27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto aitwa Takukuru, aibuka na hoja nyingine

Na AGATHA CHARLES


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imemtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kufika ofisi za taasisi hiyo zilizoko Upanga jijini Dar es Salaam mapema ili kutoa ushirikiano wa taarifa aliyoitoa kuhusu kuwepo kwa rushwa katika mradi wa uzalishaji wa chuma –Liganga na Mchuchuma.

Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo kwa Vyombo vya Habari ilieleza kuwa  taarifa hiyo ya Zitto ilizilalamikia kampuni tatu za China, Urusi na Uturuki kuwa zimewahonga baadhi ya watendaji wa serikali kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Ofisi ya Rais.

“Taarifa hiyo inayalalamikia makampuni matatu ya chuma ya China, Urusi na Uturuki kuwa yamehonga baadhi ya watendaji wa serikali kutoka Wizara ya Fedha, Viwanda na Biashara pamoja na Ofisi ya Rais kwa lengo la kuchelewesha ukamilishaji wa mradi wa Mchuchuma na Liganga hadi hapo ujenzi wa mradi wa reli ya mwemndokasi-SGR utakapokamilika,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Brigedia Jenerali Mbungo katika taarifa hiyo alieleza kuwa kabla ya kutoa wito wa kumtaka Zitto kufika ofisi hapo, taasisi hiyo ilifanya jitihada za kuwasiliana naye kwa njia ya simu bila mafanikio.

Wakati Takukuru ikitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari saa 6:42  jana mchana dakika chache baadae Zitto aliibuka na kuandika kupitia akaunti yake ya Twitter akithibitisha kupata wito huo na kueleza kuwa atafika katika ofisi hizo.

Katika andiko lake hilo kupitia akaunti yake ya Zitto Kabwe Ruyagwa‏ aliitaka Takukuru kuwa tayari kusema hadharani atakayoyasema na kuchunguza atakayowaambia.

“Nitakwenda kwa roho nyeupe kabisa. Wawe tayari kusema hadharani nitakayoyasema na kuchunguza nitakayowaambia. Hujuma dhidi ya Mradi wa kimkakati wa #MchuchumaNaLiganga hazivumiliki na zinatoka juu kabisa. Poleni wana #KaziNabata jamaa wamenikurupua huko. Narudi batani. Ciao,” linasomeka andiko hilo la Zitto.

Katika taarifa yake Takukuru ilieleza kuwa lengo la kumtafuta Zitto ni kutaka kujiridhisha iwapo ni kweli ndiye aliyetoa taarifa hizo za tuhuma za rushwa.

“Lengo la kumtafuta lilikuwa ni kwanza, kujiridhisha iwapo ni kweli ndiye aliyetoa taarifa hiyo, pili ni kuhitaji ushirikiano wake katika kushughulikia suala hilo. Tunatoa taarifa hii kupitia vyombo vya habari kumwomba Zitto afike ofisi za T AKUKURU -Upanga Dar es Salaam iwezekanavyo ili tushirikiane katika kushughulikia suala hili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya taifa,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.

Brigedia Jenerali Mbungo pamoja na kuwashukuru wananchi kwa kutoa taarifa aliwataka kutumia njia sahihi na rasmi kuwasilisha malalamiko dhidi ya vitendo vya rushwa ili hatua stahiki za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja.

Taarifa iliyoisukuma Takukuru kumtafuta Zitto ni ile inayodaiwa kutolewa na mwanasiasa huyo juzi na kuanza kusambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii akieleza namna rushwa hiyo ilivyofanyika kwa lengo la kuwahonga watendaji hao ni kuhakikisha nchi hizo zinapata soko la chuma chao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles