KAMATI ya Katiba na Sheria ya Chama cha ACT–Wazalendo,inatarajia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ya Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Kumi na Tano ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 2016, kuhusu masuala ya mafuta na gesi asilia Zanzibar ili kuipa mamlaka kamili.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe, alisema hoja hiyo ataiwasilisha yeye mwenyewe.
Alisema tayari amewasilisha barua kwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila juu ya azma yake.
Alisema Oktoba8, mwaka huu, chama chake kilifanya mkutano mkuu wa kidemokrasia uliolenga kujadili masuala mbalimbali yanayohusu Taifa, ambao pamoja na mambo mengine ulitoa maazimio kadhaa ya kisera juu ya chama chake, ikiwamo suala la kuibua upya mchakato wa Katiba mpya.
Alilitaja jambo jingine kuwa ni Sheria Mpya ya Usimamizi, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ili kuanzisha Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPDC) ambayo itashiriki shughuli za utafutaji na uendelazaji wa mafuta na gesi asilia kwa niaba ya Serikali ya Zanzibar.
“Sheria husika ilitungwa na kupitishwa mwezi huu na Baraza la Wawakilishi katika vikao vyake vilivyomalizika hivi karibuni.
“Mjadala mpana katika mkutano wetuulionyesha dhahiri pamoja na Baraza la Wawakilishi kutunga sheria hiyo, badoSMZ haipati uhalali wa kisheria na kikatiba juu ya usimamizi,utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia kwa upande wa Zanzibar,” alisema.
Alisema baada ya mjadala wa kina, walibaini sheria husika ni batili kwa kuwa inakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.