28.4 C
Dar es Salaam
Friday, February 23, 2024

Contact us: [email protected]

Zana haramu za uvuvi zakamatwa Sikonge

Na Allan Vicent, Tabora

Halmashauri ya wilaya ya Sikonge Mkoani Tabora imekamata zana haramu za uvuvi zenye thamani ya zaidi ya sh mil 100 na watu 7 waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivyo wanashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kusababisha uharibifu mkubwa wa viumbe maji.

Akizungumza na vyombo vya habari leo Desemba 19, Mkuu wa wilaya hiyo Peresi Magiri alipongeza halmashauri hiyo kupitia Idara ya Mifugo na Uvuvi kwa kufanya doria za mara kwa mara katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti vitendo hivyo. 

Amebainisha kuwa watuhumiwa 7 wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa ili sheria ichukue mkondo wake.

Ameongeza kuwa matumizi ya zana haramu za uvuvi ni hatari kwa rasilimali zilizoko katika mito na mabwawa kwa sababu hupelekea kukosekana kwa kitoweo cha samaki hivyo akatoa wito wa kukomeshwa kwa vitendo hivyo mara moja.  

Magiri ameitaka Idara ya Mifugo na Uvuvi kuendeleza doria hizo ili kuhakikisha zana haramu zote ikiwemo makokoro, nyavu, vyandarua na vinginevyo vinakamatwa na kuteketezwa ili kukomesha tabia hiyo.

Aidha, amewataka Wataalamu wa Idara hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili wajue vifaa vinavyoruhusiwa na visivyoruhusiwa kwenye uvuvi na athari za zana haramu kwa ustawi wa viumbe maji, huku akiwashauri kuhakikisha vifaa bora vya uvuvi vinapatikana kwa urahisi na kwa bei nzuri.

Awali, Kaimu Mkuu wa Idara hiyo, Mipawa Majebele alisema kuwa watuhumiwa hao walikamatwa kutokana na doria iliyofanyika katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kudhibiti vitendo hivyo ambapo jumla ya nyavu haramu 276 na mashine 3 za kuvuta maji vyote vikiwa na thamani ya zaidi ya sh mil 100 vilikamatwa.

Amesisitiza kuwa doria hiyo ni muhimu sana kwa kuwa inasaidia kuokoa viumbe maji vilivyoko katika mito na mabwawa wilayani humo kwa kuwa ni rasilimali muhimu ambayo huchochea uchumi wa wananchi kupitia uuzaji samaki.

Amebainisha kuwa doria hiyo imesaidia sana kuongeza uzalishaji wa viumbe maji hivyo kutengeneza ajira kwa wavuvi 1219 ambao wameweza kujipatia kipato cha sh mil 100 na kuiwezesha halmashauri kuingiza kipato cha zaidi ya sh mil 33.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Tito Luchagula amesema kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu na wataweka utaratibu mzuri utakaosaidia wavuvi kufanya shughuli zao pasipo kubughudhiwa na mtu.

Amesisisitiza kuwa hatua kali zitaendelea kuchukuliwa kwa wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo huathiri kwa kiasi kikubwa mapato ya halmashauri ikiwemo kupunguza kitoweo cha samaki katika wilaya hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles