Na TOBIAS NSUNGWE
MBUNGE wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo), amezidi kuzishauri mamlaka zinazohusika kulifanya zoezi la viongozi kutaja rasilimali zao na madeni kuwa la uwazi zaidi, ili kuimarisha vita dhidi ya ubadhirifu na ufisadi.
Zitto alitoa wito huo jana, katika taarifa yake kuuarifu umma kwamba amekwisha jaza fomu za rasilimali na madeni kama sheria inavyowataka viongozi kufanya hivyo kila ifikapo mwisho wa mwaka. Taarifa inaonesha kuwa, Mbunge huyo machachari alitoa tamko la rasilimali zake na madeni kwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi Desemba 27, 2016.
Mbunge huyo alisema kuwa, ibara ya 132(4) na (5) na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Sheria namba 13 ya mwaka 1995 inataka viongozi wote wa umma kujaza fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni. Tamko hilo huwasilishwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kabla ya mwisho wa kila mwaka.
Zitto amesisitiza uwazi katika kukamilisha zoezi hilo, huku akitolea mfano wa Uingereza na Canada, ambako alidai daftari la matamko ya Rasilimali na Madeni ya Viongozi lipo wazi kwa kila mwananchi kuona na huuzwa kwenye duka la vitabu la Bunge.
Katika taarifa yake hiyo, Zitto amerejea wito wake wa kumshauri Rais John Magufuli kusaidia kufanya mabadiliko makubwa ya Sheria ya Maadili ya Viongozi, ili kurejesha na kuboresha miiko ya viongozi katika kuimarisha vita dhidi ya ufisadi nchini.
Pia Zitto amemtaka Rais Magufuli kuweka wazi mshahara wake na pia aweke wazi mali, madeni na maslahi yake ya kibiashara ili awe mfano kwa viongozi wengine nchini.
“Ni matumaini yangu kwamba, itafikia wakati Daftari la Rasilimali na Madeni la Viongozi wa Umma litakuwa linawekwa wazi kwa umma ili wananchi waweze kujua mali, madeni na maslahi ya viongozi wao na pale ambapo kiongozi ametoa habari zisizo sahihi au kuficha mwananchi aweze kutoa taarifa kwenye Sekretarieti na Baraza la Maadili liweze kufanya kazi yake ipasavyo,” alisema Zitto.
Machi mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Angela Kairuki, alisema Serikali italipa kipaumbele suala la uhakiki wa mali za viongozi wa umma kwa kuiwezesha Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi kufanya kazi zake kwa ukamilifu kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma Na. 13 ya mwaka 1995.
“Suala la uhakiki wa rasilimali na madeni ya viongozi tutahakikisha linapewa kipaumbele katika Awamu hii ya Tano ya uongozi,” alisema.
Kwa mujibu wa Waziri Kairuki, Serikali itajitahidi kuongeza jitihada ili uhakiki wa rasilimali na madeni ya viongozi wa umma ufanyike, pamoja na kuiongezea Taasisi hiyo bajeti ya kutosha.
Hivi karibuni Rais alimteua Jaji Harold Reginald Nsekela kuwa Kamishina mpya wa Sekretarieti hiyo kuchukua nafasi ya Jaji Mstaafu Salome Kaganda, ambaye alistaafu hivi karibuni.