WIZARA ya Maliasili na Utalii ndiyo yenye jukumu la kusimamia na kutunza maliasili zote ambazo Taifa hili limejaaliwa kuwa nazo.
Wizara hiyo imebeba jukumu kubwa ambalo kwa namna moja au nyingine, linasaidia kuchangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kila mwaka.
Kwa mfano mwaka jana, tumeona sekta ya utalii ikichangia zaidi ya Sh bilioni 27Â katika pato la Taifa.
Hili si jambo dogo ni jambo la kujivunia na kuona fahari kuwa rasilimali tulizopewa na Mungu zinaleta matunda.
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na wizara hii, ndiyo maana kumekuwapo na mafanikio makubwa karibu maeneo mengi, yakiwamo ya wanyama, misitu na mengine mengi.
Leo tumelazimika kuandika haya baada ya kuwapo na malalamiko mengi kutoka kwa wakazi wa Wilaya ya Muheza mkoani Tanga, ambao wanalalamikia wizara hii kusitisha biashara ya vipepeo kwa miaka 14 sasa.
Pia kumekuwapo na malalamiko mengi tangu mwaka 2003, baada ya Serikali kutangaza rasmi kusitisha biashara ya kusafirisha vipepeo nje ya nchi, kutokana na sababu kadha wa kadha ambazo leo ni miaka 14 sasa, huku wananchi ambao ni wafugaji wakibaki wameduwaa.
Zuio la usafirishaji wa viumbe hai, inawezekana wazi kulikuwa na kasoro kubwa, lakini inakuwaje jambo hili linachukua muda mrefu kiasi hiki?
Tunajiuliza kwa sababu wananchi ambao wanategemea biashara hii wameshindwa kuendeleza maisha yao ya kila siku.
Tumelazimika kusema haya, baada ya timu ya wahariri wa vyombo vya habari kutembelea milima ya asili ya Amani na kusikiliza kilio cha wananchi ambao walikuwa wananufaika na mradi huo.
Meneja Mradi wa vipepeo, Amir Sheghembe aliwaambia wahariri na waandishi waandamizi kuwa miradi ya ufugaji wa vipepeo ilibuniwa ili kuwaepusha wananchi na kufanya shughuli za uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji miti ya mbao kutoka kwenye msitu huo .
Tunakubaliana na meneja huyo, kuwa kama kweli wananchi wangeachwa wakaingia kwenye msitu huo, basi uharibu ungekuwa mkubwa, jambo ambalo lingesababisha kupoteza uhalisia wake.
Ni ukweli usiopingika kwamba zuio hili limesababisha mradi huu kuyumba, kwani wananchi wamekosa fedha na Serikali imekosa mapato kwa takribani miaka yote hiyo.
Meneja huyo, anasema wakati wa mauzo ya vipepeo, wananchi walikuwa na uhakika wa kupata mapato karibu ya asilimia 60 ya  mauzo huku, asilimia 10 zikirudi kwa ajili ya kusaidia miradi ya maendeleo kwenye vijiji husika.
Jambo hili si dogo, wananchi wamepoteza fedha nyingi ambazo zingewasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku, ikiwamo kusomesha watoto, kujenga makazi bora tofauti na ilivyo sasa.
Sisi MTANZANIA, tunamshauri Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe na wasaidizi wake kupitia upya uamuzi huu ili kuwasaidia wananchi wengi wa maeneo haya ambao maisha yao kwa kiasi kikubwa yanategemea uuzaji wa vipepeo nje ya nchi.
Kwa kufanya hivyo, kutakuwa kumefungia milango mipya kwa Serikali na wananchi kuingiza fedha za kigeni kama ilivyokuwa hapo awali, lakini pia kusaidia maisha ya wananchi hawa ambao kwa namna moja au nyingine wanaonekana wazi kukata tamaa.
Ni matarajio yetu kwamba jambo hili litapata ufumbuzi haraka iwezekanavyo ili Tanzania ya viwanda ianzie kwa mwananchi mmoja mmoja, kisha isambae kwa watu wote.