JOSEPH HIZA NA MITANDAO
CLAUDIA Wanjiru ni mwanamtindo mwenye makovu usoni, ambayo aliyapata baada ya kunusurika mkasa wa moto akiwa mwanafunzi wadarasa la saba.
Kabla ya mkasa huo, Claudia, ambaye kwa sasa ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) nchini Kenya alikuwa na ndoto ya kuwa mwanamitindo.
Lakini licha ya makovu usoni, amehakikisha ndoto hiyo anaitimiza.
Akizungumza namna alivyopatwa na makovu hayo,anasema “tulipokuwa kwenye hoteli tukiwekewa chakula, jiko la gesi lililipuka na mafuta yakanimwagikia usoni. Nilianza kukimbia nikitafuta maji”.
Alichukuliwa kisha akapelekwa hospitalini. Alikuwa ameungua kwa asilimia 14 usoni. Alikaa hospitalini kwa muda wa miezi mitatu.
Hali hii ilifanya maisha yake kubadilika, hata kukosa marafiki.
“Baada ya kuungua, watoto ambao walikuwa wadogo kwangu kiumri, walikuwa wananiogopa, na wale wa rika langu, walikuwa wananicheka na kunitania.
Nikiwa shuleni, nilikuwa napata barua za matusi na mwalimu alipokuwa akitupatia zoezi la kufanya kwa makundi, hakuna mtu aliyekuwa akikubali kuwa naye kundi moja,” anasema.
Hali hii ilipelekea Claudia kukumbwa na msongo wa mawazo kutokana na namna watu walivyomtendea na kumsema.
“Watu walisema nilijaribu kubadilisha rangiya ngozi yangu lakini dawa zikagoma; Wengine walidai eti nina Ukimwi. Nilikuwa najipendekeza kwa watu ili nipate marafiki, lakini mtu aliyekuwa anakubali kuwarafiki yangu alikuwa na lengo fiche.”
“Kutokana na kukosa marafiki, nilijaribu kujitoa uhai kwa kuweka jiko katika chumba changu na kufunga mlango na madirisha, lakini sikufa, nikajua Mungu ameniokoa.”
“Nilijua kwamba Mungu amenipatia nafasi nyingine na kuwa ananipenda si lazima nipendwe na mtu kwa kuwa yeye ndiye aliyenipatia maisha haya, ni yeye ndiye aliniweka duniani.”
Aliponusurika baada ya kujaribu kujitoa uhai, akaamua kujikubali na kujitahidi kufikia ndoto yake ya kuwa mwanamitindo.
“Nikaanza uanamitindo, ili niwasaidie wasichana wengine ambao pengine wanazuiwa kushiriki kwa sababu ni wanene ama niwafupi. Lengo, wasome historia yangu ili wajue kuna matumaini.”
Amejaribu kwenda katika mashindano ya uanamitindo lakini kila wakati mawakala humbagua.
“Kuna wakati nilienda kujisajili katika mashindano ya uanamitindo lakini wakala akanizuia mlangoni na kuniambia niwanamitindo pekee walioruhusiwa kuingia,” anasema.
Lakini alijua kukataliwa kwake ni kwasababu ya makovu yake.
Licha ya kukataliwa na mawakala, Claudia ambaye pia anajitambulisha kama ‘Vanilla Afrika’ kama jina lake la kisanii, hakukata tama.
Kwa msaada wa wanafunzi wenzake, hupigwa picha katika mazingira tofauti na kuziweka katika mtandao wa Instagram.
Makovu pia yamemkosesha mchumba. “Mvulana ambaye nilikuwa namchumbia, kila wakati tukikosana, ananikumbusha juu ya alamazangu usoni.
Huniambia anavumilia kuwa na mimi kwa sababu hakuna mtu mwingine anayeweza kunipenda na alama hizo.”
Hata hivyo, msichana huyu anaulezea urembo kulingana na anavyotambua.
“Urembo ni tabia, ni kumsaidia mtu, kumheshimu mtu, urembo ni utu… Hii ndiyo maana ya urembo, kwasababu mtu anaweza kuwa na sura ya kupendeza, lakini hana tabia za kupendeza.
“Kama mimi mwenyewe niko na hizi alama, najiambia kwamba mimi ni mrembo, kwasababu si alama zinanipatia jina, alama ni ngozi tu, kila mtu anayo.”