Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amewataka wenyeviti wa Serikali za mitaa kusimamia vema fedha zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kwenye majimbo mbalimbali nchini ili kutomwangusha kwani ndiye mgombea wa urais mwaka 2025 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Septemba 15, mwaka jana wakati akizungumza na wanawake katika Siku ya Demokrasia Duniani Rais Samia alisema atagombea urais mwaka 2025.
Akizungumza wakati wa hafla ya kumpongeza iliyoandaliwa na Wenyeviti wa Serikali za Mitaa Jimbo la Ilala, Zungu amesema wananchi wana imani kubwa na CCM hivyo ni wajibu wa viongozi hao kukidhi matarajio yao kwa kufanya kazi kwa bidii.
“Tuna kazi kubwa ya kusimamia fedha alizoleta mheshimiwa rais kwenye majimbo yetu, mama Samia ndiye mgombea wetu wa urais 2025 hakuna mgombea mwingine hivyo, umoja wetu ndiyo utatufanya tushinde kwa zaidi ya asilimia 98…tukapambane kusimamia miradi mikubwa,” amesema Zungu.
Aidha amesema ataendelea kushirikiana na wenyeviti hao katika kutekeleza majukumu yao kwani mafanikio ya Serikali yanategemea pia ufanisi wao.
Akizungumzia uchaguzi wa ndani ya chama unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu Zungu amewasihi wana – CCM kuendeleza umoja na kuepuka kugombana.
“Tunaingia kwenye uchaguzi wa chama tuendeleze umoja, hakuna haja ya kugombana kwenye uchaguzi ukipata shukuru na usipopata pia shukuru kwa sababu hiyo ni kazi ya Mwenyezi Mungu,” amesema.
Pia amewahimiza wenyeviti hao kuwahamasisha wananchi kujitokeza kuhesabiwa wakati wa zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti ili kuiwezesha Serikali kuweza kupanga huduma za kijamii.
Naye Diwani wa Kata ya Upanga Mashariki ambaye alizungumza kwa niaba ya madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sultan Ahmed Salim, amesema Zungu anastahili kupata nafasi hiyo kutokana na uzoefu mkubwa alionao na namna anavyojituma kufanya kazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ilala, Ubaya Chuma, amesema Zungu ana uzoefu mkubwa kuanzia ndani ya chama kutokana na nyadhifa mbalimbali alizoshika kuanzia jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM) hadi Wazazi hivyo wana imani haendi kujifunza.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Karume, Haji Bechina, amesema kuchaguliwa kwa Zungu ni kielelezo cha imani kubwa waliyonayo wabunge.
Februari 11 mwaka huu Zungu alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge akichukua nafasi ya Dk. Tulia Ackson ambaye alichaguliwa kuwa Spika.