Na ANDREW MSECHU
KIONGOZI wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, amepeleka kile alichiokiita ushahidi wa tuhuma za rushwa inayodaiwa kuhusisha viongozi wa juu serikalini katika mradi wa uzalishaji chuma wa Mchuchuma na Liganga kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akizungumza baada ya kufika katika ofisi za Takukuru zilizopo Upanga, Dar es Salaam jana, Zitto, alisema aliwasilisha vielelezo hivyo kwa kuwaeleza zilizomfanya aamini kuwa ucheleweshaji wa mradi huo ni wa makusidi, unaofanywa na watendaji wa Serikali kwa ajili ya kufaidisha kampuni zinazoagiza bidhaa zinazotumika katika miradi ya chuma ikiwamo kampuni inayojenga reli ya kati na inayojenga bomba la mafuta kutoka Hoima hadi Tanga.
“Kwa hiyo nimewapa maelezo yangu na kuwapa nyaraka wanazopaswa kuzipitia kuthibitisha wasiwasi wangu na nitawaletea baadhi ya nyaraka kuthibitisha ucheleweshaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga ni wa makusudi, ambao una madhara kwa nchi, ambao mimi ninaona ni hujuma kwa nchi,” alisema.
Alisema amewapa changamoto kwa kuwaeleza wazi kuwa anaamini kwamba kumuita kwao ni kwa ajili ya kujaribu kudhibiti jambo hilo na si kupata ukweli wake na iwapo hawatalifanyia kazi suala hilo itakuwa haina maana.
Zitto aliyekaa katika ofisi hizo kwa zaidi ya saa mbili alisema aliwaeleza madhara yanayoweza kutokea kwa kuchelewa kuchukua uamuzi kunakofanywa na Serikali hasa kutokana na kuhusika moja kwa moja kwa wizara tatu, ambazo ni Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Fedha na Ofisi ya Rais, Ikulu.
Alisema suala hilo linaanza kwa taarifa za awali kuwa mwekezaji katika mradi huo anataka ahueni vingi lakini ndivyo hivyo hivyo ambavyo wakandarasi wa reli ya kati na wa bomba la mafuta Hoima-Tanga wamevipata.
“Hawa wote malighafi yao ni chuma na iwapo mradi wa Mchuchuma na Liganga ungeanza hawa wote wasingeagiza chuma kutoka nje. Na kutumia chuma kutoka ndani badala ya kutoka nje kwa fedha za kigeni ni hatua ambayo ingechangia ukuaji wa uchumi na hata kusaidia agenda ya viwanda,” alisema.
Hata hivyo, alisema ana wasiwasi kama Takukuru wataweza kuchunguza vyema suala hilo kwa kuwa linahusisha hadi viongozi wa juu ambao wengine hata sheria zinawapa kinga.
Katika hatua nyingine, Msemaji wa Takukuru, Doreen Kapwani, alisema ni kweli Zitto alifika katika ofisi zao kama alivyokuwa ameahidi na kutoa maelezo yake katika dawati la walalamikaji.
Wiki iliyopita Zitto alitoa tuhuma kwamba viongozi wa juu wa Serikali wanahusika katika rushwa ya kuzisaidia kampuni za nje kuuza chuma nchini na kuyumbisha kwa makusudi uendelezaji wa uzalishaji wa chuma cha Mchuchuma na Liganga kwa kumkwamisha mwekezaji aliyekuwa tayari kuzalisha chuma kwa ajili ya miradi ya ndani na ya nje.
Haya tena TAKUKURU, kazi kwenu – tunasubiri matokeo