WAKE WAWA KIVUTIO

Kama kawaida, walinzi 12 wa Kim walionekana kila alikokwenda na daima walikuwa kivutio kwa walioshuhudia na vyombo vya habari.

Kuwa mmoja wa walinzi hawa wakakamavu wa Kim wanaokimbia kimbia kulikinga gari kunahitaji zoezi zito la mchakato wa uteuzi kukiwa na mchujo mkali.

Hutumika kama ngao ya kiongozi huyo na huchaguliwa kwa ukakamavu wao, urefu, macho makali, shabaha, sanaa ya mapigano na hata haiba nzuri.

Wote ni askari kutoka Jeshi la Watu wa Korea (KPA) na huchaguliwa na wakala wa Serikali ajulikanaye kama Central Party Office Number Six.

SABABU ZA KUFANYIA MKUTANO VIETNAM                                    

Eneo la mkutano wa kwanza wa Donald Trump-Kim- Singapore ilichaguliwa kwa sababu ni moja ya nchi chache zenye uhusiano wa kidiplomasia na Marekani na Korea Kaskazini pia.

Hivyo, kwanini Vietnam imekuwa chaguo la mkutano huu, ilihali kuna mataifa mengine yenye sifa kama za Singapore au Vietnam?

Korea Kaskazini na Vietnam zina vitu vichache vinavyozifananisha.

Yote ni moja ya mataifa machache yaliyobakia yakiendekeza utawala wa kikomunisti.

Cuba ingeweza kuchaguliwa lakini ipo ubavuni mno na Marekani kuweza kukubalika na utawala wa Kim.

Vietnam huisaidia Korea Kaskazini kwa mafunzo na teknolojia katika maeneo kama vile uzalishaji na kilimo.

Pia zote zimewahi kupigana vita kali na Marekani, lakini zilikuja kwenda njia tofauti baadaye.

Kaskazini ilibakia kutengwa na dunia nzima kutokana na kuongozwa na familia moja inayotumia mkono wa chuma dhidi ya watu wake wanaoishi katika umasikini mkubwa.

Lakini Vietnam ilibadilika kwa kuwa na mwelekeo mzuri katika uhusiano wa kimataifa ikiwamo na Marekani na inashuhudia na ustawi.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,573FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles