NA MWANDISHI WETU, UNGUJA
RAIS wa Zazibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema jumla ya Sh bilioni 2.8 zimekusanywa kwa ununuzi wa madawati shule za msingi na sekondari za Serikali.
Akizungumza mjini hapa jana wakati wa hafla ya kuhamasisha uchangiaji madawati kwa shule za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Dk. Shein, alisema bado wadau wengine wanaendelea kuchangia.
Alisema miongoni mwa fedha hizo ni Sh milioni 500 zilizotolewa katika hafla hiyo na Sh bilioni 1.8 ni ahadi na Sh milioni 483 zilishakusanywa hadi mwishoni mwa Machi, mwaka huu.
Dk. Shein alisema elimu ni suala lenye historia kubwa kwa mwananadamu na linagusa maendeleo yote duniani.
Alisema jitihada kubwa zimechukuliwa na Serikali tangu mwaka 1964, licha ya changamoto kuwapo na ndiyo maana wamechukua uamuzi wa kuwaita viongozi wake wote katika hafla hiyo ili na wao wachangie madawati.
“Hatuwezi kuongoza Serikali kwa zao la karafuu peke yake na ndiyo maana tumeona haja ya kuongeza mambo mengine ya kuimarisha uchumi wetu, baada ya Mapinduzi Zanzibar idadi yetu tulikuwa laki tatu, lakini leo tuko milioni moja na laki nne,” alisema.
Pia alisema azma ya Serikali kwa hapo baadaye ni kuhakikisha kuwa shule za sekondari nazo hazitokuwa na michango ya aina yoyote na kusisitiza kuwa dhana ya elimu bure ni kuhakikisha mambo yote yanasimamiwa na Serikali.
Alimshukuru Rais Dk. John Magufuli kwa kuwapatia mgawo wa madawati, ikiwa ni mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kukabiliana na tatizo la madawati kwa shule za Zanzibar.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alisema pamoja na juhudi kubwa ya SMZ kuongeza bajeti ya wizara kila mwaka na kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017 imefikia asilimia 20 ya matumizi ya Serikali, lakini bado baadhi ya changamoto zipo, ikiwamo uhaba wa madawati.
Alisema hivi sasa wanatumia Sh milioni 31 kila mwezi kwa gharama za uji na madaftari kwa shule za maandalizi na msingi na hivi sasa wazazi hawapaswi kugharamia kununua madaftari kwa matumizi ya watoto wao.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kuna uhaba wa madawati 41,871 kwa ajili ya shule za msingi na viti 43,489 na meza 43,489 kwa ajili ya shule za sekondari za Serikali. Licha ya kutoa fedha kila mwaka kupitia kodi ya bandari, lakini kiwango cha fedha kinachokusanywa hakilingani na ongezeko kubwa la wanafunzi,” alisema.