24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Huku ndiyo kutunguliwa kwa siasa za vyama vingi

MWANDISHI WETU

MUSWADA wa Mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Siasa nchini umepitishwa na Bunge na sasa unangojea saini ya Rais Dk. John Magufuli ili kuwa sheria.

Licha ya malalamiko kadhaa kutolewa na wanasiasa wa kambi ya upinzani ndani na nje ya Bunge, hata hivyo hawakufanikiwa kufanya marekebisho waliyokuwa wakiyalalamikia.

Nje ya Bunge tumeshuhudia asasi mbalimbali za kiraia zikionyesha upungufu na hatari ya baadhi ya vifungu vya muswada huo.

Duru za kisiasa zinaonyesha kuwa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi-CCM, ambao ni wengi bungeni wameutetea muswada huo kwa kudai utasafisha siasa za vyama vingi nchini.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama amesema muswada huo kiboko.

Hoja za wanaokosoa wanadai kuwa muswada huo haukilengi chama tawala bali ni vyama vya upinzani na ndiyo maana wabunge wa CCM wameushadadia sana.

Inaelezwa kuwa muswada huo unakwenda kutungua siasa za vyama vingi pamoja na kuibua changamoto kwa vyombo vya ulinzi na usalama wa raia nchini.

Kutunguliwa vyama:

Je, ni namna gani vyama vya siasa vimetunguliwa na muswada huu? Tunaangalia vifungu mbalimbali vinavyosababisha wasiwasi na kuonyesha ushahidi kuwa vyama vya siasa vimetunguliwa kwa kiasi kikubwa.

Mosi, kifungu cha 19 kinasema msajili wa vyama vya siasa anaweza kusimamisha usajili wa chama chochote cha siasa kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaoamua kuweka kwa malengo ya kutaka chama husika kijirekebishe.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa chama chochote ambacho kitakumbana na adhabu kutoka kwa Msajili wa vyama hakitaruhusiwa kufanya shughuli za kisiasa.

Katika kifungu hiki pia msajili anapewa mamlaka ya kukifutia usajili chama chochote ambacho atakipatia adhabu kulingana na kanuni zitakazowekwa.

Kifungu hicho kinalalamikiwa kuwa kitasababisha vyama vingi kushindwa kushiriki uchaguzi kwa kuwa adhabu inaweza kutokea muda mfupi kuelekea kwenye zoezi hilo.

Pili, kifungu cha 5A kinataka msajili kupewa taarifa kimaandishi na taasisi yoyote ya ndani ama ya nje ya Tanzania itakapotaka kutoa mafunzo ya elimu ya uraia pamoja na kuwajengea uwezo kwa chama cha siasa wanaagizwa kuwataja wawezeshe malengo na nyenzo zitakazotumika katika mafunzo hayo. Kinyume cha hapo adhabu ni shilingi milioni thelathini au kifungo cha miezi 6 jela.

Aidha, katika kifungu hicho kinampa mamlaka msajili wa vyama vya siasa kutoa kibali ama kukataa kufanyika kwa mafunzo hayo na endapo taasisi inayowezesha mafunzo hayo haina kibali.

Tatu, Kifungu cha 5B kinampa nguvu msajili wa vyama vya siasa nchini kuomba na kupewa taarifa yoyote ile ya chama chochote cha siasa na kwa wakati wowote.

Kifungu hicho kinaeleza kuwa endapo kiongozi yeyote wa chama cha siasa atashindwa kutekeleza matakwa ya msajili, tendo hilo litakuwa ni kosa ambalo faini yake ni shilingi milioni moja au kifungo kisichopungua miezi sita gerezani na kisichozidi miezi 12.

Mara baada ya kutolewa adhabu hiyo kwa mhusika au chama husika kitatakiwa kutoa taarifa zilizohitajika. Kama chama au kiongozi yeyote ataendelea kutotoa taarifa inayohitajika basi chama hicho kinasimamishwa ama kufutiwa usajili kabisa.

Nne, Kifungu cha 6 kinabainisha ulinzi wa msajili wa vyama vya siasa pamoja na wafanyakazi wa ofisi yake dhidi ya kufunguliwa kesi yoyote mahakamani.

Kifungu hiki kinatanabaisha kuwa “Shauri lolote halitafunguliwa dhidi ya Msajili, Naibu Msajili, Mkurugenzi ama maofisa wengine chini ya Msajili kwa lolote watakalolifanya ama kutolifanya kwa nia njema chini ya sheria hii.”

Tano, kifungu cha 11C kinaruhusu vyama vya siasa kuunda ushirikiano na kufikia malengo ya pamoja ya kisiasa lakini kanuni za kuunda ushirikiano zitatungwa na waziri. Kifungu kinasomeka “Waziri atatunga kanuni zitakazoweka masharti na utaratibu wa namna ya kuunda ushirikiano huo.”

Sita, kifungu cha 19A kinasema msajili anaweza kukisimamisha usajili wa chama kwa sababu atakazozitaja na kwa muda atakaoweka ili chama hicho kiweze kujirekebisha. Chama ambacho kimesimamishiwa usajili hakitaweza kufanya shughuli zote za kisiasa. Na iwapo msajili ataona chama hicho hakijajirekebisha anaweza kukifutia usajili.

