BRUMADINHO, BRAZIL
TAKRIBANI watu 200 hawajulikani waliko baada ya bwawa la maji kuvunja kingo zake katika mgodi wa kampuni ya chuma kusini mashariki mwa nchi ya Brazil.
Katika tukio hilo inadaiwa takribani watu tisa wamefariki dunia huku uongozi ukisema huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka kwa kuwa karibu watu 200 bado hawajulikani walipo.
Maporomoko hayo yamewazika watu wengine waliokuwa katika kantini wakila chakula kwa kuwa ulikuwa muda ya mchana.
Inaelezwa kuwa mgodi huo unamilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya Vale inayomilikiwa na serikali ya Brazil.
Miaka mitatu iliyopita watu kumi na tisa walifariki kutokana na maporomoko mengine yaliyotokea kwenye mgodi unaomilikiwa na kampuni hiyo. Hadi leo eneo hilo bado linakabiliana na changamoto za kimazingira zilizotokana na maporomoko hayo.
Taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini Brazil vimesema kuwa maji yaliyochanganyika na matope yaliwafunika mamia ya wafanyakazi wa shirika hilo na watu wengine.
Shughuli ya kuwatafuta manusura inaendelea karibu na mji wa Brumadinho, katika jimbo la Minas Gerais.
Gavana wa jimbo hilo, Romeu Zema amesema kuna hofu huenda watu wengi wamefariki katika tukio hilo.
Baadhi ya watu waliokwama kwenye matope, waliokolewa kwa kutumia helikopta baada ya barabara kuharibiwa.
Watu wengine wamehamishwa kutoka makazi yao kutokana na sababu za kiusalama.
Kwa mujibu wa Afisa mkuu mtendaji wa kampuni ya Vale, Fabio Schvartsman amesema theluthi moja ya wafanyikazi karibu 300 hawajulikani waliko.