NA DK. CHRIS MAUKI
Makosa ambayo Wazazi au walezi hufanya katika kutoa adhabu (Disciplining Mistakes) Kudekeza (Lax Parenting). Hii inatokea pale mazi au wazazi wanaposhindwa kusimamia adhabu waliyoiweka, maranyinine wanasema kwa mdomo tu pasipo matendo, na taratibu mtoto anawasoma wazazi wake kuwa ni mbwa wasio meno (toothless dogs). Mtoto hapa huweza kujitetea, kulalama na kupindisha pindisha sheria au amri zilizowekwa ili tu kukwepa adhabu, na maranyingi hufanikiwa. Mzazi/mlezi unatakiwa kuwa imara na mwenye msimamo kusimamia ulichokisema katika kuadhibu. Mama na baba wote wawe na msimamo mmoja, sio mmoja anakuwa tayari kuadhibu na mwingine anatetea mtoto kutoadhibiwa. Au mama anasema tu kuhusu kuadhibu na kuja kushitaki kwa baba, kama vile yeye sio mzazi bali msaidizi wa kazi. Kama umedhamiria kutoa adhabu, basi adhabu hiyo itolewe, labda tu kuwe na msamaha ambao pia unaeleweka na utamsaidia anayesamehewa siyo ajione kuwa kasamehewa kwa sababu hakustahili adhabu.
Kosa la pili ni lile linalofanywa na baadhi ya wazazi kwa kusifia au kuchochea tabia isiyofaa bila wao kujua. Kwa mfano; mtoto anapofanya kituko, badala ya kumkaripia utakuta anatazamwa na watu wataitana kuja kumuona anachofanya. Hii humfanya kujisikia jasiri kwa kushika hisia za wengi, uwezekano upo mkubwa kuwa tabia hiyo itandelea. Mfano mwingine katika hilo ni pale mtoto anapoelezea kupigwa na mwenzake na mzazi/mlezi anamwambia “na wewe mpige”, “kunja ngumi” “mtukane na wewe” huku ni kumharibu kabisa mtoto. Mzazi/mlezi adhibu kila tabia mbovu na chochea au hamasisha kila tabia iliyonjema indelee.
Ukali wa maneno matupu (Verbosity). Hili ni kosa la mzazi hasa pale wanapopayuka au kuropoka au kuongea sana wakati anapotaka kutoa adhabu. Mfano, mtu anasema “mimi nimeshasema, hapa hapatoshi leo, lazima nimwonyeshe adabu”. Huu siyo wakati wa kutunga mashairi ya adhabu ila ni wakati wa kuadhibu. Tumia maneno machache, pasipo mihemko mingi wakati unaadhibu, elezea kwa kifupi juu ya adhabu unayotaka kuitoa, na msimamo wako na kumhimiza kutenda au kufanya kile kinachombidi.
Kuzidiwa na hisia za hasira (Over reactivity). Mzazi au mlezi, wakati wa kuadhibu aidha kwa kitendo au kwa maneno usizidiwe na hasira au na hisia kali, jitahidi kutuliza hasira zako, maneno yako na sauti yako kwa mtoto au yule anayeadhibiwa yawe ya kawaida na yenye ujumbe wa kueleweka na sio vitisho vitupu. Kumaanisha kwa mzazi hakupimwi na jinsi unayvo mpayukia au kumropokea anayeadabishwa, pia hakupimwi na jinsi unavyomshika na kumtingishatingisha au kumsukuma na kumuahidi vitisho bali kwa maneno ya chini, utulivu na sauti inayothibitisha msimamo wako.
Adhabu
Adhabu ni tendo au neno lolote linalotumika au kutolewa kufuatia tabia isiyofaa kwa kusudi la kuipunguza au kukomesha tabia hiyo.