Na GRACE SHITUNDU, DAR ES SALAM
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amesifia hatua iliyofikiwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kudai imeimarisha nguvu ya upinzani tofauti na awali.
Zitto ambaye pia ni Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, aliyasema hayo wakati wa mahojiano maalumu katika kipindi cha Luninga cha 360 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds.
Alisema kuwapo umoja huo, unaoundwa na vyama vinne vya Chadema, CUF, NCCR- Mageuzi na NLD kumeimarisha upinzani, licha ya kukabiliana na changamoto chache.
“Jambo lolote la umoja linakuwa na nguvu, kunaweza kukawa na udhaifu, naweza kusema ni hatua kubwa ambayo umoja huo umefika,” alisema.
Akizungumzia sababu zilizofanya chama chake kushindwa kujiunga na umoja huo, Zitto alisema ilitokana na kutofautiana katika misingi waliojiwekea.
“Katika chama chetu tulijiwekea misingi ambayo tulianza kuingia kwa kuweka Azimio la Tabora ambalo lilimtaka kila mwanachama aliyetaka kugombea kutangaza kwa wananchi mali na madeni aliyonayo misingi hiyo ndiyo iliyotufanya tushindwe,”alisema Zitto.
Hata hivyo, alisema kuna baadhi ya mambo wanashirikiana na Ukawa. “Kuna mambo ambayo nawaunga mkono na wao wananiunga mkono,kuna mambo kama hayastahili siwezi kuwaunga mkono,”alisema.
Akizungumzia mgogoro unaondelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF), Zitto alisema ni changamoto zilizopo ndani ya katiba ya chama hicho ambazo zinasababisha kufifisha nguvu ya kudai ubakaji wa demokrasia uliofanyika visiwani.
“Ni vyema wazee wa chama na viongozi wakakutana na kutatua mgogoro huo kwa kuwa umekuwa ni chanzo cha kufifisha nguvu ya kudai ubakaji wa demokrasia uliofanyika visiwani Zanzibar.
“Pia nawashauri viongozi wa vyama vingine kutokuingilia mgogoro huo kwa kuwa upande fulani hali hiyo inazidisha mpasuko huku upande huu ukiona wao ndo halali na hawa haramu.
“Katika mahojiano wanayofanya viongozi wa pande zote mbili na vyombo vya habari hakuna anayezungumzia suala la demokrasia ya Zanzibar zaidi ya kuzungumzia mgogoro huo,” alisema Zitto.
Kuhusu mwenendo wa Serikali ya Rais Dk.John Magufuli, Zitto alisema ina mambo mazuri ambayo anayaunga mkono, lakini yapo yamengine ataendelea kuyakosoa.
“Mimi tangu niwe mbunge nimekuwa nikipinga ufisadi sasa kama Rais anashughulika mambo kama hayo, lazima nitamuunga mkono,yapo mengine sikubaliani nayo na sitakuwa na woga wa kumkosoa,”alisema