ZAINAB IDDY-DAR ES SALAAM
WAKATI Wanayanga wakimtwisha zigo la lawama kocha wao, Mwinyi Zahera, baada ya kupokea kipigo, nahodha wa timu hiyo, Ibrahim Ajib, amesema sababu kubwa ni uwanja walioutumia na si kocha.
Yanga juzi ilijikuta ikipoteza alama tatu mbele ya Lipuli FC, baada ya kufungwa bao 1-0, mechi iliyochezwa Uwanja wa Samora Iringa huku Zahera akiwa jijini Dar es Salaam na timu ikiwa chini ya Noel Mwandila.
Matokeo hayo yaliifanya Yanga kusalia kwenye nafasi ya kwanza ikiwa na alama zake 67, huku Lipuli wakifikisha alama 44 kwenye nafasi ya nne.
Akizungumza na MTANZANIA, Ajib alisema wachezaji walitumia nguvu na akili nyingi ili wapate ushindi lakini walijikuta wanatoka patupu.
“Mechi za mikono zina changamoto nyingi hususani katika suala la viwanja, lakini pia mpira una matokeo matatu na tulioyapata ni sehemu mojawapo.
“Sijaona sababu ya kumlaumu kocha kwa ajili ya haya matokeo tulioyapata, kwani si mara ya kwanzo yeye hayupo kwenye timu na sisi tunapata ushindi.
Ajibu aliongeza: “Hili limeshatokea tuangalie mechi inayokuja vipi tutajipanga kuhakikisha haturudii makosa hata kama uwanja utakuwa si rafiki tena kwetu.”