Saba, kifungu 21E kinampa msajili nguvu ya kumsimamisha mwanachama yeyote wa chama chochote cha siasa ambaye atavunja kifungu chochote cha sheria hiyo.

Kifungu hiki kinafafanua kuwa waziri mwenye dhamana ya vyama vya siasa atawajibika kutunga kanuni za namna gani wanachama wa vyama vya siasa wanaweza kusimamishwa.

Nane, kifungu cha 22 kinaelezea suala la mapato ya vyama vya siasa. Kinaeleza kuwa ni marufuku kwa vyama vya siasa kupokea fedha kutoka taasisi au mtu yeyote nje ya nchi. Hii ina maanisha kuwa marafiki, wafuasi na washirika wao waliopo nje ya nchi hawataruhusiwa kuchangia fedha za shughuli yoyote kwa chama cha siasa nchini.

Kwa mfano, vyama vya siasa hushirikiana katika nchi mbalimbali, kama vile Ujerumani na Uingereza ambako watu binafsi au taasisi fulani zinawachangia wanasiasa na vyama vyao kama marafiki au sehemu ya mchango wao katika shughuli wanayofanya. Muswada huu unakataza hayo yote.

Tisa, kifungu cha 24 kinatoa mamlaka kwa msajili kuzuia ruzuku ya chama cha siasa kwa muda atakaoweka wazi au usiowekwa wazi iwapo matumizi ya fedha hizo yatakuwa yenye kutia shaka. Katika kifungu hicho ndipo kuna adhabu kwa chama kitakachokuwa na hati chafu, ambapo hakitapewa ruzuku kwa miezi 6.

Aidha, msajili wa vyama vya siasa anapewa mamlaka ya kumwagiza Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu (CAG) kufanya ukaguzi maalumu kwenye chama cha siasa endapo kutakuwa na shaka kwenye matumizi ya rasilimali za chama.

Kumi, kifungu kidogo cha 8(E)(2) kimeainisha kuwa, chama cha siasa hakitatoa fedha za kuratibu vikundi vya ulinzi ndani ya chama au kuratibu mafunzo ya kijeshi au matumizi ya silaha na kadhalika. Hilo linafuta moja kwa moja vikundi vya ulinzi kama Green Guard (CCM), Redbrigade (Chadema)  na Blue Guard (CUF).

Kumi na moja, kifungu kidogo cha 8(E) (3) kinasema chama cha siasa kitakachokiuka kifungu hiki kitafutiwa usajili na viongozi waliojihusisha na kosa hilo wanaweza kufungwa kifungo kisichopungua miaka 5 au kisichozidi miaka 20 au vyote kwa pamoja.

Kwa mujibu wa ibara ya 147 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeeleza bayana kuwa ni marufuku mtu yeyote au chama cha siasa au kikundi chochote hawataruhusiwa kuanzisha kikundi cha kijeshi, mgambo au kikundi cha ulinzi isipokuwa Serikali pekee.

Kupitishwa kwa muswada huo na utakapokuwa sheria baada ya kusainiwa na Rais kunalipatia changamoto jeshi la polisi katika kuratibu ulinzi wa viongozi. Inakubaliwa kuwa vikundi vya ulinzi havihitajiki kwenye vyama, lakini changamoto kubwa itakuwa wakati wa uchaguzi kutokana na uchache wa askari wakati wa kuhudumia maeneo yote nchini.

Katika kile kilichoelezwa kuwa muswada huo hauna lengo jema kwa vyama vya upinzani na kuwa ni ukiukaji wa haki za kikatiba za shughuli za siasa, baadhi ya wanasiasa walilazimika kukimbilia mahakamani.

Hata hivyo Mahakama ilitupilia mbali kesi hiyo ambayo iliyofunguliwa na vyama 10 vya upinzani kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa Mwaka 2018, ilieleza kuwa muswada huo unajaribu kuzifanya shughuli za kisiasa kama vile ni makosa ya jinai.

Wanasiasa wamedai kuwa muswada huo unampa mamlaka makubwa msajili wa vyama vya siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo ikiwemo uchaguzi wa viongozi na kusimamisha uanachama kwa wanachama wa vyama hivyo.

Hoja yao kubwa kwenye kesi hiyo ilikuwa kupinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kuzuia muswada huo usijadiliwe bungeni. Hata hivyo hawakufua dafu.

Katika kesi hiyo Jaji Benhajj Masoud, katika uamuzi wake alikubaliana na upande wa Serikali kuwa walalamikaji hawakupaswa kuomba Mahakama itamke kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Haki za Msingi na Wajibu kinakiuka Katiba na kuomba mahakama itamke kuwa muswada huo unakiuka Katiba.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamedai kuwa kuna ukakasi mkubwa katika baadhi ya vifungu hasa nguvu kubwa alizopewa msajili.

Wamesema watakaoanza kuathirika pindi muswada huo utakapokuwa sheria na kuanza kutekelezwa ni vyama vyote vya upinzani hasa pale msajili atakapotumia mamlaka yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles