23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

MWIGULU AWATAKA POLISI KUWATENDEA HAKI RAIA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, akizindua Programu ya Mafunzo ya Uongozi kwa maofisa wa Jeshi la Polisi, Dodoma yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi kwa kushirikiana na Chuo cha Aalto cha Finland. Kulia ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu na kushoto ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja.

Na SARAH MOSES – DODOMA  

JESHI la Polisi limetakiwa kutenda haki kwa wananchi wake na si kuwaongoza watu kama wanyama.

Agizo hilo limetolewa mjini hapa juzi na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya uongozi kwa viongozi wa ngazi za juu wa jeshi hilo, yanayotolewa na Chuo cha Aalto Executive Education Academy (AEE) cha nchini Finland.

Mwigulu alisema polisi ni mojawapo ya taasisi inayolaumiwa na kwamba licha ya kuwa kuna mambo mengine mazuri wanayafanya, lakini jamii haiyasifii.

“Licha ya jeshi letu kufanya vizuri, lakini jamii imekuwa ikiangalia zaidi upande wa makosa mnayoyafanya, hivyo basi mnatakiwa kuwa makini zaidi,” alisema.

Alisema upungufu huo unasababishwa na kutokuwa na weledi na ujuzi wa kutosha katika uongozi.

“Viongozi wengi huwa wanawaza kuingia katika madaraka, lakini siyo kutoka. Wamesahau kuwa kwenye uongozi wakikaa watu watawaona wambea na kuwataka waachie madaraka.

“Vile vile ukiingia mkataba mpya wa uongozi, watu watakuombea ufe na ikitokea ukastaafu, basi hapo utapendwa na kila mtu kwa sababu watakutakia maisha yaliyo mema,” alisema.

Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki, alisema viongozi wote wanatakiwa kupewa elimu ya uongozi ikiwamo ya kuwaandaa viongozi wengine.

“Pamoja na Jeshi la Polisi kuwa la kwanza kupata mafunzo hayo, hata viongozi wa kisiasa wanatakiwa kupewa elimu hiyo ya uongozi kwa sababu itawasaidia,” alisema.

Alisema analo jukumu la kuhakikisha watumishi wa umma wanafanya kazi kwa weledi na maadili.

Kwa upande wake, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu, alisema karne ya sasa inahitaji viongozi wenye uwezo mkubwa kwa sababu jamii imeelimika zaidi kuliko zamani.

Alisema mabadiliko hayo kwa jamii yamesababisha changamoto za kukithiri kwa uhalifu na kusema kuwa nchi hazina mipaka ya asili kama zamani hali inayosababisha ugumu wa kuwatawala watu.

“Wahalifu wamekuwa wakifanya uhalifu zaidi kwa sasa kuliko zamani na kusema kuwa mazingira hayo yanahitaji aina mpya ya uongozi ikiwemo kiuchumi, kisiasa na kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles